AKILI ZA KIJIWENI: Kaseja sasa ndo ameanza kazi Kagera

SIKU za mwanzoni za Juma Kaseja ndani ya Kagera Sugar baada ya kukabidhiwa ukocha mkuu zilikuwa tamu sana kutokana na mwenendo mzuri ambao timu hiyo ilikuwa nao wakati kipa huyo wa zamani wa Simba alipoanza kazi.

Ikashinda mechi mbili mfululizo za Ligi kisha ikamnyoa mtu kwenye Kombe la TFF mambo yakaonekana kama yameshakaa kwenye mstari chini ya Kaseja ambaye aliwahi pia kuwa kocha wa makipa wa haohao Kagera Sugar.

Stori hapa kijiweni kwetu zikawa ni za kummwagia maua tu Kaseja tukiamini ndio mkombozi wa Kagera Sugar ambayo tangu msimu ulipoanza haikuwa inafanya vizuri hadi ikasababisha iachane na makocha wawili tofauti ambao ni Nkata Paul na baadaye Melis Medo.

Hatukutaka kuamini kwamba inawezekana Kagera Sugar ilikuwa inafanya vizuri zile mechi za mwanzo ikiwa chini ya Kaseja kwa sababu ya morali tu ambayo mara kwa mara huwa inaibuka pale timu inapobadili makocha.

Hata hivyo, kitendo cha kupoteza mechi tatu mfululizo baadaye kinamuweka katika wakati mgumu sana Kaseja kwani kimemuathiri katika maeneo mawili ambayo kwanza ni katika Ligi Kuu na jingine ni kwenye Kombe la TFF.

Kufungwa mabao 2-0 na Singida Black Stars kumeifanya Kagera Sugar itolewe kwenye mashindano na athari ya pili ni kushuka hadi katika nafasi mbili za mwisho kwenye msimamo wa ligi baada ya kupoteza mechi dhidi ya Tanzania Prisons na Dodoma Jiji.

Sasa Kaseja anakabiliwa na mechi nne ngumu mbele yake ambazo akifanya vizuri atatupa cha kusema sisi tunaomkubali uwezo wake lakini ikishindikana maana yake atatupa kazi ngumu kumtetea.

Mechi hizo inayofuata nyumbani dhidi ya Azam FC na nyingine ya Mashujaa FC kisha atakuwa na mbili ugenini dhidi ya Namungo na Simba ambazo anapaswa kuvuna idadi kubwa ya pointi ili abaki Ligi Kuu.

Ugumu wa hizo mechi na nyakati anazopitia Kaseja ndani ya Kagera Sugar vitafutika iwapo atakusanya pointi za kutosha katika hizo mechi nne ilizobakiza vinginevyo itakuwa mtihani kidogo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *