AKILI ZA KIJIWENI: Malale Hamsini ameokota dodo PALE Mbeya City

KUNA watu wana bahati zao duniani na mfano wa hao ni kocha Malale Hamsini ambaye hivi karibuni alijiunga na Mbeya City kuwa kocha mkuu.

Tangu alipoachana na JKT Tanzania mwaka jana, alikuwa zake mapumzikoni na baada ya miezi mingi kupita, ameibukia kwa Wana Komakumwanya wa Mbeya ambao wanashiriki Ligi ya Championship.

Malale amejiunga na Mbeya City akichukua nafasi iliyoachwa na Salum Mayanga ambaye amepata ofa ya kujiunga na Mashujaa FC inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo nayo iliachana na kocha wake Mohammed Abdallah ‘Baresi’.

Hapa kijiweni tunaona Mayanga amefanya uamuzi mgumu sana kwa vile amekwenda katika timu ambayo haipo nafasi nzuri kwenye msimamo wa Ligi Kuu lakini yeye ni kocha mkongwe na mzoefu anajua nini cha kufanya na hadi ameamua kutua Mashujaa basi ana hesabu zake ambazo anaamini zitatimia.

Sasa tukirudi kwa Malale Hamsini, tunasema Mungu amemjalia bahati kwa sababu anajiunga na timu ambayo iko katika nafasi nzuri katika Ligi ya Championship na ina uwezekano mkubwa wa kupanda Ligi Kuu msimu ujao hivyo kazi yake yeye ni kumalizia tu mkia.

Mwalimu Mayanga ameamuachia timu nzuri ambayo ilipata ushindi katika idadi kubwa ya mechi za mwanzoni za Ligi ya Championship zilizopelekea iwe katika nafasi za juu na yeye Malale Hamsini amebakisha mechi chache tu za kuhakikisha timu haitoki kwenye mstari na kushindwa kutimiza lengo la msingi ambalo ni kupanda daraja.

Kwa uzoefu na uwezo wa kocha Malale Hamsini, sidhani kama kibarua hiki kitamshinda kwani hii sio mara yake ya kwanza kuinoa timu inayopambana kupanda Ligi Kuu na alishafanikiwa hivyo sasa hivi itakuwa ni kama marudio tu.

Bahati nzuri kwake ni sapoti kubwa ambayo Mbeya City inapata nje ya uwanja kutoka kwa viongozi wa mkoa, viongozi wa timu na mashabiki ambayo ina nafasi kubwa ya kuiweka timu katika morali na hamasa ya kupambana katika kila mechi.

Na kwa namna Mbeya City ilivyojipanga, kuna dalili zote kuwa timu itapanda daraja na Malale Hamsini ataboresha sivii yake kama miongoni mwa makocha hodari wa kupandisha timu Ligi Kuu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *