
Dar es Salaam. Ili kurahisisha utafutaji taarifa mtandaoni kampuni ya Google inayomiliki Akili Mnemba (AI) ya mazungumzo ya Gemini imeamua kuiweka programu hiyo kwenye kipengele cha kutafuta cha ‘Google Search’.
Hatua hiyo inatajwa kumrahisishia mtumiaji kutafuta taarifa sambamba na kumpa uzoefu wa matumizi ya Akili Mnemba.
Ikumbukwe Akili Mnemba ni teknolojia inayowezesha kompyuta na mashine kuiga uwezo wa binadamu kama vile kujifunza, kufikiri, kufanya uamuzi, na kuwa na ubunifu katika sekta mbalimbali kama afya, elimu, fedha, soko na mawasiliano.
Miongoni mwa zana za Akili Mnemba za mazungumzo ‘AI Chatbots’ kutoka kampuni tofauti za teknolojia ni ChatGPT, Gemini, Microsoft Copilot, Claude, Youchat, Ada na Cleverbot zinasaidia kurahisisha kazi, kuchambua data, uamuzi wa kibiashara au binafsi au hata kufundishia.
Google imetoa taarifa hiyo jana kwenye kongamano la kila mwaka la wataalamu wa programu huko California, Marekani ikiwa ni sehemu ya juhudi za kampuni hiyo kubwa ya teknolojia kubaki na ushindani dhidi ya ChatGPT na huduma zingine za Akili Mnemba, ambazo zinaitishia Google kwenye utafutaji wa mtandaoni.
Mtendaji Mkuu wa kampuni tanzu ya Google iitwayo Alphabet, Sundar Pichai amesema ujumuishaji wa ‘chatbot’ ya Gemini ni awamu mpya ya mabadiliko ya jukwaa la Akili Mnemba.
“Kwa uwezo wa kufikiri ulioendelea kuboreshwa, unaweza kuuliza maswali marefu na magumu zaidi,” amesema Pichai akinukuliwa na BBC.
Mtumiaji wa mtandao wa intaneti, David Nestory ameiambia Mwananchi Digital kuwa hatua hiyo itarahisisha utafutaji wa taarifa na majibu ya maswali magumu.
“Itarahisisha muda wa kutafuta kwa kuwa ukiingia Google utaona tu Gemini ipo pale unauliza kwa haraka,” amesema.
Katika hatua nyingine kampuni hiyo imekuja na miwani inayotumia Akili Mnemba ikiwa ni zaidi ya muongo mmoja baada ya kuzindua miwani janja na “Google Glasses” ambayo haikufanya vizuri sokoni.
Miwani hiyo mpya ya Google inatengenezwa kwa kushirikiana na wauzaji wa miwani Warby Parker na Gentle Monster itakuwa na kamera, maikrofoni na spika ambayo inaweza kutumika hata katika shughuli za uandishi wa habari.
Hata hivyo, Google inatarajia kushindana na miwani inayotumia akili Mnemba ya kampuni ya Meta iliyotengenezwa na Ray-Ban.