
Arusha. Mahakama ya Rufaa Tanzania imemwachia huru Alphonce Michael maarufu Rasi aliyehukumiwa kunyongwa hadi kufa, baada ya kutiwa hatiani kwa mauaji ya Steven Kimario.
Alidaiwa baada ya mauaji hayo aliuweka mwili wake kwenye mfuko wa nailoni na kisha kuuchoma moto.
Rasi alihukumiwa Agosti 22, 2022 na Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi iliyopewa mamlaka ya kusikiliza kesi ya mauaji iliyokuwa ikimkabili.
Katika kesi hiyo Michael na mwenzake Humphrey Manongi ambaye hakuwa mhusika katika rufaa hiyo, walishtakiwa kwa mauaji ya Kimario, kosa wanalodaiwa kutenda Desemba 13, 2016 katika eneo la Savena, Majengo wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi ilimwachia huru Humphrey, huku ikimtia hatiani Michael na kumhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa, lakini naye hakukubaliana na uamuzi akakata rufaa.
Hukumu ya rufaa iliyomwachia huru Michael ilitolewa Machi 26, 2025 na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani ambao ni Lugano Mwandambo, Paul Kihwelo na Agnes Mgeyekwa.
Majaji walifikia uamuzi huo baada ya kupitia mwenendo wa kesi na kusikiliza hoja za pande zote mbili na kubaini ushahidi wa upande wa mashtaka haukuweza kuthibitisha pasipo kuacha shaka kuwa Michael alihusika na mauaji hayo.
Tukio lilivyokuwa
Ilidaiwa Necta Kimario alikuwa akiishi na mtoto wake, Jamila Ahmed (shahidi wa saba) na mfanyakazi wa nyumbani aliyetajwa kwa jina la Jonisia Aloyce au Masilayo. Walikuwa wakiishi nyumba ya kupanga yenye vyumba viwili eneo la Majengo.
Ilidaiwa Necta na mrufani walikuwa marafiki. Desemba 13, 2016 Necta alitembelewa na mjomba wake Steven Kimario (marehemu).
Siku ya tukio inadaiwa Jamila na Jonisia walilala kwenye chumba kimojawapo. Steven (marehemu) usiku alikwenda kwenye chumba hicho kutafuta maji ya kunywa.
Jamila alidai baada ya kuondoka, Steven alirudi chumbani akitaka kufanya mapenzi na Masilayo ambaye alipiga kelele kuomba msaada.
Ilidaiwa wakati huo Necta hakuwepo ila rafiki yake aliyekuwa karibu alimjulisha juu ya suala hilo, hivyo akarudi akiwa na mrufani wakamvamia Steven wakiwa sebuleni kwa kumpiga sehemu tofauti za mwili wake.
Necta alidaiwa kutumia waya wa runinga kumpiga Steven (marehemu), huku mrufani akitumia kisu kumchoma.
Ilidaiwa mahakamani kuwa licha ya majirani kuomba wasitishe kipigo, hawakuacha.
Shahidi wa saba alidai siku iliyofuata alimwona mama yake, rafiki yake na mtu mwingine ambaye hakumfahamu wakishuka kwenye teksi nyeupe na kuingia ndani ya nyumba.
Alidai muda mfupi baadaye, watatu hao walitoka na mfuko mweupe wa nailoni ambao waliuweka kwenye buti la gari na kuondoka kwenda mahali pasipojulikana.
Shahidi wa nane ambaye alikuwa dereva wa teksi hiyo, Elihudi James alidai alikodishwa kuwapeleka watu hao eneo la Mto Rau ambako kifurushi kilichokuwa kwenye mfuko wa nailoni kiliteketezwa kwa moto.
Shahidi wa nne, Gervas Moshi ambaye ni muuza duka la vinywaji kando ya barabara inayoelekea Rau, alidai kumuona kijana aliyekuwa na nywele za kutisha akiwa ameongozana na mtu mwingine.
Alidai watu hao walishuka kutoka kwenye teksi nyeupe iliyoegeshwa mita kati ya 10 hadi 15 kutoka dukani na kuondoka baada ya dakika 10.
Shahidi alidai alisikia taarifa za maiti iliyokuwa kwenye mfuko wa nailoni kuungua kando mwa mto eneo la Bondeni.
Januari 5, 2017 Moshi alidai alihudhuria gwaride la utambulisho ambako alimtambua mtu aliyewahi kufika dukani kwake Desemba 15, 2016 kununua sigara na vinywaji vikali, ila mwaka mmoja na nusu baadaye, alipoitwa kwenye gwaride lingine la utambulisho hakumtambua mrufani kutokana na muda kupita.
Mahakama ilitegemea ushahidi wa shahidi wa nane ambaye alidai kukodiwa na mteja wa kiume kubeba kifurushi kutoka kwenye nyumba moja eneo la Majengo ambako aliwakuta watu wengine wawili.
Alidai baada ya kufika eneo la Rau, aliagizwa kusimama karibu na mto ambako Rasi na mwenzake walichomoa kifurushi hicho kwenye buti la gari na kuondoka nacho kuelekea mtoni ambako wakiwa njiani kurudi alionywa na Rasi kuwa kifurushi walichokuwa nacho kilikuwa mwili wa binadamu.
Alidai kutishiwa kuuawa endapo angemweleza mtu yeyote na kwa kuogopa hilo alilazimika kunyamaza na siri hiyo hadi alipokamatwa na polisi.
Katika gwaride la utambulisho lililofanyika mwaka 2018, shahidi huyo alimtambua mrufani kama mmoja wa watu waliomkodi hadi Rau.
Kuhusu kugunduliwa maiti iliyokuwa ikiteketea moto Bondeni kando mwa Mto Rau, kulielezwa na shahidi wa kwanza wa mashtaka, Ernest Mambo aliyekuwa akikaa jirani na mto huo.
Alidai alikuwa miongoni mwa watu waliobaini maiti iliyokuwa ikiungua mtoni mchana akawasiliana na mwenyekiti wa kijiji na polisi walifika muda mfupi baadaye.
Shahidi wa 10, Sajenti wa Polisi Vitalis alidai akiwa na timu yake walifika eneo la tukio wakachukua mwili wa binadamu uliokuwa ukiungua ukiwa kwenye mfuko wa nailoni ambao ulipelekwa Hospitali ya Rufaa ya KCMC na baadaye kutambuliwa ni Steven Kimario.
Shahidi wa tano Dk Alex Mrema aliyeuchunguza mwili huo Desemba 23, 2016 alisema chanzo cha kifo ni majeraha mwilini kutokana na kuungua.
Mrufani alikamatwa Juni 15, 2018, Kahama mkoani Shinyanga. Mahakama ilisema upande wa mashtaka umethibitisha kesi hiyo pasipo kuacha shaka kuwa mrufani alihusika na mauaji licha ya kuwa mahakama ilitegemea ushahidi wa kimazingira.
Rufaa ilivyokuwa
Mrufani akiwakilishwa na Wakili David Shilatu aliwasilisha sababu tatu za rufaa kwamba mahakama ilikosea katika msingi wa hukumu kutegemea ushahidi wa kimazingira na hukumu ilitokana na ushahidi dhaifu ambao haukuthibitishwa kwa kiwango kinachotakiwa.
Mjibu rufaa aliwakilishwa na mawakili wanne wa Serikali.
Shilatu alidai masharti ya msingi ya utegemezi wa ushahidi wa kimazingira kwa kumtia hatiani hayakutimizwa, akitoa mfano wa ushahidi wa shahidi wa saba ambaye alishindwa kumtambua mrufani mahakamani licha ya kudai kufahamiana naye.
Alidai kushindwa kufanya hivyo kulidhoofisha ushahidi. Alidai Masilayo alikuwa shahidi muhimu ambaye hakupelekwa mahakamani bila sababu za msingi.
Uamuzi wa majaji
Majaji katika hukumu hiyo wamesema mbali ya shahidi wa saba, hakuna mwingine wa upande wa mashtaka aliyetoa ushahidi wa moja kwa moja, hivyo ushahidi pekee unaotegemewa ni wa mazingira.
Katika hukumu majaji wamesema wamelazimika kuchunguza tena ushahidi uliopo kwenye kumbukumbu kwa kuwa ni rufaa ya kwanza.
Baada ya kupitia mwenendo wa shauri hilo, wameeleza kukubaliana na Wakili Shilatu kuwa uwepo wa Masilayo ulikuwa muhimu ili kutoa uthibitisho wa ushahidi wa shahidi wa saba.
Amesema awali, Masilayo alikuwa mmoja wa washtakiwa lakini kesi dhidi yake ilifutwa katika hatua za awali.
Majaji wamesema kutokuwepo kwa maelezo kwa nini mtu kama huyo ambaye kutokana na kumbukumbu alikuwa chanzo cha sakata hilo kunaacha shaka kwenye kesi ya mashtaka.
Hukumu inasema bado kuna mengi zaidi ambayo kwa mujibu wa shahidi wa tisa na wa 10 walidai walipopekua chumba tukio lilipotokea, walikuta madoa ya damu sakafuni na kuchukua sampuli za damu ila hakuna kilichofanyika, jambo linalozua maswali mengi.
Majaji wamesema baada ya kuchambua mwenendo wa shauri hilo lililomtia hatiani mrufani, wamejiridhisha upande wa mashtaka haukutekeleza wajibu wake wa kuthibitisha kesi hiyo pasipo kuacha shaka yoyote.
Mahakama katika hukumu hiyo iliikubali rufaa, kutengua adhabu ya kunyongwa hadi kufa aliyokuwa amehukumiwa mrufani na kuamuru aachiwe huru.