
Arusha. Mahakama ya Rufani imebariki adhabu ya kunyongwa hadi kufa aliyopewa Rajabu Juma, baada ya kutupilia mbali rufaa aliyowasilisha kupinga hukumu hiyo, kufuatia kutiwa hatiani kwa kosa la mauaji ya mkewe, Rehema Petro.
Miongoni mwa sababu zilizofanya Mahakama ya Rufani kutupilia mbali rufaa ya Rajabu Juma ni kujiridhisha na maelezo ya onyo aliyoyatoa, ambapo alikiri kumuua mkewe kwa kumchinja na kisha kuutelekeza mwili wake.
Jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani ambao ni Stella Mugasha, Lucia Kairo na Mustafa Ismail walioketi Kigoma, wametoa hukumu hiyo Mei 19, 2025.
Rufaa hiyo ilikuwa inapinga hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mei 31, 2023 katika kesi ya jinai ya mwaka 2022.
Msingi wa rufaa
Upande wa mashitaka ulieleza Mahakama Kuu kuwa kosa hilo lilitendeka Aprili 4, 2022 katika eneo la Nyambutwe, Wilaya ya Uvinza, mkoani Kigoma.
Mashahidi wa Jamhuri ambao ni maofisa wa Polisi, Koplo Rajabu (shahidi wa pili), Koplo Abel (shahidi wa nane) na Menasi Temba (shahidi wa tisa), walieleza kujulishwa katika eneo la Darajani, kitongoji cha Nyambutwe, kuna mwili wa mwanamke umekutwa umetelekezwa.
Wao pamoja na shahidi wa tatu ambaye ni Dk Kasian Adam na shahidi wa nne, Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Omari Kilala, walienda eneo la tukio na kukuta mwili wa mwanamke ukiwa umefungwa na kitenge, huku ukiwa na jeraha la kukatwa shingoni, damu ikitoka.
Walieleza kuwa ilionekana tukio hilo limefanyika eneo lingine na mwili huo kupelekwa hapo ambapo mwili huo ulitambuliwa na ndugu yake, Nasibu Kajabala.
Uchunguzi uliofanywa na shahidi wa tatu, ulibaini kuwa mwili huo ulikuwa umegongwa na kitu butu ambacho kiliharibu fuvu la kichwa, alichinjwa, jambo lililofanya mumewe kukamatwa kama mshukiwa wa tukio hilo.
Kumbukumbu za rufaa hiyo zinaonyesha ushahidi wa shahidi wa pili, nane na tisa unaonyesha mrufani alikiri kuhusika na kifo cha mkewe kupitia maelezo yake ya onyo ambayo yalipokelewa mahakamani hapo kama kielelezo cha sita.
Ilielezwa kuwa katika maelezo hayo mrufani huyo alieleza siku ya tukio akiwa na mkewe (marehemu kwa sasa) kitandani wakijiandaa kufanya tendo la ndoa, mkewe alianguka vibaya kitandani, akampiga kichwa hadi kufa na kwa hofu aliuchukua mwisho huo akaenda kuutelekeza kwenye ukingo wa mto na kuondoka.
Alipofikishwa mahakamani alikana kutenda kosa hilo ambapo katika kesi hiyo upande wa mashitaka ulikuwa na mashahidi tisa.
Akijitetea mahakamani hapo mrufani huyo alieleza siku ya tukio aliondoka nyumbani kwake saa 12:30 asubuhi akiendesha baiskeli yake kwenda kuchota maji kwa ajili ya shughuli yake ya uzalishaji wa chumvi na akiwa njiani alikutana na watoto wake wakienda shule.
Alieleza kuwa alipofika alianza kunoa shoka lake kwa ajili ya kupasua kuni ndipo akapigiwa simu na mtu kumjulisha kuwa mkewe amechinjwa na mwili wake kutelekezwa.
Alieleza baada ya kupiga simu kadhaa, alienda eneo la tukio ndipo alipokutana na maofisa Polisi na watu wengine ambapo aliutambua mwili huo, na baadaye kuhojiwa na Polisi na kukana kukiri kuhusika na mauaji hayo.
Baada ya Mahakama hiyo kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili ilimkuta na hatia na kumuhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.
Katika rufaa hiyo Rajabu alikuwa na sababu tano za ikiwemo Mahakama iliyosikiliza kesi hiyo ilikosea kisheria ilipomtia hatiani kutokana na ushahidi dhaifu na uliokinzana, alinyimwa haki ya kuwasilisha mawasilisho ya mwisho.
Nyingine ni hukumu dhidi yake ilitokana na ushahidi wa kimazingira na maelezo ya onyo ambayo alidai yalichukuliwa bila hiari yake na kupokelewa kimakosa mahakamani, pamoja na kesi hiyo kutothibitishwa bila kuacha shaka yoyote.
Upande wa mjibu rufaa ulieleza mahakama kuwa mrufani alikuwa na hatia ya mauaji hayo na ushahidi wake uchukuliwe kuwa bora zaidi ambao upande wa mashitaka ungeutoa.
Wakisisitiza hoja hiyo, waliielekeza mahakama kwenye kesi ya Majid Hussein Mboryo & 2 Others dhidi ya Jamhuri, katika rufaa ya Jinai, namba 141/ 2015, ambapo ilionekana kuwa ushahidi bora ni wa mshtakiwa anayekiri hatia yake.
Katika ukurasa wa 87 wa rekodi ya rufaa, mrufani huyo alikiri alikuwa pamoja na mkewe, akimaanisha kuwa yeye ndiye alikuwa mtu wa mwisho kuonekana akiwa na Rehema (marehemu kwa sasa).
Uamuzi Majaji
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, jopo la majaji hao watatu walieleza kabla ya kuangalia sababu hizo za rufaa wanalazimika kuanza kushughulikia na wasiwasi uliopo namna ya kielelezo cha sita kilivyopokelewa na Mahakama.
Jaji Ismali alieleza kuwa rekodi ya rufaa, ushahidi wa shahidi wa tisa aliyerekodi maelezo ya ukiri ya mrufani huyo na wakati kielelezo hicho kinawasilishwa mahakamani hapo halikupingwa na upande wa utetezi, hivyo Mahakama ikapokea kielelezo hicho cha sita.
Kuhusu iwapo shauri hilo lilithibitishwa bila kuacha shaka, amesema ni msingi wa sheria kuwa katika kesi zote za jinai ni jukumu la upande wa mashitaka kuthibitisha hatia ya mshtakiwa.
Jaji Ismail amesema miongoni mwa masuala yaliyomtia hatiani Rajabu ni pamoja na ungamo lake la kukiri kosa hili na ushahidi wa kimazingira ambapo mrufani alikuwa mtu wa mwisho kuonekana akiwa na Rehema (marehemu kwa sasa).
Amesema Mahakama hiyo ya juu imekuwa ikirudia mara kwa mara kwamba shahidi bora katika kesi za jinai ni mshtakiwa ambaye anakiri hatia yake kwa uhuru, akisisitiza kesi ya Majid Hussein (supra).
“Kwa maoni yetu, neno uhuru limetumika kwa makusudi, kusisitiza jambo kwamba ungamo lazima liwe la hiari, bila shuruti, vitisho au ahadi,” amesema
Jaji Ismail amesema uhakiki wao wa kina wa rekodi umewapeleka kwenye ukurasa wa 87 wa rekodi ya rufaa ambayo ina maelezo ya onyo ya Rajabu ambapo amenukuliwa akisema yafuatayo:
…Kisha tukarudi eneo ulipokuwa mwili wa marehemu kushuhudia uchunguzi wa mwili wa marehemu pamoja na watu wengine. Baada ya uchunguzi kukamilika afande alinitaka nikatoe maelezo polisi ambapo nilikiri kumuua mke wangu kisha kumchinja na kutelekeza mwili wake njiani. Kwa kitendo nilichofanya naomba nisamehewe….”
Jaji amesema kama rekodi ya rufaa inavyoonyesha, hakuna kitu kinacholeta hisia yoyote kwamba mrufani alilazimishwa kufanya hivyo na kuwa kwa mtazamo wao hawaoni chochote kibaya katika uamuzi wa Mahakama ya mwanzo.
Kuhusu ushahidi wa kimazingira, Jaji Ismail amesema ushahidi wa mashitaka uliotolewa unapaswa kueleza iwapo ushahidi huo utasababisha hitimisho kwamba ni mtuhumiwa na si mtu mwingine aliyefanya uhalifu huo.
Jaji Ismail amesema wamezingatia mwenendo wa mrufani baada ya kifo cha mkewe ambapo alichukua mwili huo na kwenda kuutupa ili kujenga hisia ya kutatanisha kwamba mkewe (Rehema) aliuawa.
“Tumezingatia pia jinsi mrufani alivyojifanya kutojua kutokuwepo kwa marehemu na, wakati fulani, akidai kwamba mkewe alikuwa ametoka kijijini, ukweli huu hauwezi kuwa maelezo au dhana nyingine zaidi ya hatia,”
“Tuna maoni thabiti kwamba hali hizi zinaelekeza kwa mrufani bila pingamizi kuwa muhusika wa mauaji hayo,” ameongeza Jaji Ismail
Jopo la majaji hao walihitimisha kwa kutupilia mbali rufaa hiyo kutokana na sababu za rufaa kutokuwa na mashiko na kuwa shitaka hilo lilithibitishwa bila kuacha shaka, hivyo kushikilia uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma.