ULE mchezo ambao Ladack Chasambi alijifunga bao ambalo lilikuwa la kusawazisha kwa Fountain Gate dhidi ya Simba ungeweza kuwa mwanzo wa maisha magumu kwa winga huyo mwenye umri wa miaka 20.
Maana tayari kulishaanza maneno maneno kutoka kwa baadhi ya mashabiki hoyahoya wakidai kuwa dogo alifanya lile tukio kwa makusudi kisa tu kuna siku alisema kuwa ndani ya Simba hana mchezaji anayemtazama kama mfano kwake.

Na upande wa pili nako wakawa hawako nyuma kwa kumkejeli dogo hadi bwana yule naye akaamua kutengeneza jezi yenye jina la Chasambi na ilionekana kwao lengo lilikuwa ni kutumia fursa hiyo kuwavuruga Simba.
Hapa kijiweni tuliona hayo kama mambo ya kishamba kwa vile suala la mchezaji kujifunga ni la kawaida kwenye soka.
Ni vile tu sisi wengi wetu tunaanza kupenda timu na siyo mpira ndiyo maana tunajikuta tunaumia kupitiliza yakitokea matukio kama la Chasambi.
Hata hivyo, kuna watu wawili Simba ambao walichangia kwa kiasi kikubwa kulipooza suala hilo na kumrudishia Chasambi hali ya kujiamini hadi akaweza kufunga bao katika mchezo dhidi ya Tanzania Prisons.

Wa kwanza ni Azim Dewji ambaye ni mfadhili wa zamani na mtu mwenye heshima kubwa ndani ya Simba aliyeitisha mkutano na vyombo vya habari na kuwasihi mashabiki wa timu hiyo kumuunga mkono dogo badala ya kumtoa mchezoni.
Baadaye kocha Fadlu Davids naye akasisitiza kitu kama hicho huku akisema wao upande wa benchi la ufundi wako pamoja na Chasambi na watahakikisha wanamlinda kwa hali na mali kuhakikisha lililotokea babati haliwi chanzo cha kupotea kwake.

Katika mechi dhidi ya Tanzania Prisons akamuanzisha katika kikosi cha kwanza jambo ambalo lilizaa matunda kwa mchezaji huyo kufunga bao huku akionyesha kiwango bora.
Fadlu Davids na Azim Dewji hapana shaka wamefanya jambo kubwa ambalo litabaki kichwani mwa Ladack Chasambi kwa muda mrefu.