AKILI ZA KIJIWENI: Singida Black Stars sasa iwakumbuke wa nyumbani

KIJIWE kinatoa hongera nyingi kwa Chui wa Singida, Singida Black Stars kwa kujenga uwanja mzuri wa nyasi bandia ambao utatumiwa na kikosi cha timu hiyo kwa mazoezi na hata mechi.

Haya ni maendeleo makubwa kwa mpira wetu kuona mkoa kama wa Singida unapata uwanja mzuri na hivyo kuendelea kupunguza namba ya viwanja vyenye eneo lisiloridhisha la kuchezea ambalo linafanya mpira usichezeke. Vizuri.

Ligi yetu imepanda viwango bhana, hivyo lazima tuwe na viwanja vizuri vinavyoendana na ukubwa wetu sasa hivi na siyo viwanja vyenye eneo la kuchezea kama majaruba ya mpunga.

Ukienda Singida na timu yako sasa hivi basi usiwe na presha kwani uwanja wa kufanya boli litembee upo ni wewe mwenyewe tu kwenda pale na vipengele vyako ila sio vinginevyo.

Baada ya kufanikiwa kujenga uwanja mzuri, ni wakati sasa wa Singida Black Stars kuhakikisha inakuwa timu yenye manufaa makubwa kwa watu wa Singida kwani wahenga walisema siku zote roho nzuri inaanzia nyumbani.

Kama itajenga maduka na maeneo ya kibiashara kuzunguka uwanja huo, kipaumbele cha kwanza kinapaswa kuwa wakazi wa Singida na sio wageni kutoka mikoa mingine ambao mwishowe wakipata mzigo kutokana na vyanzo hivyo, wataanza kuangalia kwanza namna ya kupanufaisha kwao.

Timu za vijana za Singida Black Stars zitoe fursa kubwa kwa watoto wa Singida ili waandaliwe vyema wawe wachezaji wazuri ambao wakija kufanikiwa watarudisha hela nyumbani na kuuendeleza mkoa huo ambao bado haujapiga hatua kubwa kimaendeleo.

Hili litafanya watu wa Singida wajione ni sehemu ya timu na hivyo wataipa sapoti kubwa ambayo itaifanya Singida Black Stars kuwa miongoni mwa timu zenye idadi kubwa ya mashabiki tofauti na ilivyo sasa ambayo inaonekana kuwa ya watu wachache.

Mafanikio ya timu kwa kiasi kikubwa yanachangiwa na sapoti ya nje ya uwanja hasa uwepo wa mashabiki hivyo Singida Black Stars inapaswa kujenga mazingira mazuri ya kuwashawishi Wanasingida kuiunga mkono kwa ukubwa timu yao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *