
Televisheni ya al Alam imelinukuu gazeti moja la Kizayuni na kuandika kuwa, ndege 15 za kijeshi za Israel zilishirikiana kuiwinda ndege moja tu isiyo na rubani ya Hizbullah ya Lebanon na hazikuweza kuitungua. Tukio lililotokea wakati walowezi wote wa Kizayuni wakiwa wamejichimbia kwenye mashimo kwa kuigopa droni hiyo ya Hizbullah.
Televisheni hiyo ya al Alam imelinukuu gazeti la Kizayuni la Haaretz likifichua mgogoro mkubwa uliomo ndani ya utawala wa Kizayuni na kutoa ushahidi kutoka kwa duru za kiusalama, kijeshi na nyaraka za kuaminika na kuandika: “Ndege 15 za jeshi la anga la Israel ziliiwinda ndege moja tu isiyo na rubani ya Hizbullah, wakati walowezi wote wa Kizayuni wa miji ya kaskazini wakiwa wamekimbilia kwenye mahandaki kwa hofu ya droni hiyo, na licha ya ndege hizo za kijeshi za Israel kuiwinda droni hiyo ya Hizbullah kwa muda wa nusu saa nzima, lakini zilishindwa kuitungua… Kashfa hiyo imetokea katika hali ambayo waziri mkuu Benjamin Netanyahu na waziri wake wa vita Yoav Gallant, usiku na machana wanajigamba kuwa Hizbullah haipo tena.”
Televisheni hiyo ya al Alam imenukuu pia makala ya mwandishi wa gazeti la Rai al Youm, Zaher Andraus ambaye amesema: “Kaskazini mwa Israel, kuanzia Haifa hadi kwenye mpaka wa Lebanon ni eneo la wafu kutokana na mashambulizi ya kila siku na ya mfululizo ya Hizbullah ya Lebanon dhidi ya vitongoji vya walowezi wa Kizayuni. Licha ya Israel kuanzisha vita vya nchi kavu huko kusini mwa Lebanon, lakini maisha katika ardhi za kaskazini mwa Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni yamesimama kikamilifu, barabara ziko tupu, ving’ora vya hatari vinasikika mfululizo bila ya kusita na hali hiyo imekuwa kitu cha lazima hivi sasa kwa Wazayuni waliobakia kwenye maeneo hayo.”