Alichokifanya Lissu nje ya mahakama ya Kisutu akirejeshwa rumande

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, amerudishwa Gereza la Ukonga baada ya kesi zake kuahirishwa hadi Juni 2, 2025 na alipokuwa akiwaaga waandishi wa habari, amesema ‘kimeumana.’

Lissu, ambaye anakabiliwa na kesi mbili ya uhaini na ya uchochezi alitolewa ndani ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu saa 7:13 mchana, na gari lake kuondoka saa 7:25.

Kesi zote mbili zilizosikilizwa leo Jumatatu Mei 19, 2025 ya uhaini na ya uchochezi, ambazo zilisikilizwa leo, zimeahirishwa hadi Juni 2, 2024.

Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu akisalimiana na John Heche ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Bara.

Mamia ya wafuasi wa Chadema waliokuwa nje ya uzio wa mahakama hiyo walisikia kauli hiyo ya ‘kimeumana’ wakati Lissu aliponyoosha vidole viwili juu huku akitabasamu.

Baada ya kauli hiyo, wanachama na wafuasi wa Chadema, pamoja na wananchi waliokuwepo, walianza kupaza sauti wakisema ‘rais…rais!” kabla ya kuimba wimbo wa Paulo na Sila kwa takriban dakika tano, kisha waliimba wimbo mwingine uliosema “Bado kidogo historia itabadilika.”

Baadaye, walianza kupaza kauli ya kampeni ya chama chao, ‘No reforms, no election’.

Nje ya Mahakama

Mamia ya wanachama walijitokeza kufuatilia hatima ya kesi hizo. Baadhi yao walivaa sare rasmi za chama, huku wengine wakivaa fulana nyeupe zenye nembo ya Chadema na maandishi yanayosomeka No reforms, no election.

Huku wakiimba na kucheza, wafuasi na wapenzi hao wa Chadema walimshangilia Lissu wakiimba wimbo wa Paulo na Sila waliimba milango ya gereza ikafunguka, wakati kiongozi huyo akitoka nje ya Mahakama hiyo.

Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche na Katibu Mkuu, John Mnyika walizungumza na wafuasi hao na kuwashukuru kwa ushirikiano wao huku wakiwataka kujitokeza kwa wingi zaidi mahakamani hapo kesi hiyo itakapotajwa tena.

Wakati wakizungumza hayo, wafuasi walipaza sauti wakitaka kampeni ya tone tone iendelee na kushinikiza Heche akusanye fedha hapohapo, kiongozi huyo alitii na kuvua kofia yake kukusanya, zoezi ambalo lilifanyika muda mfupi kabla ya viongozi hao kuondoka.

Wakati hayo yakiendelea, Polisi waliokuwa mahakamani hapo kwa wingi hawakutumia nguvu kubwa kuwaweka kwenye mstari wafuasi hao, na badala yake iliwaelekeza kufuata taratibu na kutozuia watumiaji wengine wa barabara.

Tofauti na siku mbili zilizopita ambapo kesi hiyo ilisikilizwa kwa njia ya mtandao, safari hii Lissu alihudhuria mahakamani, na polisi walionekana kuepuka kutumia nguvu kubwa kuwatawanya wafuasi. Badala yake, waliwasihi wakae maeneo ya karibu na Mahakama kwa utaratibu wakati kesi ikiendelea.

Lissu anakabiliwa na kesi mbili; ya uhaini, ambayo ilitajwa na ile ya kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni, ambayo tayari hoja za awali zimesomwa na upande wa mashitaka.

Wakati Lissu akifikishwa mahakamani, takriban askari 16 wenye silaha walikuwa wameimarisha ulinzi nje ya geti kuu la Mahakama ya Kisutu, huku wengine wakiwa maeneo ya jirani pamoja na kwenye magari ya polisi yaliyoegeshwa karibu.

Polisi waliwataka wafuasi wa Chadema kusogea umbali wa takriban mita 100 kutoka geti kuu la mahakama, lakini wanachama hao waligoma wakisema hawavunji sheria na kuwa wamepewa ruhusa kuingia mahakamani kwa utaratibu maalumu.

Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu akisalimiana na Jaji mstaafu wa Kenya, David Maraga.

“Sisi hatuvunji sheria, tumeruhusiwa kuja mahakamani,” walisema. Polisi waliwaomba wasogee nyuma, lakini waliendelea kubaki wakiwa umbali wa mita 100 kutoka lango kuu.

Ikumbukwe kuwa siku za nyuma, polisi walikuwa wakitumia nguvu na hata mbwa kuwatawanya watu karibu na mahakama hiyo. Lakini safari hii hali ilikuwa tofauti; raia waliruhusiwa kusimama na hata kuzungumza na polisi bila bughudha.

Lema, Boni Yai wahamasisha utulivu

Wakati kesi ikiendelea, viongozi wa Chadema, Godbless Lema ambaye ni Mjumbe wa kamati kuu ya chama hicho na Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, Boniface Jackob,  maarufu Boni Yai waliwatembelea wanachama waliokuwa nje ya Mahakama na kuwataka waendelee kuwa watulivu. Walipokelewa kwa shangwe kubwa, na wakatoa taarifa ya kinachoendelea mahakamani.

Baadhi ya wafuasi walieleza kuwa baada ya kesi hiyo, walipanga kutembea kwa miguu kutoka Kisutu hadi makao makuu ya Chadema.

Ugawaji wa chakula

Wakati tukio hilo likiendelea, Chadema iligawa chakula cha mchana kwa wafuasi, wapenzi na wapita njia waliokuwepo nje ya Mahakama.

Kauli yao ilikuwa: “Hata Chadema kuna ubwabwa.” Chakula hicho ambacho kilijumuisha ubwabwa, nyama, maharagwe na mboga za majani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *