
Manila. Aliyekuwa Rais wa Ufilipino, Rodrigo Duterte, amekamatwa leo Jumanne Machi 11, 2025 mjini Manila kwa hati ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).
Kwa mujibu wa The New York Times, Duterte amekamatwa baada ya Mahakama ya ICC kutoa waranti inayomtuhumu kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu katika vita vyake vya dawa za kulevya, ambapo mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema makumi ya maelfu ya Wafilipino waliuawa.
Taarifa zinasema aliwekwa kizuizini katika uwanja wa ndege wa Manila baada ya kurejea kutoka safari ya Hong Kong, kulingana na Serikali ya Ufilipino.
Wakili wa Duterte, Salvador Panelo amesema kukamatwa kwake ni kinyume cha sheria, kwa sababu Ufilipino ilijiondoa katika Mahakama ya ICC wakati Duterte akiwa Rais.
Duterte mwenye umri wa miaka 79 aliondoka madarakani mwaka 2022, anatajwa kuwa Rais mbabe hata hivyo bado ni mmoja wa wanasiasa wenye ushawishi mkubwa Ufilipino.
Lakini kukamatwa kwake kumetajwa kunaweza kuwa hatua kubwa kuelekea uwajibikaji kwa maelfu ya Wafilipino ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakitafuta haki kwa wapendwa wao, ambao wengi wao waliuawa kwa kupigwa risasi na maofisa wa polisi na walinzi.
Wanaharakati wamesema idadi kubwa ya waathirika walikuwa maskini. Pia waliuliwa Wafilipino wa mijini ambao baadhi yao walikuwa watoto wadogo na watu ambao hawakuwa na uhusiano wowote na biashara ya dawa za kulevya.
Ni watu wachache tu walipatikana na hatia kuhusiana na mauaji hayo, ambayo mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema jumla ya watu 30,000.
“Nina furaha sana kwamba Duterte amekamatwa ili hatimaye tupate haki,” amenukuliwa Cristina Jumola ambaye wanawe watatu waliuawa wakati wa vita vya dawa za kulevya.
Akiwa ofisini kipindi bado ni Rais Duterte aliiondoa Ufilipino kutoka Mahakama hiyo ya ICC ambayo ilikuwa imeanza kuchunguza mauaji hayo ya kiholela.
Lakini Ufilipino bado ni mwanachama wa Interpol, ambayo inaweza kutaka kukamatwa kwa Duterte kwa niaba ya ICC, hata hivyo mwakilishi wa Interpol alikuwepo wakati Duterte alipokamatwa.
Wakati muhula wa Duterte wa miaka sita ulipomalizika mwaka 2022, utawala wake ulieleza kuwa watu 6,252 waliuawa na vikosi vya usalama, ambao wote wakielezwa kama washukiwa wa dawa za kulevya.