AKILI ZA KIJIWENI: Dabi ya Kariakoo iheshimiwe jamani

KESHOKUTWA mida ya saa 1:15 usiku kitaanza kuwaka pale kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa mechi moja tamu sana ya watani wa jadi, Yanga na Simba, zinapokutana kwenye mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara.

Hii mechi wote tunakubaliana kwamba imeshikilia hatima ya ubingwa na timu ambayo itafungwa hapo isijipe kabisa imani kwamba itaweza kutoboa katika mechi zitakazobakia na kutwaa ubingwa.

Huu ndio mchezo mkubwa na wenye hadhi ya juu katika soka la ngazi ya klabu na timu hizo mbili zinapokutana nchi inasimama kwa muda kuziacha zimalizane na baada ya hapo shughuli zinaendelea kama kawaida sio mchezo kwa kweli.

Na uhondo wa mechi hii hauishii hapa ndani tu bali hata kwa mataifa mengine yamekuwa yakifuatilia mchezo huo kwa vile unahusisha miongoni mwa timu kongwe barani Afrika na żenye idadi kubwa ya mashabiki.

Sasa basi heshima hiyo ya Dabi ya Kariakoo inapaswa kulindwa kwa wahusika wote wa mchezo kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwa mujibu wa kanuni na taratibu badala ya kufanya kinyume jambo ambalo linaweza kututia doa.

Timu ziache kuendekeza imani za kishirikina katika mechi kama hiyo kwani kwa kufanya hivyo zinaweza kuathiri wachezaji kisaikolojia na wakashindwa kufanya vyema au zinaweza kusababisha adhabu za faini na fedha ambazo zinazigharimu.

Mashabiki waingie na kushangilia kistaarabu pasipo kuharibu utaratibu unaotumika hivi sasa na walinde miundombinu ya uwanjani hasa mabomba ya maliwatoni kwani wakishindwa kuyatunza ipo siku mambo yatakuja kuharibika.

Watu wengine muhimu ambao wanapaswa kuhakikisha wanaipa heshima na hadhi kubwa ni marefa. Wachezeshe vizuri mechi ikiisha tujadili viwango vya timu na wachezaji na sio wao.