
WATU wengi tunatamani kuona siku moja wimbo wa taifa la Tanzania unaimbwa huku bendera yetu ikipepea kwenye Fainali za Kombe la Dunia ambayo ndiyo mashindano makubwa ya soka ulimwenguni.
Hapa kijiweni tulipoona FIFA imeongeza idadi ya timu za Afrika kwenye Kombe la Dunia kufikia tisa huku kukiwa na uwezekano wa kuwa 10 kutoka tano zilizokuwa zinawakilisha bara hili hapo mwanzo, ndiyo tukajua muda wa kutoboa umefika.
Maana kwa miaka ya hivi karibuni soka letu limepigapiga hatua kidogo, hivyo tukaona tunaweza kubishana na kuwa miongoni mwa timu tisa zitakazoenda kule Marekani, Mexico na Canada mwakani.
Hata hivyo, wasiwasi ukaanza kutupata baada ya FIFA kupanga makundi ya mashindano ya kufuzu kwa Bara la Afrika na Taifa Stars tukaangukia katika kundi E pamoja na timu za Morocco, Zambia, Niger, Eritrea na Congo.
Hawa kina Niger, Zambia, Congo na Eritrea hawakutuogopesha na tunaamini kabisa tunaweza kuzima nao uwanjani na tukapata pointi na tumeonyesha hilo kwa kuzichapa Niger na Zambia ugenini, ila shida kubwa ni hao wazee wa kazi Morocco.
Jamaa wakaja kwetu wakatufunga mabao 2-0, hapo wakawa wameshaweka rehani matumaini yetu ya kufuzu Kombe la Dunia katika kundi hilo na hawakuishia kwetu tu, wakazichapa timu nyingine za kundi wakakaa zao kileleni.
Juzi tukawafuata kwao katika mechi ya marudiano ambayo waliipania sana hadi kuipeleka huko Oujda ambako ni mbali sana kutoka mji mkuu wa Casablanca huku kikosi chao kikiwa na mastaa kibao wanaocheza soka la kulipwa Ulaya.
Tukajitahidi kweli kuwazuia lakini wakatumia uzoefu wao kutufunga mabao mawili yaliyoamua mchezo ambayo moja lilitokana na mpira wa kona na lingine la mkwaju wa penalti wakazika matumaini yetu ya kuongoza kundi.
Matokeo ya juzi yanauma lakini kiukweli siwezi kumlaumu mtu yeyote kwa Taifa Stars kupoteza. Jamaa walitumia daraja la ubora wao kutuadhibu kwa mipira ya kutenga maana walishatuona tuko bora katika kuwadhibiti kutengeneza mabao kwa njia ya kawaida wakaja na mpango mbadala ambao ulifanikiwa.