
Dar es Salaam. Baadhi ya viongozi wa Al Ahli Tripoli wameonekana kukiuka masharti katika matumizi ya mlango wa kupita kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ambapo walitaka kutumia mlango waliopita Simba jambo ambalo sio sahihi ndipo walinzi walilazimika kutumia nguvu kwa wageni hao kuwalazimisha kufuata masharti.
Tukio hilo limetokea leo Jumapili Septemba 22, 2024 timu zikiwasili uwanjani huku zikiwa zimesalia dakika chache kabla ya mtanange huo wa marudiano Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya awali kupigwa kwa Mkapa ambapo Simba ndio wenyeji.
Baadhi ya viongozi wa Al Ahli walionekana kulazimisha kutaka kupita mlango wanaoingilia Simba ambao sio sahihi kwa kuwa walielekezwa kupita mlango wanaopitia waandishi wa habari.
Baada ya kuwaelekeza viongozi hao walionekana kutotaka kutii agizo la wasimamizi wa uwanja (Steward) na kuanza kuwarushia maneno na kutoa ishara mbaya.
Jambo hilo liliwalazimu walinzi kutumia nguvu kuwapitisha eneo wanalotakiwa kupita badala ya mlango walioutumia Simba.
Mchezo wa kwanza uliopigwa Libya baina ya timu hizo uliisha kwa suluhu ambapo mshindi kati yao atafuzu hatua ya makundi.