AKILI ZA KIJIWENI: Ateba abadilike Simba inamtegemea

JANA Lionel Ateba katukwaza sana hapa kijiweni baada ya mchezo wa kwanza wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baina ya Al Masry na Simba uliochezwa kule Misri.

Kulikuwa na makundi mawili yaliyotibuliwa nyongo na Ateba mara baada ya mechi hiyo iliyomalizika kwa Simba kufungwa mabao 2-0 ambayo tuliitazama kwa pamoja katika banda la jirani na kijiwe chetu kilipo.

Kundi la kwanza ni kina sisi ambao tuliweka mikeka yetu tukiamini Simba itapata goli au magoli na baadhi wakaipa Simba odi ya kutopoteza mechi hiyo tukiamini wale Al Masry ni wepesi tu mbele ya mnyama.

Na mnyama alitengeneza nafasi kibao ambazo nyingi zilipotezwa na Ateba ambaye alionekana kuwa na mawenge kweli mbele ya lango la Al Masry hadi kukosa mabao mengi ambayo angeweza kufunga kama tu angetuliza kichwa chake vizuri.

Kundi la pili ni mashabiki wa Simba ambao walikuwa wanatamani timu yao iimalize shughuli ugenini na ikija hapa Dar es Salaam isiwe na presha kubwa bali icheze mechi ya kukamilisha ratiba tu.

Hivyo mabao aliyokosa juzi wanaona yameipa timu yao mlima mrefu wa kupanda katika mechi ya marudiano itakayochezwa Jumatano ijayo ili iweze kuingia hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo.

Hii sio mara ya kwanza kwa Ateba kuzingua kwa kukosa mabao mengi licha ya kupata idadi kubwa ya nafasi kwenye lango la timu pinzani na sababu mara kwa mara inakuwa ni yeye mwenyewe kukosa utulivu na pia kutokuwApo katika sehemu sahihi kwa wakati.

Kwa mchezaji wa hadhi yake hatakiwi kufanya mambo kama hayo kwa vile Simba ilimsajili ikiamini atawavusha kutoka hatua moja kwenda nyingine na kukiimarisha kikosi chao hasa kwenye mashindano ya kimataifa.

Lakini kama hafanyi hivyo na badala yake anaigharimu timu, hakuna sababu ya Simba kuendelea kutumia mamilioni ya fedha kuwa naye kikosini wakati harudishi thamani hata nusu ya kile ambacho klabu inatumia kwake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *