Algeria yaadhimisha miaka 70 tangu yalipoanza Mapinduzi ya kuutokomeza ukoloni wa Ufaransa

Algeria jana iliadhimisha mwaka wa 70 wa kuanza Mapinduzi ya ukombozi wa nchi hiyo dhidi ya mkoloni Ufaransa kwa gwaride la kijeshi lililofanyika katika mji mkuu Algiers.

Akiwa ndani ya kifaru, Rais Abdelmadjid Tebboune alishiriki katika gwaride hilo, huku akitoa saluti kuusalimia umati mkubwa wa watu waliokuwa wakishangilia kabla ya kuongoza sherehe hizo.

Mnamo Novemba 1, 1954, Harakati ya Taifa ya Ukombozi  ya Algeria FLN ilizishambulia ngome na vituo vya Wafaransa nchini humo na kuanzisha rasmi Vita vya Algeria ambavyo ndivyo vilivyopelekea nchi hiyo kupata uhuru kutoka kwa Ufaransa.

Gwaride la maadhimisho ya Mapinduzi ya Algeria

Nchi hiyo ilitangaza uhuru wake rasmi Julai 5, 1962, baada ya vita vya umwagaji mkubwa wa damu vya miaka saba vilivyohitimisha miaka 132 ya utawala wa kikoloni.

Vita hivyo, ambavyo viongozi wa Algeria wanasema viliua watu wapatao milioni 1.5, vimebaki kuwa nukta ya mvutano katika uhusiano kati ya Algeria na Ufaransa.

Maadhimisho hayo ya mapinduzi ya Algeria mara nyingi hutumiwa kama tukio la utoaji msamaha kwa wafungwa.

Ihsane El Kadi, mwandishi wa habari nchini Algeria ambaye alikuwa sauti kuu wakati wa maandamano ya demokrasia ya 2019 ya nchi hiyo, aliachiliwa kutoka gerezani Alkhamisi jioni pamoja na watu wengine wanane ambao walifungwa jela baada ya kuikosoa serikali…/