AKILI ZA KIJIWENI: Tuwaache Azam FC waendeshe timu yao

BAADA ya Azam FC kutolewa kwenye Kombe la Muungano, watu wanaishambulia sana kwa maneno haipo siriazi, kwa nini inatolewa katika mashindano kama hayo na timu kama JKU.

Kwa mfano hapa kijiweni ambao wanaongoza kwa kuishambulia kwa maneno Azam, ni jamaa zetu wa zile timu mbili kubwa ambazo zipo pale karibu na lile soko maarufu la Dar es Salaam.

Wengine wamefika mbali zaidi hadi kufikia hatua ya kuipangia familia ya Mzee Bakhresa nini cha kufanya eti kama vipi iachane na habari za kuihudumia Azam na hizo fedha izitumie kwa shughuli nyingine maana timu haiipi faida.

Hili jambo linashangaza kidogo maana kwanza hela ni zao na wenyewe familia ya Bakhresa ndio wanajua wazitumie vipi badala ya kupangiwa na kina sie ambao hatuchangii hata robo ya gharama za uendeshaji wa timu.

Lakini kitu kingine hawa mashabiki wa hizi timu zetu kubwa waache unafiki wa kujifanya wana uchungu sana na Azam wakati kiuhalisia hawataki kuona inafanya vizuri na ikizigusa timu zao wanajaa mapovu ya hasira.

Hiyo Azam ambayo leo wanajidai wanaumia kuona ikifanya vizuri, ndio huwa wanaiongelea vibaya pindi ikizifunga timu zao na kuziharibu hesabu zao za kutwaa ubingwa wa ligi au mashindano mengine.

Wanasahau wao ndio wanajifanyaga Azam ifanye vizuri kitu ambacho ili kitokee basi timu zao zinapaswa pia ziwe zinafungwa maana ili Azam iwe bingwa basi zinazotakiwa kufungwa pia miongoni ni timu zao.

Ni walewale ambao Azam, ikichukua mchezaji nyota na tegemeo kutoka kwenye timu zao hasira zinawajaa vifuani hadi kutishia kutonunua bidhaa lakini wao hukenua hadi jino la mwisho pindi timu zao zikichukua mchezaji au wachezaji tegemeo wa wauza Aiskrimu.

Kuna husemi unasema kama hauwezi kukinufaisha basi usikidhuru hivyo wazee wa Kariakoo kama hamuwezi kuinufaisha Azam basi msiidhuru.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *