Aliyemtoa Michael Jackson kimuziki afariki dunia

Marekani, Mtayarishaji nguli wa muziki duniani, Quince Jones, ambaye alitayarisha albamu za wanamuziki nguli kama Michael Jackson, Frank Sinatra na mamia ya wengine amefariki dunia akiwa na miaka 91.

Msemaji wake, Arnold Robinson, amesema Jones amefariki usiku wa Jumapili Novemba 3, 2024 nyumbani kwake katika eneo la Bel Air, Los Angeles nchini Marekani akiwa amezungukwa na familia yake.
 

                     

“Usiku wa leo, tukiwa na mioyo mizito lakini yenye upendo, tunatangaza habari za msiba wa baba yetu na ndugu yetu Quincy Jones. Na ingawa hili ni pigo kubwa kwa familia yetu, tunasherehekea maisha makubwa aliyoyaishi na tunajua kamwe hatutapata mwingine kama yeye.” imesema taarifa familia.

Jones alichukuliwa kama mtayarishaji bora wa muziki katika karne ya 20 kutokana ustadi wake kwenye albamu za Michael Jackson za Off the Wall, Thriller na Bad miaka ya themanini ambazo zilimfanya mwimbaji huyo wa Marekani kuwa msanii mkubwa duniani.

Albamu ya Michael Jackson ya Thriller inayotajwa kuwa na mafanikio zaidi iliuza zaidi ya nakala milioni 20 mnamo mwaka wa 1983 pekee na imekuwa ikishindana na albamu kama Greatest Hits 1971-1975 ya Eagles na nyinginezo kama albamu iliyouzwa zaidi wakati wote.

Pia alitayarisha nyimbo za magwiji Sinatra, Aretha Franklin, Donna Summer na wengine wengi.

Pia alikuwa mtunzi mwenye mafanikio katika nyimbo zilizotamba katika chati za muziki na sinema. Pia alikuwa kiongozi wa bendi ya muziki wa Jazz na mpigaji wa ala tofauti za muziki hasa kinanda na tarumbeta.