
Arusha. Mahakama ya Rufani imebariki adhabu ya kunyongwa hadi kufa aliyohukumiwa Sungwa Mpelwa, ambaye alikutwa na hatia ya kumuua dada yake Mbula Mpelwa, kisa kudaiwa Sh600,000.
Sungwa alishtakiwa kwa tuhuma za mauaji kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu, ikidaiwa Machi 27, 2016 katika Kijiji cha Pugu, Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, alimuua dada yake, baada ya kukataa kurejesha Sh600, 000 alizokopeshwa na Mbula kutoka kwenye mahari kwa binti yake.
Rufaa hiyo inatokana na hukumu ya Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, ya Machi 11, 2022.
Mahakama ya Rufani iliyoketi Shinyanga chini ya majaji watatu Lugano Mwambando, Sam Rumanyika na Amour Khamis, imetupilia mbali rufaa ya Sungwa, baada ya kujiridhisha kuwa upande wa mashtaka ulithibitisha mashtaka hayo pasipo kuacha shaka.
Hukumu hiyo iliyotolewa Novemba 6, 2024 na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa mahakama, ikisisitiza kuwa uamuzi wa mahakama kuu ulikuwa sahihi kwa mujibu wa sheria.
Hukumu hiyo imezingatia sababu za kukata rufaa, endapo taarifa ya maelezo ya ziada ya kimahakama na maelezo ya onyo yalitumika kimakosa kumtia Sungwa hatiani na endapo kesi hiyo ilithibitishwa bila kuacha mashaka yoyote.
Jaji Khamis anasema akisoma hukumu hiyo, kuwa kumbukumbu zinaonyesha kuwa wakati shahidi wa kwanza anataka kutoa kielelezo cha kwanza (maelezo ya ziada ya ungamo), wakili wa mrufani hakuwa na pingamizi lolote.
“Hiyo inamaanisha, mrufani ambaye aliwakilishwa kikamilifu, katika kipindi chote cha kesi hakukana ukweli au uhalali wa hati iliyomshtaki. Kwa hivyo, tumeridhika kuwa kielelezo hicho hakikuhitaji uthibitisho,” anasema Jaji Khamis.
Jaji huyo ameeleza kuhusu kielelezo cha pili (maelezo ya onyo ya mrufani), kumbukumbu zinaonyesha kuwa shahidi wa pili alipotaka kuwasilisha kielelezo hicho, pingamizi liliwasilishwa ila mwisho wa kesi hiyo ndogo, mahakama iliona maelezo hayo ni ya kweli na kutupa pingamizi hilo.
Kuhusu endapo upande wa mashtaka ulithibitisha kesi bila shaka, Jaji huyo anasema mahakama iligundua marehemu aliuawa kwa kukatwa na panga na chanzo cha kifo kwa mujibu wa ripoti ya uchunguzi wa kifo ni kutokwa na damu nyingi.
Kuhusu madai ya wakili wa mrufani ya kuwepo kwa mkanganyiko wa tarehe ambayo mrufani alikamatwa na kurekodi maelezo ya ziada ya mahakama, amesema:
“Suala hili halipaswi kutufunga kwani lilishughulikiwa vya kutosha na mahakama ya awali katika uamuzi wake ulioonyeshwa ukurasa wa 130 wa rekodi, hivyo kutofautiana si jambo la maana na halikupindisha ungamo la mtuhumiwa kuhusu viambatisho vya mauaji, na kwa sababu zilizotajwa tunatupilia mbali rufaa kwa ujumla wake,” amesema.
Keshi ya awali
Awali kesi iliposikilizwa Mahakama Kuu, upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi watano, akiwemo Saka Nindwa, mtoto wa marehemu, aliyedai kuwa Machi 27, 2016 alisikia mlango ukigongwa na watu wawili walivamia wakiwa wameshika tochi na kumkata marehemu kwa panga.
Shahidi wa tatu alidai kumsikia marehemu akipiga kelele akisema, “Sungwa nimekukosea nini unaniua hivi?”
Baada ya kauli hiyo, shahidi alidai wauaji walizima tochi na kuondoka eneo la tukio.
Shahidi huyo alidai wauaji hao walikuwa wamevalia makoti marefu yaliyozuia kutambuliwa na hakusikia sauti yoyote aliyoifahamu wakati wa tukio hilo, ingawa alisisitiza kuwa alimsikia marehemu akimtaja mrufani wakati wa shambulio hilo na kuwa wawili hao hawakuwa na maelewano mazuri.
Shahidi wa nne ambaye ni mkwe wa marehemu, Tabu Dotto, alidai kulikuwa na ugomvi kati ya mrufani na marehemu na kuwa mrufani alikataa kurejesha Sh600,000, zilizomkopesha ambazo zilitokana na mahari kwa binti ya marehemu.
Shahidi huyo alidai kuwa katika kumpa Mbula hofu ili aache kudai fedha hizo, Sungwa alimtumia barua bila kutaja jina lake, ikiwa na picha ya panga, ikimaanisha kuwa yuko mbioni kushambuliwa na kuwa tukio hilo liliripotiwa kwa uongozi wa eneo hilo.
Shahidi wa tano ambaye ni askari polisi 8038, PW5 Koplo Aloyce, aliyemkamata mrufani huyo katika Kijiji cha Nzela mkoani Geita, pia alidai mahakamani kuwa Mbula alipomtembelea mwaka 2016 alimwonyesha barua ambayo haikutajwa jina lake, iliyodaiwa kuandikwa na mrufani.
Shahidi wa pili, Sanjenti James alidai katika maelezo ya onyo, mrufani huyo alikiri kushirikiana na mtoto wake (Msafiri Sungwa) kumuua marehemu.
Ripoti ya uchunguzi wa mwili ilionyesha kuwa marehemu alikuwa na majeraha mengi ya kukatwa kichwani, kuvunjika kwa fuvu la kichwa na chanzo cha kifo chake ni kuvuja damu nyingi.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa mrufani huyo akihojiwa mbele ya mlinzi wa amani, alikiri kutenda kosa hilo na maelezo hayo yalipokelewa mahakamani kama kielelezo cha kwanza.
Katika utetezi wake, Sungwa alikiri kuandika maelezo ya onyo ila alikana kumuua dada yake na kuwa hakuhudhuria mazishi yake, ingawa alikamatwa baada ya mazishi hayo.
Alidai kuwa hakuwahi kumtembelea marehemu na watoto wake hawakumfahamu lakini alikiri kuwa dada yake alimripoti katika kituo cha polisi kuhusiana na barua ya vitisho ambayo alikana kuhusika nayo.
Licha ya utetezi huo, Mahakama Kuu ilikuta na hatia na kumhukumu kunyongwa hadi kufa.
Baada ya kutoridhishwa na hukumu hiyo, Sungwa alikata rufaa akiwa na sababu mbili, kwamba kesi yake haikuthibitishwa bila kuacha shaka na kuwa Jaji kukosea kisheria kutegemea taarifa ya ziada ya kimahakama na maelezo ya onyo ambayo hayakuthibitishwa.
Katika rufaa hiyo, Sungwa aliwakilishwa na Wakili Augustino Michael huku Jamhuri ikiwakilishwa na mawakili wa Serikali Suzan Masule na Violeth Mushumbusi.