
Dar es Salaam. Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT), imependekeza kufanyika mabadiliko ya mwongozo unaoruhusu kuuzwa magari yaliyotumika na Serikali Kuu kwa umbali wa zaidi ya kilomita 200,000, ikitaka yagawiwe kwa halmashauri.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa ALAT Murshind Ngeze, idara kama maendeleo ya jamii na ukaguzi wa ndani katika halmashauri ni muhimu lakini mara nyingi wasimamizi wake wanakosa vitendea kazi yakiwemo magari, hivyo wakipata hata yaliyozidi kilomita 200,000 yatasaidia.
Wakati Ngeze akitoa pendekezo hilo jana Jumatano, Machi 19, 2025, watumishi ngazi ya halmashauri wanasema kufanya hivyo ni kuziongezea halmashauri mzigo wa gharama za matengenezo ya magari hayo kwa kuwa yameshachoka.
Hata hivyo, mapendekezo ya Ngeze yanalenga mwongozo wa Serikali unaotafsiri gari chakavu ni lile lililotumika kwa zaidi ya kilomita 200,000, linapaswa ama kuuzwa kwa mtu binafsi au kumkopesha mtumishi.
Ngeze ameyasema hayo Dar es Salaam, alipozungumza na waandishi wa habari ikiwa ni wiki moja baada ya kufanyika kwa mkutano mkuu wa jumuiya hiyo jijini Dodoma.
Amesema baadhi ya idara ndani ya halmashauri zinakwama kutekeleza wajibu wake kutokana na kukosekana vitendea kazi yakiwemo magari.
“Idara kama maendeleo ya jamii ndio inayohusika na utoaji mikopo ya asilimia 10 na ufuatiliaji wa madeni na hata utoaji elimu kwa wananchi, ikitokea hawana usafiri inakuwa changamoto,” amesema.
Kwa sababu katika halmashauri kuna magari yaliyozidi kilomita 500,000, amesema ni vema yale ambayo mwongozo wa Serikali Kuu unataka yauzwe, yasiuzwe badala yake zigawiwe halmashauri ziyatumie.
“Mimi kwenye halmashauri ninayohudumu (Bukoba) kuna gari la tangu mwaka 1993 na bado linafanya kazi, tunaomba Serikali ifanyie marekebisho huu mwongozo ili magari yaliyotumika na Serikali Kuu kwa zaidi ya kilomita 200,000 yasiuzwe bali yagawiwe kwa idara za halmashauri,” amesisitiza.
Halmashauri yapinga
Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Ubungo (DED), Aron Kigurumjuli amesema pendekezo hilo ni hatari kwa halmashauri kwa kuwa zitaongeza gharama za matumizi.
Gharama hizo, Kigurumjuli amesema zitatokana na matengenezo ya magari hayo kwa kuwa yameshachoka kiasi cha kuhitaji marekebisho ya mara kwa mara.
“Kama Serikali Kuu imeshindwa na ikaona iliuze gari, halmashauri itawezaje kumudu hizo gharama za matengenezo, ukizingatia halmashauri nyingi hazijamudu hata kujitegemea, zinaitegemea Serikali Kuu,” amesema.
Pia, amesema mwongozo unaotumika na Serikali Kuu ndio huohuo uliopo hata serikali za mitaa, hivyo gari isiyofaa eneo moja haitafaa kwingineko kokote serikalini.
“Halmashauri sio eneo la kutupa vibovu, lakini mwongozo wa magari chakavu wa Serikali ndio huohuo unaotumika hata halmashauri kwa kuwa nayo ni Serikali, huwezi kusema Serikali Kuu gari fulani halifai lakini halmashauri linafaa hapana,” amesisitiza.
Katika mkutano wake huo, Ngeze ameahidi mamlaka za mitaa zitatekeleza maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyetaka kuongezwa ukusanyaji mapato na kusimamiwa kwenye matumizi.
Lingine, amesema halmashauri hizo zitazingatia kuweka mipango yao kwendana na mpango wa maendeleo wa nchi wa mwaka 2050.
“Amewataka kubuni vyanzo vipya vya mapato ili halmashauri zijitegemee badala ya kutegemea Serikali kuu na ametutaka tuzingatie sheria, yote haya tunaahidi kuyazingatia,” amesema.
Sambamba na hayo, amewataka madiwani katika kila kata kufanya mikutano ya hadhara kwenye ngazi zote, ili kueleza utekelezaji wa miradi mbalimbali uliofanywa na Serikali.