AKILI ZA KIJIWENI: Mpanzu, Camara wamemaliza deni Simba

AWAMU tano tofauti nyuma Simba ilishindwa kuvuka kutoka hatua ya robo fainali kwenda nusu fainali ya mashindano ya klabu Afrika.

Hili ni jambo ambalo limekuwa likiwatia unyonge sana mashabiki wa mnyama hapa kijiweni kwetu na kwingine hasa ukizingatia watani wao Yanga walifanya hivyo msimu wa 2022/2023 ambao walipenya hadi kucheza fainali.

Maana kila wanapotaka kuzungumzia mashindano ya klabu Afrika, wenzao wa Yanga wanawaita Mwakarobo kwa maana kwamba Simba ni timu ya kuishia hatua ya robo fainali tu na haiwezi kusogea zaidi ya hapo.

Lakini juzi Jumatano, Simba ilimaliza hiyo historia isiyovutia kwa kuifunga Al Masry ya Misri kwa mikwaju ya penalti 4-1 baada ya dakika 90 kumalizika kwa ushindi wa Simba wa mabao 2-0 uliofanya mechi mbili baina ya timu hizo kuisha kwa sare ya mabao 2-2.

Katika dakika 90, Elie Mpanzu alifanya uamuzi mmoja wa faida ambao uliipa Simba bao la kwanza katika dakika ya 22 ambalo lilikuwa muhimu sana kuirudisha timu yake mchezoni alipoamua kuachia kombora kali la mguu wa kulia lililojaa nyavuni baada ya kupokea mpira wa kurusha wa Shomari Kapombe akiwa nje ya boksi la Al Masry.

Baadaye Steven Mukwala akaongeza bao la pili na mechi ikaamuliwa kwenda katika mikwaju ya penalti ndipo kipa Moussa Camara akawa shujaa wa Simba kwa kupangua penalti mbili na kuiwezesha timu yake kushinda kwa mikwaju ya penalti 4-1.

Walichokifanya Mpanzu na Camara juzi hapana shaka kimemaliza deni ambalo wawili hao walikuwa nalo ndani ya Simba kwani tangu waliposajiliwa hadi juzi, hakuna mmoja wao ambaye alifanya tukio kubwa ambalo linaacha historia ndani ya klabu hiyo.

Walikuwa wanacheza vizuri lakini alama ya mchezaji kwenye timu huwa inaachwa kwa namna kama ya juzi ambapo mchango au juhudi binafsi anazofanya zinaamua matokeo yanayoipa timu taji au kuitoa hatua moja kwenda nyingine hasa kama huko nyuma ilikuwa haijafanya hivyo.

Abdallah Kib

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *