
Arusha. Mahakama Kuu Masijala ndogo ya Kigoma, imemuhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa, Sudy Omary baada ya kumkuta na hatia ya kumuua Joseph Misigaro.
Imeelezwa kuwa Omary alimpiga Misigiro makofi mawili, hali iliyosababisha kuvunjika kwa fuvu la kichwa. Matokeo ya jeraha hilo yalikuwa kuganda kwa damu kwenye ubongo, jambo lililosababisha uvimbe kichwani na hatimaye kusababisha kifo chake.
Omary alimshambulia Joseph kwa kumpiga makofi mawili baada ya mke wa Joseph, ambaye alikuwa shahidi wa kwanza katika kesi hiyo, Ashura Eliud, kupewa Sh3,000 na Sudy kwa ajili ya kuvuna mahindi ambapo hakuifanya kazi hiyo kwa wakati na mtuhumiwa alienda kumuuliza.
Ilidaiwa kuwa Joseph alimwambia mshitakiwa kuwa mkewe atafanya kazi hiyo Jumatatu, jibu linaonekana kutomridhisha mshitakiwa ambapo aliamua kumpiga makofi mawili ambayo yalimfanya Joseph adondoke chini na kupoteza fahamu na kufariki akiwa hospitalini.
Hukumu hiyo ilitolewa Septemba 20, 2024 na Jaji John Nkwabi, ambaye alisema upande wa mashitaka umethibitisha bila kuacha shaka.
Akisoma hukumu hiyo, Jaji Nkwabi alisema mshitakiwa ametiwa hatiani kama alivyoshitakiwa kwa kosa la mauaji na upande wa mashitaka ulikuwa na mashahidi saba huku utetezi ukiwa na mashahidi wanne.
Akiendelea kupitia ushahidi, Jaji Nkwabi alisema ukweli ambao haupingiki ni kuwa Joseph amekufa kifo kisicho cha kawaida na hukumu hiyo imezingatia kwamba mshitakiwa ndiye aliyesababisha kifo cha marehemu huyo.
“Nimejiridhisha kuwa Ashura alisema ukweli aliposema aliona mtuhumiwa akimpiga makofi marehemu aliyeanguka chini, alipiga kelele na mtuhumiwa kukamatwa katika eneo la tukio,”alisema Jaji
Kuhusu nia ya kusababisha kifo, Jaji Nkwabi alisema ushahidi unaonyesha mshitakiwa alimpiga marehemu mara mbili kichwani, sehemu ya mwili iliyo hatarini na zaidi ya hayo fuvu la kichwa lilivunjika, jambo linaloonesha nguvu kubwa ilitumika.
“Ilikuwa ni kama adhabu kwa marehemu, pengine, mtuhumiwa alifikiri kuwa marehemu ndiye aliyesababisha kazi hiyo kuchelewa kufanyika. Kwa mjadala huo hapo juu unathibitisha wazi mtuhumiwa alikuwa na nia ya kumuua marehemu,”amesema Jaji.
Jaji huyo alihitimisha kuwa Mahakama inamtia hatiani kwa kosa la mauaji kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, na kumuhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.
Kwa mujibu wa shahidi wa kwanza wa mashitaka ambaye ni mke wa marehemu, Ashura Eliud, alidai siku ya tukio Mei 21, 2023, katika Kijiji cha Kumwambu kilichopo wilayani Kibondo mkoani Kigoma, mshitakiwa alimshambulia mumewe kwa kumpiga makofi mawili.
Omary anadaiwa kukamatwa eneo la tukio baada ya kelele iliyopigwa na Ashura, miongoni mwa waliomkamata ni pamoja na Mwenyekiti wa kitongoji ambapo walikwenda Polisi kuchukua fomu ya polisi namba tatu (PF3), kwa ajili ya matibabu.
Ilidaiwa Mei 22, 2023 saa tano asubuhi, Misigaro alikufa mbele ya mtoto wake (Boazi Joseph), katika Hospitali ya Wilaya ya Kibondo.
Ashura alidai sababu shambulio hilo ni baada ya yeye (Ashura) kupokea Sh3,000 kutoka mshitakiwa kwa ajili ya kuvuna mahindi ambapo Ashura hakuifanya kazi hiyo kwa wakati na mtuhumiwa alienda kumuuliza.
Ilidaiwa kuwa Misigaro alimwambia mshitakiwa kuwa mkewe atafanya kazi hiyo Jumatatu, jibu linaonekana kutomridhisha mshitakiwa hivyo akampiga makofi mawili ambayo yalimfanya Joseph adondoke chini, kupoteza fahamu na kufariki akiwa hospitalini.
Utetezi wake
Katika utetezi wake Omary alikana kutenda kosa hilo na kudai siku ya tukio akitoka kwenye kazi yake ya kuchimba mawe, alikutana na watoto wawili wa marehemu waliomshika na kumtaka arudi katika eneo ambalo marehemu alikuwa amelala.
Alidai kushangaa kushitakiwa kwa kosa la mauaji na kuiomba Mahakama hiyo imuachilie huru.