
KILE kilichofanywa na Simba kwa winga wao Ladack Chasambi aliyejifunga kule Babati walipocheza na Fountain Gate ni babu kubwa sana hata hapa kijiweni tulipongeza.
Ni jambo la kawaida linalopaswa kufanywa na timu au hata wadau wa michezo pindi mchezaji hasa mwenye umri mdogo anapokosea uwanjani ili kulinda kipaji chake na sio vinginevyo.
Kuna namna mchezaji anarudisha hali ya kujiamini na hapotezi utulivu wake pindi anapoona wachezaji wenzake, viongozi, benchi la ufundi na hasa mashabiki wa timu yake wanasimama upande wake na kumuunga mkono kama walivyofanya Simba kwa Chasambi.
Sasa Yanga kulitokea ishu inayofanana kidogo na ile ya Chasambi ambayo ilikuwa ni kosa la kipa Abubakar Khomeiny la kupangua vibaya mpira katika mechi dhidi ya Mashujaa na kuwapa fursa wapinzani wao kupata bao la pili ingawa mechi ilimalizika kwa Yanga kushinda mabao 3-2.
Wachezaji wenzake, viongozi na benchi la ufundi baada ya mechi ile wamejitahidi kusimama na Khomeiny lakini kundi kubwa la mashabiki wa Yanga, halimtazami wala kumsema vyema kipa huyo jambo ambalo linaweza kuchangia kumshusha kisaikolojia.
Wanamtazama kama kipa fulani hivi ambaye hana hadhi ya kuchezea Yanga wakati siku chache nyuma kabla ya kucheza na Mashujaa alililinda vyema lango lao katika mechi dhidi ya Coastal Union, Namungo na TP Mazembe.
Kitu ambacho Simba ilikifanya kwa Chasambi kilipaswa kufanywa na Yanga kwa Khomeiny kwa vile bado ana kipaji na umri wake unampa fursa ya kurekebisha mapungufu yake na kutoa mchango kwa muda mrefu ndani ya timu hiyo.
Ifahamike mchezaji wa soka kukosea ni jambo la kawaida na halipaswi kumfanya aonekane kama hana hadhi ya kuchezea timu wakati huo anaonyesha kipaji na jitihada za kuimarika baada ya kukosea au kuigharimu timu.
Khomeiny pia anapaswa kuchukulia hilo lililotokea kama changamoto ya kumfanya aimarike zaidi badala ya kumtoa mchezoni.