Aliyemtoa utumbo mpenzi wake kutumikia kifungo cha miaka saba

Songea. Mahakama Kuu kanda ya Songea, imemuhukumu kifungo cha miaka saba jela, Abasi Majadini baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kujaribu kumuua mpenzi wake, Dora Kayombo kwa kumchoma kwa kisu tumboni hadi utumbo ukatoka nje.

Baada ya kufanya tukio hilo Machi 3, 2023 katika eneo la Matarawe Megengeni katika Manispaa ya Songea, Majadini alisogea pembeni kidogo na kuwasha sigara na kuvuta huku akitamka maneno kuwa, “ningekuua leo. Ningekumaliza leo.”

Hukumu hiyo imetolewa jana Alhamisi Machi 6, 2025 na Jaji Emmanuel Kawishe, ambapo alisema ushahidi wa mashahidi sita wa Jamhuri na vielelezo vinne, umethibitisha pasipo kuacha mashaka kuwa ni mshitakiwa pekee ndiye aliyefanya ukatili huo.

Katika utetezi wake, Majadini alikana kumchoma visu mpenzi wake huyo, na kudai kuwa baada ya kutokea ugomvi baina ya Dora na mwanaume mwingine, alikaa pembeni ya mpenzi wake huyo umbali wa karibu hatua tatu akivuta sigara.

Akaiambia mahakama alikuwa vizuri tu hadi alipopigwa na kitu kizito na kupoteza fahamu na alipozinduka baada ya siku tatu, alijikuta yuko hospitali amezungukwa na askari polisi na akasema anafahamu ni polisi walimpeleka hapo.

Kulingana na ushahidi wake, sio polisi walimtoa kwenye gari bali ni shemeji yake alifanya hivyo na kumpeleka hadi jengo la hospitali kwa matibabu.

Katika hukumu yake, Jaji alisema inashangaza kuwa mshtakiwa anasema alikuwa amepoteza fahamu lakini hapohapo alifahamu kuwa ni polisi ndio waliomwacha kwenye gari nje ya hospitali hadi alipopata msaada kutoka kwa shemeji yake.

“Swali ninalojiuliza, ni kwa nini alipigwa na kitu kizito kama alivyoieleza mahakama? alisema mshindani wake alikimbia baada ya ugomvi. Alikuwa anavuta sigara ndipo alipopigwa na kitu kizito,”alieleza Jaji katika hukumu yake.

“Hiyo inaashiria alipigwa kwa sababu ya kumchoma kisu shahidi wa kwanza (Dora) ambaye ni mpenzi wake. Hii inajenga hisia kuwa ushahidi wa shahidi wa nne na tano ni kweli kuwa alishambuliwa na raia wema baada ya kumchoma kisu.”

“Aliiambia mahakama kuwa alipigwa na kitu kizito usoni. Ninashawishika kuamini kuwa alama alizonazo kichwani na usoni zilitokana na kupigwa na wananchi wenye hasira kama mashahidi hao walivyoeleza kuwa alikuwa amezingirwa na watu,” alisema.

Baada ya kuchambua ushahidi, alisema mshtakiwa alitumia silaha aina ya kisu ambayo ni hatari na maeneo aliyomshambulia mpenzi wake ni tumboni, kifuani na begani ambayo ni hatarishi.

“Mapigo aliyoyapiga ni mawili tumboni, moja kwenye kifua na lingine kwenye bega. Maneno aliyoyatamka kuwa ningekuua leo. Kitendo cha kukaa pembeni kuvuta sigara yanadhihirisha nia yake dhidi ya mwathirika.”

Kutokana na uchambuzi huo, Jaji alisema anashawishika kuamini ushahidi wa upande wa mashitaka kuwa Majadini ndio aliyefanya jaribio hilo la mauaji na hivyo kulingana na kanuni za kutoa adhabu, anamuhukumu kifungo cha miaka saba jela.

Simulizi za mpenzi wake

Katika ushahidi wake, shahidi wa kwanza, Dora Kayombo alieleza alikuwa akiishi eneo la Matarawe na Aprili 2022, aliingia katika mahusiano na mshtakiwa na walikuwa wakitembeleana mara kwa mara.

Alieleza mapenzi yao hayo yalidumu kwa miezi 11 tu na Machi 10, 2023, mwanaye wa kiume ambaye anasoma Dar es Salaam alirudi nyumbani na siku hiyohiyo, mpenzi wake naye akafika nyumbani hapo akitaka kulala.

Chumba alichokuwa akiishi hakikuwa na uwezo wa kulaza watu watatu, hivyo alimwambia mwanaye aende akalale katika chumba cha mpenzi wake, maagizo ambayo shahidi huyo anasema hayakuwa yamempendeza mtoto wake.

Hivyo akamshauri mshtakiwa atafute nyumba nyingine kubwa ambayo ingewafanya waishi pamoja bila matatizo, na mshtakiwa akaridhia wazo hilo.

Hata hivyo, Machi 23, 2023, alipokea ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) kutoka kwa mpenzi wake huyo akitaka apelekewe jaketi lake alilokuwa ameliacha kwake na siku hiyohiyo saa 1:30 usiku, akapokea SMS nyingine ya kukumbushia.

SMS hiyo ilimtaka kumpelekea jaketi hilo katika grosari iitwayo Kagundula, lakini akaamua kulipeleka jaketi hilo nyumbani.

Siku hiyo saa 3:00 usiku, mpangaji mwenzake aitwaye Florah Nyika ambaye alikuwa rafiki yake wa karibu, alimuomba amsindikize kwenda mtaa wa Mwembechai kumuona dada yake ambaye alikuwa ni mgonjwa na alikubali.

Wakiwa njiani walikutana na mshtakiwa ambaye alikuwa anatokea upande ule wanaokwenda aliwasogelea na kuwasalimia ambapo Flora akasogea pembeni kama mita tatu kuwapisha wazungumze na hakuwa na wasiwasi wowote.

Shahidi huyo akaeleza kuwa wakati mshtakiwa anamkumbatia kama ulivyokuwa utaratibu wao kama sehemu ya kudumisha mapenzi yao, alisikia mlio “kachaa” na ndipo akagundua kuna kitu kimeingizwa tumboni kwake na kutolewa.

Alishangaa kuona utumbo wake ukitoka nje na ndipo alipogundua amechomwa na kisu, na hapo akamuona mshtakiwa akinyanyua mkono na kumchoma tena tumboni, kisha akaendelea kumchoma nacho begani.

Florah akasogea kwa ajili ya kumuokoa mwathirika na kumfunga tumbo ili utumbo usiendelee kutoka nje, mshitakiwa alidondosha kisu ardhini na alimsikia akisema, “ningekuua leo”.

Baada ya kumfunga kwa kutumia mtandio (scarf), Florah alienda kuomba msaada katika baa iliyokuwa jirani ambapo alifanikiwa kukutana na daktari aitwaye Zenda ambaye wanafahamiana na baada ya hapo alipoteza fahamu.

Alipata fahamu akiwa Hospitali ya Rufaa ya Songea katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) baada ya siku tatu na katika matibabu yake alifanyiwa upasuaji na kulazwa kwa siku 10.

Ushahidi wake huo uliungwa mkono na ushahidi wa rafiki yake Flora, ambapo alielezea kuwa hafahamu sababu za mshtakiwa kumchoma kisu Dora ambaye alikuwa mpenzi wake kwa muda mrefu.

Mashahidi wengine ambao ni maofisa wa Jeshi la Polisi walielezea namna walivyopata taarifa ya tukio hilo na kufika eneo la tukio na kukuta Sungusungu wapo na kupata kisu kilichotumika, huku daktari akieleza alivyomtibu.

Utetezi wa mshtakiwa

Akitoa utetezi wake, mshtakiwa huyo alieleza kuwa mwaka 2022 akiwa amelala chumbani na mpenzi wake  saa 1:30 asubuhi, mwanaume mmoja aliingia.

Mwanaume huyo alianza kutoa lugha ya matusi na alipomuuliza mkewe (Dora) huyo ni nani, akasema alikuwa ni mpenzi wake wa zamani aitwaye Ally Mohamed, au Champlini ambaye alikuwa akiishi mtaa wa Mahenge Manispaa ya Songea.

Alidai kuwa Ally na Dora walishawahi kuishi pamoja kwa miaka 10 kama mume na mke, lakini hawakuwa wamefunga ndoa na baadaye waliachana na kutokana na ugomvi uliotokea nyumbani kwa Dora, aliamua kwenda kuishi Mji Mwema.

Baadaye mke wake huyo alimjulisha kuwa mama mkwe wake alitaka wakutane eneo la Msamala ambapo mgogoro wao ulisuluhishwa na wakaendelea kuishi kama mume na mke hadi siku ya tukio yaani Machi 23, 2023.

Siku hiyo, alidai aliondoka nyumbani na kwenda katika shughuli zake za kila siku ambapo saa 11:30 jioni alikwenda kuonana na mteja katika grosari ya Ngadula ambayo ni karibu sana na nyumba waliyokuwa wakiishi na Dora.

Akiwa hapo grosari, alimuita mkewe kwa simu ili achukue fedha alizokuwa amepata siku hiyo, lakini hakujibu na baadaye alimuomba amletee jaketi lake hata hivyo pia hakujibu ujumbe wake huo aliomtumia.

Kwenye saa 2:30 usiku, alijibu ujumbe kuwa amepeleka jaketi hilo nyumbani kwake na baada ya hapo akawa hapokei simu zake.

Akaamua kuondoa kwenye hiyo grosari kurudi nyumbani na akiwa njiani na baada ya kupita baa ya Mapesa Inn, alisikia kelele kutoka uchochoroni ikisema “Dora Masodo huyu”, lakini hakuitambua sauti hiyo ilikuwa kwenye giza nene.

Aliwasha mwanga kupitia simu yake ambapo kwa mshangao alimuona mwanaume akimkumbatia mkewe na kumbusu, ambapo kulitokea ugomvi na wakati mkewe akijaribu kusuluhisha ugomvi, alianguka eneo lenye vioo.

Waliendelea kupigana kwa muda mrefu ambapo baadaye mwanaume aliyekuwa akipigana naye alikimbia na alimtambua kuwa ni Ally Mohamed au Champlin na wakati huo mkewe alikuwa chini akilalamika kuwa ameumia.

Alimuuliza mpenzi wake kwa nini anaendelea kufuatana na mwanamme huyo?

 Alisema alitembea kwa mita tatu akivuta sigara huku  akiendelea kumuuliza mkewe maswali akiwa na hasira ambapo walikaa umbali wa mita 10 kutoka walipokuwa wakigombana na Champlin.

Hapo ndipo alipigwa na kitu kizito kichwani hadi akapoteza fahamu na hakufahamu nini kilitokea na alizinduka baada ya siku tatu akiwa hospitali ya Rufaa ya Songea chini ya ulinzi wa Polisi.