
HADI sasa bao bora katika Ligi Kuu msimu huu kwa mujibu wa kura zilizopigwa hapa kijiweni ni lile la Seleman Rashind ‘Bwenzi’ alilopachika dhidi ya Yanga.
Jamaa alifunga bonge la bao kwa kumtungua kipa hodari wa Yanga, Djigui Diarra akiwa katikati ya uwanja na alipiga shuti la mbali lililomshinda kipa huyo kutoka Mali na kujaa wavuni.
Kuna kamjadala kalitaka kuanza bao lile lisingehesabiwa iwapo Diarra asingeugusa ule mpira lakini sio kweli. Hata kipa wa Yanga asingeugusa lile bao lingehesabiwa kwa vile ule sio mpira wa pigo lisilo la moja kwa moja.
Sheria inafafanua mpira unaoanzishwa katikati baada ya timu kufungwa bao unahesabika ni bao ikiwa utaingia moja kwa moja golini lakini kama utaingia katika lango la timu inayopiga basi wapinzani watazawadiwa pigo la kona.
Sasa kumfunga kipa mzuri kama Diarra tena mfungaji ukiwa katikati mwa uwanja sio jambo rahisi na ndiyo maana hapa kijiweni wote kwa kauli moja tumekubaliana lile hadi sasa ndiyo bao bora hadi ikitokea mwingine akafunga zuri zaidi ya la Bwenzi.
Bao lile linaonekana kuchangia kwa kiasi kikubwa kumwongezea konfidensi Bwenzi kwani akaja kufunga tena katika mechi iliyofuata ambayo KenGold ilipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Fountain Gate ambao ikaifanya timu hiyo kufikisha pointi tisa kwenye ligi.
Tunaamini mwanzo mzuri wa Bwenzi KenGold utakuwa ndiyo tiketi kwake kuikamata ligi ya Tanzania baada ya kusota kwa miaka kadhaa katika timu mbalimbali bila mafanikio hadi pale alipoibukia timu hiyo ya kule Chunya, Mbeya.
Kwa sasa yeye ndiyetegemeo pale maana aliyetegemea kuibeba, Bernard Morrison kwa sasa yupo nje ya uwanja akiuguza majeraha yake ambayo yatamfanya akosekane kwa mechi kadhaa.
Wanasema mvumilivu hula mbivu na huenda usemi huu tukaushuhudia kwa Seleman Bwenzi pale KenGold.