
KAPTENI Mbwana Samatta alitupa unyonge sana mwanzoni mwa msimu huu kutokana na kutopata nafasi ya kutosha ya kucheza katika kikosi cha PAOK ya Ugiriki akionekana kutokuwa chaguo la benchi lao la ufundi.
Tuliumia sana hapa kijiweni kwa sababu kuna mambo mengi ambayo tulianza kuyawaza vichwani mwetu kutokana na hilo lililokuwa linatokea kwa ‘El Capitano’ wetu wa Taifa Stars.
Baadhi ya fikra zikaanza kuamini kwamba Samatta anaelekea mwisho wa heshima na daraja ambalo amejijengea katika soka la Ulaya tangu alipoondoka miaka takribani minane iliyopita kwenda Ulaya akitokea TP Mazembe.
Hatukutamani kuona hilo likitokea kwa vile tuliona kama Ugiriki hakuna presha sana kulinganisha na Ubelgiji, England na Uturuki ambako amepitia katika utafutaji wake wa malisho ya kijani Ulaya.
Jambo lililotuumiza zaidi ni kwamba Samatta huu ni msimu wake wa mwisho kwa mujibu wa mkataba wake aliosaini na PAOK wakati anajiunga nayo mwaka 2023 akitokea Fenerbahce ya Uturuki.
Tuliumia kwa sababu angepata wakati mgumu kusaka timu mara baada ya msimu huu kumalizika iwapo angeendelea kusota benchini au kuonyesha kiwango cha chini na mwisho wa yote angeangukia katika timu zinazoshiriki katika ligi za hadhi ya chini duniani.
Anayecheka mwisho ndio hucheka zaidi bhana na nahodha wetu Samatta ameamua kutuonyesha hilo dakika za jiooooooni kutokana na kile ambacho anakifanya hivi sasa ndani ya kikosi cha PAOK.
Jamaa anafunga mfululizo tena mabao ya kitemi na amekuwa akitoa pasi za mwisho na hivyo kuiwezesha timu yake kumaliza katika Top 4 kwenye Ligi Kuu ya Ugiriki.
Kiufupi sasa hivi Samatta amekuwa lulu maana hata kama PAOK walikuwa na mpango wa kumuacha, inawezekana sasa wameshabadilisha mawazo na wakimfuata kuongeza mkataba mpya wao watalazimika kuwa wanyonge kwake na ikishindikana, atapata ofa nono kwingineko.