TETESI ambazo hapa kijiweni tulikuwa tunaziona haziwezi kuwa kweli hatimaye zimetimia nazo ni ndoa ya Stephane Aziz Ki na Hamisa Mobeto.
Mastaa wawili ambao mapenzi yao yalianza kama utani na sasa wanakaribia kufunga ndoa kabla ya mwezi Mtukufu wa Ramadhan na imepangwa kuwa Februari 18 mwaka huu.

Penzi lao limekuwa habari ya mjini hasa kwani wote wawili ni watu wenye majina makubwa nchini, Aziz Ki akitamba katika soka na Hamisa Mobeto katika muziki na kazi nyingine za kisanaa.
Kama ni kunufaika basi Tanzania ambayo ni nyumbani kwa Hamisa Mobeto tutanufaika zaidi kuliko huko Burkina Faso ambako Aziz Ki ndio anatokea.

Kuna uwezekano mkubwa Aziz Ki akanunua nyumba au kujenga hapa ili familia yake iweze kukaa kwa utulivu maana wote tunafahamu kuwa mwanamke huwa na nguvu mbele ya mwanamume.
Inawezekana Aziz Ki akaenda timu ya nje ya nchi lakini ni vigumu kwa Hamisa Mobeto kuhamia huko kwa vile na yeye ana shughuli nyingi hapa ambazo zinamuingizia fedha na alianza kuzifanya kabla hata hajakutana na nyota huyo wa Burkina Faso.
Maana yake pia nchi itaendelea kunufaika na mapato kutoka kwa Aziz Ki iwe anaendelea kucheza soka la kulipwa hapahapa au awe amepata timu kwingineko tofauti na kama mchezaji huyo angeoa kwao Burkina Faso.

Kuna kitu mtaani tunamuomba Mungu awajalie Aziz Ki na Hamisa Mobeto katika ndoa yao nacho ni mtoto wa kiume ambaye atakuwa anajua kupiga kabumbu kama baba yake.
Angalau na sisi tuanze kuonja ladha ya kuwa na damu ya kutoka Afrika Magharibi ikitumikia timu zetu za taifa.