Aliyembaka, kumlawiti mama yake na kumsababishia kifo ahukumiwa kunyongwa hadi kufa

Arusha. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, imemhukumu Clemence Mendrad, kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mama yake mzazi, Rose Augustino.

Siku ya tukio Clemence alienda kumpokea mama yake aliyekuwa akitokea Ifakara, Morogoro na alipofika kwenye chumba chake alichokuwa amepanga, alimsukumia kitandani akambaka na kumlawiti na mama yake alipojaribu kupiga kelele kuomba msaada alimpiga na fimbo.

Imeelezwa mahakamani kuwa  tukio hilo la Machi 30,2024 liliokea eneo la Kiwalani, Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam ambapo baada ya kutekeleza vitendo hivyo kesho yake Clemence  alienda kumtelekeza mama yake  eneo la Buza Sigara kando ya Reli ya Tazara.

Alipotenda kosa hilo, alijifungia ndani na kujichoma na bisibisi tumboni ila majirani wakiwamo  viongozi wa eneo hilo walivunja mlango na kumpeleka hospitali, kisha  kituo cha Polisi baada ya kupata nafuu.

Jaji Butamo Philip, aliyesikiliza kesi hiyo, alitoa hukumu hiyo Aprili 4, 2025 ambapo alisema baada ya kupitia ushahidi wa pande zote mbili, Mahakama imejiridhisha kuwa upande wa mashitaka umethibitisha kosa hilo bila kuacha shaka.

Katika kumtia Clemence hatiani, Jaji huyo pamoja na ushahidi wa kimazingira alitumia maelezo aliyoyatoa wakati akihojiwa polisi katika maelezo yake ya onyo ambayo alikiri kumbaka, kumlawiti na kumjeruhi mama yake.

Ingawa mshtakiwa huyo aliyejitetea chini ya hati ya kiapo, alijaribu kukana kukiri wakati wa utetezi wake mahakamani hapo.

Jaji alisema  swali la msingi katika kesi hiyo ni nani aliyesababisha kifo cha marehemu na upande wa mashitaka ulitegemea ushahidi wa kimazingira.

Amesema mbali na ushahidi huo wa kimazingira, maelezo ya onyo ya mshtakiwa huyo yaliyopokelewa kama kielelezo alikiri kumbaka na kumlawiti mama yake katika chumba chake, pia  mfululizo wa matukio katika ushahidi yanamuunganisha mshtakiwa na kifo cha marehemu.

“Jaribio la mshtakiwa kujiua linaonyesha alitaka kukwepa alichokifanya na ripoti kutoka Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, ilionyesha hakuwa na ugonjwa wa akili, hivyo alijua kitakachompata baada ya kusababisha kifo cha mama yake mzazi,” alisema Jaji.

Alisema Mahakama imemkuta na hatia Clemence na kumuhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.

Ilivyokuwa

Clemence  alishtakiwa kwa kosa la mauaji ambapo wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo upande wa Jamhuri uliwakilishwa na mawakili watatu, huku mshtakiwa huyo akiwakilishwa na wakili mmoja.

Katika kesi hiyo Jamhuri ilikuwa na mashahidi 11 ambao ni Mwanaisha Salum ( PW1), Ummy Mwalimu (PW2), Adamu Andrea (PW3), Tajiri Shabani (PW4), Shakira Mohamed (PW5), Erack Zero Mfupi -(PW6) E8207 Sajenti  Samweli (PW7), Geofrey Simba (PW8), Dk  Alex Mashaka (PW9), Rukia Heri (PW10) na Dk  Enock Changarawe (PW11).

PW 1 ambaye ni mmiliki wa nyumba aliyokuwa amepanga Clemence, aliieleza kuwa mshtakiwa alikuwa mpangaji wake tangu  Februari 9, 2024.

Alieleza kuwa Machi 30, 2024, PW10, ambaye pia alikuwa mpangaji katika nyumba hiyo, alimweleza kuwa alimsikia mwanamke akipiga kelele kuomba msaada kutoka chumba cha mshtakiwa.

PW1 alikwenda kwenye chumba cha mshtakiwa na kumuuliza ni nini na ni nani alikuwa akipiga kelele kuomba msaada chumbani kwake, majibu ya mshtakiwa ni kwamba aliyekuwa anapiga kelele ni mpenzi wake.

Siku iliyofuata, PW 2 ambaye alikuwa mpangaji wa PW 1, alimjulisha (PW 1) kuwa alimuona Clemence akiwa amembeba mwanamke kwenye bodaboda, aliyeonekana kuwa dhaifu.

Walieleza kuwa walienda kutoa taarifa kwa balozi wa nyumba 10, Latifa Mlete, ambaye aliungana nao na kuuliza kuhusu mtu aliyekuwa amembeba wakati akiondoka na bodaboda na aliwajibu ni mke wa kaka yake.

Alipoulizwa kwa nini alilala na mke wa kaka yake usiku kucha chumbani kwake, aliwajibu mwanamke huyo alikwenda kwa mama yake ila alifukuzwa na alipoulizwa alimpeleka wapi  alijibu kuwa alimpeleka kwa mama yake mzazi, eneo la Kigilagila, Kipawa.

Walieleza kumuomba mshtakiwa kuwapeleka mahali alipompeleka mwanamke huyo na alikubali, ila wakiwa njiani aliwaambia wanaenda eneo la Sigara na haikuwa salama kwenda kwa muda huo na kuamua kurudi ila mmoja alishauri Clemence apelekwe kituo cha polisi, lakini aliomba aruhusiwe kukaa chumbani kwake kwani alikuwa na matatizo mama yake amepotea.

Kutokana na ombi hilo walikubaliana kukutana asubuhi iliyofuata ili awapeleke eneo la Sigara na kesho yake walipokwenda kumgongea, ili waende eneo hilo walikuta chumba kimefungwa.

PW 10 ambaye  alikuwa mpangaji mwenzake Clemence, siku ya tukio usiku alisikia kelele ya mwanamke akiomba msaada zikitoka kwenye chumba cha mshtakiwa.

Alieleza kuwa mwanamke huyo alikuwa akisema ‘nisaidieni nakufa’ na kwa kuwa mlango wa chumba hicho ulikuwa wazi na aliingia na kumuona  bibi kizee amelala, na mshtakiwa yuko juu yake, akatoka na kwenda nje, akakutana na watu wengine wakija chumbani kwa mshtakiwa.

Alieleza walimkuta mshtakiwa akatoka nje na kuwaeleza alikuwa amesuluhisha ugomvi  na mwanamke huyo.

Aprili Mosi, 2024 Latifa alionana na PW 5 ambaye alikuwa rafiki yake pia na baada ya muda mshtakiwa alipita akiwa na begi na ameshika viatu mikononi mwake. Latifa alimfuata na kumuuliza kwa nini aliamua kuondoka, alimjibu amuache kwani alikuwa amechanganyikiwa na alipomuuliza alipo mama yake alidai amekutwa eneo la Buza.

PW 5 alieleza Clemence alimjulisha mama yake amepelekewa hospitali hali yake siyo nzuri, kisha aliingia ndani na alipoitwa Mwenyekiti wa Mtaa mlango huo haukufunguka kwani Clemence alikuwa amejifungia kwa ndani.

Walimtaka mshtakiwa kufungua mlango, lakini hakufanya hivyo, Mwenyekiti alivunja mlango na kumkuta mshtakiwa akiwa amelala chali akiwa amejichoma na bisibisi tumboni. Kesi hiyo iliripotiwa Kituo cha Polisi Buguruni ambapo askari walikwenda kumchukua na kumpeleka hospitali.

PW 5 ambaye ni binamu wa mshtakiwa alienda Hospitali ya Temeke alipomkuta Rose akiwa hana fahamu  na kueleza alikaa hospitalini hapo hadi Aprili 2, 2024 alipohamishiwa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (Moi), kabla ya kufariki Mei 5, 2024.

PW 5 alieleza kabla ya tukio hilo marehemu alimwambia kuwa uhusiano wake na mwanaye (mshtakiwa) haukuwa mzuri.

PW 8 akiwa Kituo cha Polisi Buguruni, Aprili Mosi 2024 ,alipokea simu kuhusu tukio la mshitakiwa kujijeruhi na hali yake haikuwa nzuri na alipofika alimkuta akivuja damu, alipomuuliza kwa nini amejijeruhi alimweleza amegombana na mama yake na alimshambulia Machi 30,2024.

Alieleza Clemence alipelekwa Hospitali ya Amana kwa matibabu na aliporuhusiwa Aprili 8, 2024 alipelekwa  Kituo cha Polisi Buguruni na wapelelezi walienda kuandika maelezo ya onyo ya mshtakiwa na walipomaliza walimweleza mshtakiwa alikiri kumvamia mama yake na kumtekeleza eneo la Buza Sigara.

Aidha P8 alieleza awali katika Kituo cha Afya Buza alipolazwa Rose kabla ya kuhamishwa, timu ya wachunguzi walikutana na daktari wa zamu, aliyewaeleza kuna mtu amepelekwa hapo na wasamaria wema na katika uchunguzi wake alibaini kuwa amebakwa na kulawitiwa.

PW 7 alipewa kazi ya kuchunguza kesi hiyo na Aprili 8, 2024 baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini alimhoji mshtakiwa kwa nini alijijeruhi na Clemence alimweleza siku ya tukio usiku alimpokea mama yake na kwenda naye nyumbani kwake.

Alieleza kuwa mshtakiwa huyo alimweleza wakiwa chumbani wawili  (yeye na mama yake) alimshika mkono na kumsukumia kitandani akamvua nguo na kumbaka kisha kumlawiti, na mama yake alipoanza kupiga kelele alimpiga na fimbo kisha akapoteza fahamu.

PW 7 alieleza kuwa mshtakiwa alisema Machi 31, 2024 asubuhi alikwenda eneo la Kwalimboa akakutana na dereva bodaboda (Ibrahim Athuman), aliyemuomba namba yake ya simu na kumwambia kuwa atampigia kwa sababu alikuwa na mgonjwa.

Alieleza saa tisa alimpigia simu Ibrahim ambaye alichelewa kufika hivyo kulazimika kutafuta bodaboda nyingine, akambeba mama yake kwenye pikipiki na kwenda kumtelekeza katika eneo hilo.

PW9 aliyeufanyia uchunguzi mwili huo Mei 13,2024 alieleza kuwa kichwa cha marehemu kilikuwa na makovu upande wa kushoto, fuvu la kichwa lilikuwa limevunjika na ubongo ulikuwa umevimba na chanzo cha kifo kilikuwa jeraha kubwa la ubongo.

Katika utetezi wake, Clemence alieleza kuwa Aprili 2,2025 alijikuta amelazwa katika Hospitali ya Amana na kumuona ofisa wa Polisi , huku akijiuliza alifikaje pale, kisha akagundua kuwa alikuwa ameshonwa kwenye tumbo lake kabla ya kuruhusiwa  Aprili 8, 2024.

Alisema aliporuhusiwa alipelekwa Kituo cha polisi Buguruni na baada  ya muda mfupi alipelekwa kwenye chumba cha mahojiano ambako alihojiwa kwa nini alijichoma na bisibisi, alieleza kujibu hakuwa na uwezo wa kukumbuka chochote na kuwa siku tatu baadaye alihojiwa tena kuhusu hilo suala akajibu hakumbuki.

Aliieleza mahakama kuwa walimwambia anajifanya hajui lolote kumbe amemuua mama yake na kuwa alishtuka na kuwaambia mama yake yuko Morogoro.

Akijitetea zaidi, alieleza kuwa katika chumba cha mahojiano  kulikuwa na polisi watano waliomtaka kuwaambia ukweli na kuwa walimlazimisha akiri kosa hilo kisha akapewa karatasi asaini.

Aidha alikana kuwa na uhusiano mbaya na mama yake, kumbaka na kumlawiti kwani alikuwa mtoto wake wa pekee, na alikuwa na tatizo la mwili kufa ganzi upande wa kulia  kuanzia kichwani hadi kwenye vidole vya miguu na alianza kuugua ugonjwa huo mwaka 2018.

Alisema kuwa alikuwa msahaulifu na mama yake alimpeleka hospitali, alipewa baadhi ya dawa ambazo zilimpa nafuu, lakini ameacha kuzitumia kwa kipindi kirefu na hakumbuki siku ya mwisho kuwasiliana na mama yake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *