
UNAMKUMBUKA aliyezamisha jahazi la Simba ikiambulia pointi moja dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa KMC, si mwingine namzungumzia Abdallah Hassan amemalizana na uongozi wa timu hiyo baada ya makubaliano ya pande mbili.
Simba ambayo ilikuwa timu mwenyeji wa mchezo huo wa ligi walitangulia kwa mabao mawili kipindi cha kwanza kutoka kwa Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ na Lionel Ateba kwa penalti , lakini Coastal wakacharuka kipindi cha pili na kusawazisha kupitia kwa Abdallah Hassan na Hernest Malonga mchezo ulichezwa Oktoba 4 mwaka jana.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya klabu hiyo kimeliambia Mwanaspoti kuwa Hassan mwenye mabao mawili tangu amejiunga na timu hiyo amevunjiwa mkataba kutokana na utovu wa nidhamu wakati mchezaji mwenyewe ameweka wazi kuwa timu hiyo imeshindwa kutimiza vipengele vya kimkataba.
Hassan ameichezea Coastal Union mechi 12 kati ya 23 zilizochezwa na timu hiyo ameifungia mabao mawili tu dhidi ya Simba na ule dhidi ya KenGold mchezo uliochezwa Novemba 23 mwaka jana na timu hizo kugawana pointi moja moja baada ya sare ya bao 1-1 Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya.
Wakati hayo yakiendelea kocha Juma Mwambusi amesema anapambana na wachezaji waliopo kuhakikisha wanafikia malengo waliyojipangia kipindi hiki ambacho anahitaji kuchukua pointi zote 21 zilizobaki ili kujiweka kwenye nafasi nzuri.
“Tuna mambo mengi ya kufanya ikiwa ni pamoja na kuwarudisha wachezaji kwenye hali ya ushindani mambo ambayo yamemalizika kimakubaliano sio muhimu sana kuyazungumzia kwa sasa tunapambana kuzikusanya pointi 21 zilizi mbele yetu,” alisema na kuongeza;
“Wachezaji wangu wote wapo kwenye hali nzuri ya tunaendelea kupeana mbinu ili kuweza kuvuka kihunzi kilicho mbele yetu sio rahisi kupata matokeo kama tunavyozungumza bila maandalizi mazuri na kuwajenga wachezaji kimwili na kiakili.”
Mwambusi alisema ili kufikia malengo hayo ni kukaa vizuri na wachezaji na kuzungumza nao nini wanatakiwa kufanya na kufikia makubaliano kitu ambacho ndio kinafanyika sasa ikiwa ni pamoja na maandalizi.
Coasta Union ipo nafasi ya tisa kwenye msimamo baada ya kucheza mechi 23 imefanikiwa kukusanya pointi 25 ambazo ni sawa na wastani wa kukusanya pointi moja klwenye kila mchezo imeshinda mechi tano, sare 10 na vipigo nane.
MECHI ZILIZOBAKI
v Kagera Sugar (ugenini)
v Yanga (ugenini)
v Singida Black Stars (nyumbani)
v KenGold (nyumbani)
v Tanzania Prisons (ugenini)
v Fountain Gate (nyumbani)
v Tabora United (nyumbani)