Ali Kiba, Billnass, Harmonize wageuka asali kwa Nandy

Dar es Salaam, Siku zote mchovya asali huwa hachovyi mara moja, ndivyo ilivyo kwa Nandy linapokuja suala la kazi kwa baadhi ya wasanii wenzake kutoka katika Bongo Fleva ambao ni Ali Kiba, Harmonize na Billnass ambaye ni mumewe wa ndoa.

Hiyo ni kwa sababu hao ndio wasanii pekee ambao Nandy amewapa shavu zaidi ya mara moja katika nyimbo zake baada ya kuona zile za mwanzo walizotoa zimepata mapokezi mazuri kwa mashabiki, hivyo akachovya tena.

Ikumbukwe Nandy aliyetoka kimuziki akiwa chini ya THT kupitia wimbo wake, Nagusagusa (2016) ikiwa ni muda mfupi baada ya kufanya vizuri katika shindano la Tecno Own The Stage huko Nigeria, amefanya mengi katika muziki wake.  

Tayari ametoa albamu moja, The African Princess (2018), EP tatu, Wanibariki (2021), Taste (2021) na Maturity (2022), amefungua rekodi lebo yake, The African Princess, amefanya kazi na Epic Records, Ziiki Media, huku akishiriki Coke Studio Africa.

Je, ni kwa namna gani Nandy ambaye ni mshindi wa Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) 2023 kama Msanii Bora wa Kike amewageuza Alikiba, Billnass, Harmonize asali akichovya zaidi ya mara moja?. Hivi ndivyo mambo yalivyo.

Harmonize
Ikiwa ni takribani mwaka mmoja tangu Harmonize kuachana na WCB Wasafi, lebo iliyomtoa kimuziki, ndipo Nandy alimvuta studio na wakarekodi wimbo, Acha Lizame (2020) uliotengenezwa na Kimambo.

Ni wimbo uliopata mapokezi mazuri kwa sababu ilikuwa mara ya kwanza kwa Nandy kufanya kazi na msanii mwenye vinasaba vya WCB Wasafi kutokana hana ukaribu wa kikazi na lebo hiyo kuanzia Mkurugenzi wake, Diamond Platnumz.

Miaka minne mbele Nandy anamshirikisha tena Harmonize katika wimbo wake, Usemi Sina (2024) uliotoka hivi karibuni na sasa anafanya vizuri hasa YouTube ambapo amefika namba moja katika chati yake.

Ukiachana na Nandy, Harmonize ameshirikishwa sana na wasanii wa kike, wengine ni Queen Darleen (Mbali), Maua Sama (Niteke Remix), Abigail Chams (Closer) na Anjella (Kama, Kioo & Toroka) ambaye alimsaini katika lebo yake, Konde Music Worldwide.

Billnass
Kwa sasa Nandy anatamba na wimbo wake, Totorimi (2024) akimshirikisha Billnass ukiwa ni wa kwanza kutoa tangu wamefunga ndoa hapo Julai 16, 2022 ikiwa ni takribani miaka sita ya uhusiano wao ulioanzia katika tamasha la Fiesta.

                     

Na kabla hawajafunga ndoa, Nandy alimpa shavu Billnas katika ngoma yake, Do Me (2020), kwa ujumla wawili hao wameshirikiana katika nyimbo tano, nyingine ni Bugana (2019), Party (2021) na Bye (2022),  

Wawili hao ambao ni wazazi wa mtoto mmoja Naya, video ya wimbo wao mpya, Totorimi (2024) imewakosha wengi baada ya kumpa nafasi dada wao wa kazi za ndani Memo uhusika katika video hiyo iliyosimamiwa na Director Kenny.

Alikiba
Ukiachana na Billnass, Alikiba kutokea Kings Music ni msanii mwingine Bongo ambaye Nandy anashabiana naye sana katika muziki wakiwa tayari wametoa nyimbo tatu pamoja huku mbili kati ya hizo zikiwa za The African Princess huyo.

                       

Nandy ndiye alianza kumpa shavu Alikiba katika wimbo wake, Nibakishie (2020) ambao picha zilizopigwa katika utayarishaji wa video yake ziligeuka gumzo mtandaoni ukingatia wakati huo tayari alishaweka wazi uhusiano wake na Billnass.