AKILI ZA KIJIWENI: Kwaheri KenGold mmevuna mlichokipanda

TATHMINI ya kimpira hapa kijiweni imeishusha rasmi daraja KenGold kutoka Ligi Kuu kwenda Ligi ya Championship japo imebakiwa na mechi nne mkononi ambazo ikishinda itapata pointi 12 na ikijumlisha na ilizonazo 16, jumla itakuwa na 28.

Ukiangalia msimamo wa Ligi Kuu, kuna timu kama nne hivi ambazo zinahitaji pointi mbili tu katika michezo ambazo zimebakiza ili zivuke pointi 28 na kuna timu moja ikipata pointi nne tu inavuka pointi hizo ambazo KenGold inaweza kuzipata ikiwa itashinda mechi zake zote zilizosalia.

Sasa ugumu zaidi kwa KenGold unaonekana kuwa katika hizo mechi zenyewe nne ilizobakiza maana hamna hata moja ambayo inaonekana kuwa nafuu kwa upande wake kwa sababu mbalimbali.

Wana mechi mbili ugenini dhidi ya Coastal Union na Namungo FC ambazo nazo hazipo salama katika msimamo wa Ligi Kuu. KenGold imekuwa haina historia nzuri ugenini msimu huu kwani haijawahi kupata ushindi hata mara mara moja.

Nyumbani ina mchezo dhidi ya Pamba Jiji ambayo nayo inapambana kukwepa kushuka daraja huku ikiwa imeimarika sana mzunguko wa pili na ina mchezo dhidi ya Simba inayopigania ubingwa huku ikiwa moto wa kuotea mbali.

Binafsi sioni ni kwa namna gani KenGold itasalia Ligi Kuu na kwa sasa inapaswa kuandaa tu makazi yake katika Ligi ya Championship na ianze mapema mikakati ya kuiwezesha kupanda tena hapo baadaye.

Hata hivyo, ikishuka daraja, KenGold itapaswa ijilaumu yenyewe kwa vile ilishaandaa mazingira ya kufanya vibaya kabla hata msimu haujaanza na ikaendelea kujifelisha wakati msimu unaendelea.

Mwanzoni ilisajili wachezaji wengi wasio na uwezo na uzoefu wa ligi na katika dirisha dogo ikafanya usajili mzuri ingawa ikazembea kuhakikisha baadhi yao wanapata vibali mapema hivyo wakashindwa kucheza mechi nyingi za mzunguko wa pili.

Wakamleta kocha ambaye hakukidhi vigezo vya kuwa kocha mkuu hivyo timu ikawa inakosa huduma yake stahiki wakati wa mechi kwa vile hakuwa anakaa kwenye benchi lakini wakati huohuo walimsajili Bernard Morrison ambaye alikuwa majeruhi na walifahamu fika asingeweza kucheza mechi nyingi.

Leo zimebaki mechi nne na matumaini ya kubaki hayapo ndipo Bernard Morrison anarejea uwanjani inabidi uishie kucheka tu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *