Manchester, England. Mfanyakazi wa Manchester United aliyedumu klabuni hapo kwa muda mrefu Marie Marron, ametimuliwa.

Mmiliki mwenza wa Man United Sir Jim Ratcliffe, amekuwa na msimamo mkali sana wa kubana matumizi tangu ameingia kwenye klabu hiyo akiwa ameshawatimua wafanyakazi zaidi ya 200 klabu hapo.
Marron ambaye amekaa klabuni hapo kwa zaidi ya miaka 46 na kuhudumu kwenye nafasi mbalimbali kubwa ameshapewa taarifa kuwa mwisho wa msimu ataondoka hapo.
Wadhifa wa mwisho wa mkongwe huyo ni msimamizi wa masuala ya soka ya timu hiyo, akiwa anatajwa kama mtu mwenye heshima kubwa zaidi kwenye klabu hiyo, lakini akiwa amehusika kwenye mabadiliko mbalimbali ndani ya timu hiyo pamoja na kushiriki kutwaa makombe mengi kipindi cha kocha Alex Ferguson.
Taarifa ambayo imetoka Man United inasema kuwa Marron, aliitwa na uongozi wa United na kupewa taarifa kuwa ataondolewa kwenye klabu hiyo mwishoni mwa msimu huu.
Awali Kath Phipps, ndiye alikuwa anashikilia nafasi ya kwanza kwa mfanyakazi aliyehudumu kwenye klabu hiyo kwa muda mrefu akiwa alikaa kwa kwa miaka 55 kabla hajafariki dunia Desemba mwaka jana.
Marron amekuwa mara kwa mara akiiwakilisha United kwenye vikao vinavyoitishwa na FA, FIFA na UEFA lakini akiwa pia ni mmoja kati ya watu ambao wamekuwa wakizisoma mbinu za wapinzani kwenye michuano ya ndani na Ulaya kwa ujumla.

Wiki iliyopita alikuwa nchini Hispania kwenye mchezo wa nusu fainali wa Kombe la Europa kati ya Man United na Athletic Bilbao, mchezo ambao United waliibuka na ushindi wa mabao 3-0.
Mbali na huyo, pia imeelezwa kuwa United ina mpango wa kuwapunguza wafanyakazi wengine 200, huku baadhi wakiwa wameshapewa taarifa ya kikao na uongozi wa klabu hiyo ambacho kinatarajia kufanyika kabla msimu wa ligi haujamalizika.