Alichozungumza Papa Leo XIV na Zelensky

Vatican. Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki, Papa Leo XIV amefanya mazungumzo ya simu na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky ikiwa ni simu ya kwanza kuzungumza na kiongozi wa kitaifa tangu achaguliwe katika wadhifa huo.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika leo Jumatatu Mei 12, 2025, Papa Leo na Zelensky wamezungumzia mapendekezo ya usitishaji mapigano na malumbano kati yake na Rais wa Russia, Vladimir Putin.

Akizungumzia simu hiyo, Zelensky amesema kupitia akaunti yake ya mtandao wa Telegram amesema mazungumzo yake ya kwanza na Papa huyo mpya yalikuwa yenye tija na maana kwenye ustawi wa raia wa Ukraine.

Pia amesema amempa mwaliko Papa wa kuitembelea Ukraine ili kushuhudia uharibifu uliofanyika kwenye miundombinu na maisha ya binadamu.

“Tumezungumzia kuhusu watoto wa Ukraine waliotekwa na kuhamishwa kimabavu na Russia baada ya uvamizi wake nchini Ukraine na kuhusu juhudi za mazungumzo ya kumaliza vita hivi,” amesema Zelensky.

Msemaji wa Vatican, Matteo Bruni, alipoulizwa na Shirika la Habari la Reuters kuhusu mazungumzo hayo amethibitisha kuwa ni kweli yalifanyika.

Hata hivyo, Bruni hakutoa maelezo zaidi kuhusu yaliyojadiliwa kwenye simu hiyo.

Katika hatua nyingine, Rais, Zelenskiy amesema yuko tayari kukutana na hasimu wake, Vladimir Putin nchini Uturuki Alhamisi Mei 15, 2025.

Uamuzi huo wa Zelensky umekuja baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump kumtaka hadharani akubali mara moja pendekezo la kiongozi wa Russia la kufanya mazungumzo ya moja kwa moja.

Pendekezo la Zelensky la kukutana na Putin lilihitimisha saa 48 za mivutano mikubwa ambapo viongozi wa Ulaya waliungana na Zelensky kuitaka Russia kukubali usitishaji mapigano wa siku 30 kuanzia Jumatatu.

Hata hivyo, haikufahamika wazi ikiwa Putin alikusudia kuhudhuria binafsi. Putin na Zelensky hawajakutana tangu Desemba 2019 na wamekuwa wakianika uhasama wao hadharani.

“Nitamsubiri Putin Uturuki Alhamisi. Binafsi natumaini safari hii raia wa Russia hawataanza kutafuta visingizio,” ameandika Zelensky kwenye akaunti yake ya Mtandao wa X.

Kiongozi huyo wa Ukraine alijibu kwa tahadhari Jumapili baada ya rais wa Russia, katika hotuba ya usiku iliyorushwa kupitia Televisheni kuwa anapendekeza mazungumzo ya moja kwa moja mjini Istanbul Alhamisi ijayo, Mei 15.

Zelensky naye alisema Ukraine iko tayari kwa mazungumzo, ikiwa Russia itakubali usitishaji mapigano kwa siku 30.

Lakini Trump, ambaye ana mamlaka ya kuendeleza ama kusitisha msaada muhimu wa kijeshi wa Marekani kwa Ukraine, alionyesha msimamo tofauti

“Rais Putin wa Russia hataki kuwa na makubaliano ya usitishaji mapigano na Ukraine, bali anataka kukutana Alhamisi, nchini Uturuki, kujadili uwezekano wa kumaliza umwagikaji damu. Ukraine inapaswa kukubaliana na hili mara moja,” aliandika Trump kwenye mtandao wake wa Truth Social.

“Angalau wataweza kubaini kama kuna uwezekano wa makubaliano, na kama hakuna, basi viongozi wa Ulaya na Marekani watajua hali halisi na kuendelea ipasavyo!”

Tangu uvamizi wake nchini Ukraine, Russia imeyatwaa maeneo ya mikoa ya Donetsk, Luhansk, Kherson, Zaporizhia, Pokrovisk, na Crimea iliyotwaliwa tangu mwaka 2014.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *