Aliyekuwa DED Simanjiro kortini tuhuma za uhujumu uchumi

Simanjiro. Aliyekuwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, Samwel Warioba Gunza amefikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa kesi ya rushwa.

Gunza amefikishwa mbele ya hakimu mwandamizi wa Mahakama ya wilaya ya Simanjiro, Onesmo Nicodemo na kusomewa shitaka na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Shauri hilo la uhujumu uchumi limesomwa kwenye mahakama hiyo iliyopo mji mdogo wa Orkesumet leo Mei 19, 2025.

Mwendesha mashtaka wa Takukuru, Faustin Mushi akisoma hati ya mashitaka amesema Gunza anashtakiwa kwa kosa la uhujumu uchumi na kosa la wizi.

Amesema mshtakiwa huyo akiwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro alitumia fedha za halmashauri hiyo kiasi cha Sh5 milioni kwa matumizi yake binafsi.

Mushi amesema Gunza anashtakiwa kwa makosa ya ufujaji na ubadhirifu kinyume na kifungu cha 28 (1) cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa, sura ya 329 R.E 2022.

Amesema mshakiwa huyo pamoja na makosa ya kupangwa sura ya 200 R.E.2022 na kosa la wizi akiwa mtumishi wa umma kinyume na vifungu 258, 265 na 270 vya kanuni ya adhabu (sura ya 16 R.E. 2022).

Amesema sheria hiyo imesomwa pamoja na aya ya 21 jedwali la kwanza kifungu cha 57 (1) na 60 (2) vya sheria ya uhujumu uchumi.

Hata hivyo, hakimu Nicodemo alipomuuliza mshakiwa huyo (Gunza) kama ni kweli amefanya makosa hayo alikana mashitaka.

Hakimu huyo ameahirisha kesi hiyo hadi Mei 27, 2025 kwa hatua ya kusikiliza hoja ya awali (PH) katika mahakama hiyo.

Gunza yupo nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kusaini bondi ya Sh7 milioni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *