Akutwa amefariki ndani, mlango umefungwa kwa kufuli

Shinyanga. Wande Mbiti (38), mkazi wa Kitongoji cha Busalala, Kijiji cha Nhelegani, Kata ya Kizumbi, mkoani Shinyanga, mwenye ulemavu wa ngozi (albino), amekutwa amefariki dunia ndani ya nyumba aliyokuwa akiishi huku mlango wa nyumba hiyo ukiwa umefungwa kwa kufuli kwa nje.

Tukio hilo limebainika jana, Jumapili, Machi 2, 2025, saa saba mchana baada ya wakazi wa eneo hilo kusikia harufu kutoka katika nyumba hiyo na kutoa taarifa kwa mwenyekiti wa kitongoji, Kulwa Sheka.

Sheka amesema alipigiwa simu na kuambiwa kuwa kuna kitu kinatoa harufu katika nyumba hiyo. Alipofika, alitoa taarifa kwa polisi wa kata, ambao walibomoa dirisha na ndipo walipouona mwili wa marehemu.

Wananchi wakibomoa mlango wa nyumba alikofia Wande Mbiti katika kitongoji cha Busalala kijiji cha Nhelegani kata ya Kizumbi Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga.

Amesema baadaye walibomoa mlango.

Diwani wa Kizumbi, Ruben Kitinya, ameeleza namna alivyopata taarifa za kifo cha Wande, akisema: “Mchana tulipata taarifa kutoka kwa mwenyekiti wa kitongoji. Tulivyokuja, tukakuta mlango umefungwa kwa kufuli. Tukaamua kubomoa mlango. Hali na mazingira tuliomkuta nayo mwenzetu si mazuri, na ndiyo maana tunaliachia Jeshi la Polisi liendelee na kazi yake. Hatuwezi kuthibitisha chochote,” amesema Kitinya.

Kwa upande wake, Mbiti Kulwa, baba mzazi wa marehemu Wande, amesema aliondoka hapo nyumbani kipindi cha utawala wa Mkapa (marehemu Rais Benjamin Mkapa) baada ya kutengana na mama wa marehemu na kueleza namna alivyopokea taarifa hizo.

“Nilipigiwa simu na wenzangu nikaambiwa niwahi. Nilipofika, nikakuta mwanangu amefariki. Hapa nyumbani nina muda mrefu tangu niondoke kipindi cha utawala wa Mkapa baada ya kutengana na aliyekuwa mke wangu. Niliwaacha hapa na mama yake, nasikia na yeye aliondoka, akawa anaishi peke yake,” amesema Kulwa.

Wananchi wakisitiri mwili wa marehemu baada ya uchunguzi wa Polisi wa awali.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga, Kennedy Mgani, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, na uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa hakuna dalili zozote zinazoonyesha marehemu aliuawa.

“Taarifa hizo tulizipokea jana saa 12 jioni, na kutokana na uchunguzi wa awali, hakuna kitendo chochote cha ukatili alichofanyiwa marehemu. Baada ya hapo, tuliruhusu baba mzazi, akishirikiana na wananchi, kumsitiri Wande Mbiti maana mwili ulikuwa umeharibika sana,” amesema Mgani.