
Arusha. Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, imemhukumu Patrick Elias (33) kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela kwa kosa la kumuua mkewe bila kukusudia, baada ya mkewe kurejea nyumbani usiku akiwa chakari kwa ulevi.
Jenipher Patrick, alifariki dunia baada ya kipigo cha mumewe Julai 25, 2024 katika kijiji cha Bunyagongo, Kata ya Nshamba, Muleba Mkoa wa Kagera, kutokana na mumewe kuchukizwa na tabia yake ya kurejea usiku wa manane akiwa mlevi.
Hukumu hiyo imetolewa Februari 11,2025 na Jaji Gabriel Malata, baada ya mshitakiwa kupatikana na hatia ya kosa la kuua bila kukusudia.
Jaji amesema haki itaonekana imetendeka, kama Patrick ataenda jela miaka mitatu.
Kulingana na maelezo ya upande wa mashtaka, siku ya tukio majira ya jioni, mshtakiwa huyo alirejea nyumbani na hakumkuta mkewe.
Aliendelea kubaki nyumbani hadi usiku wa manane aliposikia sauti ya mkewe akigonga mlango akaenda kumfungulia, na ndipo akabaini kuwa mkewe analala chini kutokana na hali ya ulevi wa kupindukia aliyokuwa nayo.
“Mshtakiwa alichukizwa na tabia ya mkewe ya kurejea nyumbani usiku wa manane akiwa mlevi, alimshambulia Jenipher sehemu mbalimbali za mwili wake kwa kutumia silaha ya jadi inayoitwa ‘kiosho’,” amesema Jaji.
Akirejea maelezo hayo ya ushahidi wa Jamhuri, Jaji Malata amesema baada ya kumshambulia, mshtakiwa alimchukua mkewe na kumwingiza ndani ya nyumba waliyokuwa wakiishi na kumpatia chakula na baadaye wakaenda kulala.
Muda wa asubuhi, mshtakiwa alimwamsha mkewe kwa kujaribu kumuita, lakini hakuwa anaitika, ndipo akagundua kuwa mkewe amefariki dunia.
Kwa hofu aliyoipata, mshtakiwa alienda kumuita jirani yake aitwaye Sadoki Revelian na kumwelezea kilichotokea kisha akakimbia kutoka eneo la tukio.
Revelian ambaye ndiye alikuwa baba mwenye nyumba na mwajiri wa mshtakiwa, aliingia ndani ya chumba walichokuwa wakiishi msitakiwa na mkewe na kushuhudia mwili wa Jenipher ukiwa umelala kitandani na kufunikwa na shuka.
Jirani huyo akatoa taarifa polisi ambao walifika eneo la tukio wakiambatana na ofisa tabibu na baada ya uchunguzi wa mwili wa marehemu, ilibainika sababu ya kifo chake ni kuvuja damu ndani ya mwili kutokana na kupasuka kwa fuvu.
Februari 5, 2025, kulifanyika usikilizwaji wa awali ambapo upande wa Jamhuri uliwakilishwa na wakili wa Serikali, Matilda Assey kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashitaka (NPS) wakati mshitakiwa alitetewa na wakili wa kujitegemea Pereus Mutasingwa.
Baada ya mshtakiwa kusomewa shitaka la kuua bila kukusudia, mshtakiwa alijibu “Ni kweli nilisababisha kifo cha Jenither Patrick bila kukusudia,” na hata aliposomewa maelezo ya namna kosa lilivyotendeka, alikubali kuwa ni sahihi.
Baada ya kukiri huko, mahakama ilimtia hatiani kwa kosa la kuua bila kukusudia ambapo wakili Assey alisema ingawa Jamhuri hawana kumbukumbu za makosa mengine ya nyuma, aliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa sababu tano.
Moja ni ili iwe fundisho kwa wengine, pili mshtakiwa alitumia silaha kumpiga mtu ambaye hakuwa na kitu chochote, tatu shambulio lilikuwa eneo baya, nne ni matumizi ya nguvu na tano marehemu alikuwa mlevi na mtu asiyejiweza.
Hata hivyo, akiomba huruma ya mahakama, Wakili Mutasingwa aliyekuwa akimtetea, aliomba mteja wake apewe adhabu ndogo kwa kuwa bado ni kijana na ana mtoto mmoja anayeishi na bibi yake na wote wawili wanamtegemea yeye.
Pia, alisema mama wa mshtakiwa ana umri wa miaka 83, hivyo anamtegemea mshtakiwa kwa kila kitu, kitendo cha mke kurudi usiku wa manane ilikuwa ni tabia mbaya na lengo la mshtakiwa haikuwa kumuua, bali kumpa onyo.
Alijenga hoja kuwa pamoja na marehemu kuwa mlevi, mumewe alimbeba na kumpeleka ndani na kulala naye hadi asubuhi alipobaini amekufa, hakuisumbua polisi wala mahakama kwa kukiri kosa, na amekaa mahabusu miezi saba.
Katika hukumu yake, Jaji amesema adhabu ya mtu aliyetiwa hatiani kwa kuua bila kukusudia ni kifungo cha maisha jela ila mahakama inaweza kuangalia adhabu ndogo kulingana na mazingira ya kesi husika hadi kusababisha mauaji.
Jajji Malata amesema kuondoa maisha ya mtu kwa kukusudia ni kosa kubwa chini ya sheria na adhabu yake ni kunyongwa hadi kufa kwa mujibu wa kifungu cha 197 cha Kanuni ya Adhabu kama ilivyofanyiwa marejeo na Bunge mwaka 2022.
“Hata hivyo, kuna mazingira, ambapo kifo hutokea bila kupangwa kama uzembe, uchochezi, mapigano, kutetea haki au kujilinda. Matukio hayo yanaweza kusababisha mauaji, zaidi ya hayo jinsi mauaji yalivyotokea inakuwa mojawapo ya mambo ya kuamua katika kutoa hukumu,” amesema Jaji Malata.
“Pia, asili ya silaha kutumika, nguvu inayotumika katika kuua, uzito wa jeraha, mwenendo wa mshtakiwa kabla, wakati na baada ya kutenda kosa ni miongoni mwa mambo mengine yanayopaswa kuzingatiwa na mahakama katika kutathmini na kutoa adhabu ifaayo kwa misingi ya kesi,”aliongeza kusema Jaji.
Jaji huyo amesema mahakama hiyo baada ya kuchukua mazingira yote, inaona kwamba marehemu alikuwa amelewa, alikuwa ni mwanamke, hakuwa na silaha na Patrick alimshambulia kwa silaha ya kienyeji ijulikanayo kama kiosho.
Pia mshtakiwa alitumia nguvu nyingi kumpiga kichwa na kusababisha majeraha makubwa ya kichwa na baada ya kuchambua masuala hayo, Jaji huyo amesema mahakama hiyo inamhukumu Patrick adhabu ya kifungo cha miaka mitatu jela kwa kuua bila kukusudia.