
Jane Doe, ambaye alifungua kesi akiwashtaki, mastaa wa muziki nchini Marekani, Sean “Diddy” Combs na Jay-Z kwa madai ya unyanyasaji wa kingono miaka 25 iliyopita ameondoa kesi yake dhidi yao.
CNN imeripoti leo Jumamosi Februari 15, 2025, kuwa, mawakili wa mwanamke huyo walitoa taarifa ya mteja wao kufuta kesi dhidi ya mastaa hao jana Ijumaa huku uamuzi huo ukiwa na kipengele cha kutofunguliwa tena kesi hiyo katika siku za usoni.
“Mawakili wa mdai wamejadili suala hili na mawakili wa kila mshtakiwa (Jay Z/Diddy) ambao wanakubali na kukubaliana na uwasilishaji huu,” ilisema hati ya mahakama iliyosainiwa na mawakili wa Jane Doe.
Mwanasheria wa Jay-Z, ambaye jina lake halisi ni Shawn Carter, alipongeza uamuzi huo uliochukuliwa na mlalamikaji dhidi ya mteja wake.
“Kesi ya uongo dhidi ya Jay-Z, ambayo haikupaswa hata kufikishwa mahakamani, imefutwa kabisa,” alisema wakili wa Jay Z, Alex Spiro, katika taarifa yake aliyoichapisha kwenye mitandao ya kijamii.
“Kwa kusimama imara mbele ya madai ya uongo na mabaya, Jay Z ameonyesha kile ambacho wachache wanaweza kukikabili alikataa kusalimu amri, hakufanya suluhu, hakulipa hata senti moja, alishinda na kutakasa jina lake,” alisema wakili huyo.
Kesi ya Doe ilifunguliwa awali dhidi ya ‘Diddy’ mwezi Oktoba 2024, ambapo alidai alipewa dawa za kulevya na kubakwa naye pamoja na mtu mwingine maarufu katika sherehe ya baada ya Tuzo za MTV Video Music Awards mwaka 2000, alipokuwa na umri wa miaka 13.
Katika malalamiko yaliyorekebishwa, yaliyowasilishwa Desemba 2024, ‘Jay Z’ aliongezwa kama mshtakiwa na akashutumiwa kwa ubakaji.
Jay Z, alikanusha vikali madai hayo, huku akimtaka mlalamikaji (Doe) kufungua kesi ya jinai na siyo ya madai kama alivyofanya endapo anaamini madai yake yana ukweli wowote dhidi yake.
Mawakili wa Jay Z, walifanya juhudi kadhaa kuhakikisha kesi hiyo inatupiliwa mbali kabla ya Doe kuiondoa jana.
Mnamo Desemba, jaji alikataa ombi la Jay Z, la kuifuta kesi hiyo na akampa Doe haki ya kuendelea na kesi hiyo bila kufichua jina lake, baada ya mawakili wa Carter kumtaka jaji kujitaja hadharani jina lake.
Wakati huo, jaji aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo bila kutaja jina lake alionekana kukerwa na pendekezo la mawakili wa upande wa walalamikiwa (Diddy/ Jay Z), wa kutaka kesi hiyo ifutwe.
Januari, 2025, mawakili wa Jay Z waliomba tena kufutwa kwa kesi hiyo na wakamuomba jaji (jina halifahamiki) kutoa adhabu dhidi ya wakili aliyeiwasilisha baada ya kubaini uwepo wa udanganyifu kwenye madai yaliyowasilishwa mahakamani.
Doe alikiri kuwa kuna kutofautiana kwa baadhi ya kumbukumbu zake katika mahojiano na NBC lakini alisisitiza kuwa alibakwa.
Hata hivyo, Wakili wake, Tony Buzbee, aliambia CNN wakati huo, “Mteja wetu anasisitiza kwa nguvu kuwa kile alichosema ni kweli, kulingana na kumbukumbu yake.”
Mawakili wa Diddy waliiambia CNN kuwa kufutwa kwa kesi ya Doe ni “uthibitisho mwingine kwamba kesi hizi zinajengwa katika misingi ya uongo, huku wakilaani uwepo wa utitiri wa kesi zinazofunguliwa dhidi ya mastaa hao bila utambulisho unaojulikana.
Combs (Diddy), ambaye anakabiliwa na zaidi ya kesi 40 za unyanyasaji wa kijinsia, alishtakiwa, Septemba 2024, kwa makosa ya kula njama kwa madhumuni ya uhalifu, usafirishaji wa watu kwa ajili ya biashara ya ngono na kusafirisha watu kwa madhumuni ya ukahaba.
Diddy amekana kutenda makosa hayo katika mashtaka yote 40.
Ijumaa, wakili wa Diddy aliiambia CNN kuwa mteja wake “hajawahi kumbaka wala kumsafirisha mtu yeyote kwa lengo la kumtumikisha kingono mwanamke au mwanaume, mtu mzima au mtoto.”
Wakili wa Doe alipotafutwa kuzungumzia suala hilo alikataa kuzungumza chochote.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.