Aliyekuwa DED Bunda, wengine 11 kizimbani kesi ya uhujumu uchumi

Musoma. Watumishi tisa wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda mkoani Mara, akiwamo aliyekuwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Amos Kusaja na wafanyabiashara watatu wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma wakikabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh205.7 milioni.

Washtakiwa hao wamesomewa jumla ya mashataka 38 katika kesi hiyo namba 32001/2024 leo Jumatatu, Novemba 11, 2014 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Veronica Mgendi.

Akiwasomea mashtaka, Wakili kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (Takukuru), Restuta Kessy amedai washtakiwa walitenda makosa hayo kati ya Juni na Julai 2021.

Baadhi ya watumishi wa halmashauri ya Wilaya ya Bunda mkoani Mara pamoja na wafanyabiashara waliofikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma kwa makosa ya uhujumu uchumi. Picha na Beldina Nyakeke

Kessy amesema kwa mujibu wa sheria ya uhujumu uchumi kifungu cha 26 na kifungu kidogo cha pili, ili mahakama isikilize shauri hilo, inapaswa ipate kibali sambamba na cheti kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashataka nchini, jambo ambalo limetimizwa kabla ya shauri hilo kufikishwa mahakamani hapo.

“Wamefikishwa mahakamani kwa kosa la uhujumu uchumi, pamoja na mambo mengine wanatuhumiwa kwa matumizi mabaya ya madaraka, kuongoza genge la uhalifu, hali iliyosababisha Serikali katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kupata hasara ya kiasi hicho cha fedha,” amedai Kessy.

Amefafanua kuwa wafanyabiashara hao watatu ni wazabuni ambao wanatuhumiwa kushirikiana na watumishi hao kufanya vitendo hivyo kinyume cha sheria.

Baada ya kusomewa mashtaka, wakili kiongozi wa jopo la mawakili wanne wanaowatetea washtakiwa, Leonard Magwayega ameiomba mahakama kuwapa wateja wake dhamana kwa maelezo mashtaka yao yanadhamika kwa mujibu wa sheria.

“Ninaomba mahakama yako tukufu iwape dhamana wateja wangu kwa sababu kiwango cha fedha kilichotajwa kipo ndani ya mamlaka ya mahakama hii kwa mujibu wa kifungu cha 29 kifungu kidogo cha nne aya ya (a) ya sheria ya uhujumu uchumi na makosa ya kupanga,” ameeleza Magweyega.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Mgendi ameruhusu washtakiwa hao kudhamini kwa masharti kila mmoja awe na mdhamini atakayesaini hati ya dhamana yenye thamani ya Sh3 milioni, awe na makazi yanayotambulika  pamoja na kuwa na kitambulisho cha Taifa.

“Baada ya kuangalia kiasi ambacho washtakiwa wanadaiwa kusababisha hasara na baada ya kugawa kiasi hicho, tumebaini kila mshatkiwa anadaiwa Sh8.5 milioni, hivyo kwa mujibu wa sheria kiwango hicho kinadhaminika. Kila mshtakiwa anatakiwa kuwa na mdhamini mmoja anayetambulika makazi yake, mwenye kitambulisho ambaye atasaini hati ya dhamana yenye thamani ya Sh3 milioni kila mmoja,” amesema hakimu.

Washtakiwa wote wamekidhi vigezo vya dhamana na kesi itatajwa Desemba 2, 2024 kwa ajili ya kusomewa hoja za awali.

Hii ni mara ya pili kwa Kusaja kufikishwa mahakamani. Mara ya kwanza yeye pamoja na watuhumiwa wengine 11, wakiwepo wafanyabiashara na watumishi wa Serikali walifikisha katika Mahakama ya Wilaya ya Bunda Oktoba 17, 2023 kwa tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh351.6 milioni.