Dar es Salaam. Joto la kuomba kuteuliwa kupeperusha bendera kwenye nafasi ya urais wa Tanzania katika uchaguzi mkuu 2025 kwa tiketi ya Chama cha ACT- Wazalendo limeendelea kupanda, baada ya Aaron Kalikawe kuchukua fomu ya kuomba ridhaa hiyo.
Kalikawe anayetokea tawi la NHC, Bukoba Mjini, mkoani Kagera sasa anakuwa kada wa pili akitanguliwa na kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu aliyechukua fomu kuomba ridhaa ya kuteuliwa.
Hata hivyo, huenda idadi ya makada wa kuomba ridhaa hiyo ikaongezeka kwani bado siku 19 hadi kufungwa rasmi kwa pazia hilo lililofunguliwa Aprili 18, 2025 kwa tangazo la Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu.
Kalikawe kama alivyofanya Dorothy, alichukua fomu hiyo Makao Makuu ya chama hicho, Magomeni jijini Dar es Salaam na kukabidhiwa na Katibu wa Oganaizesheni, Mafunzo na Uchaguzi, Shaweji Mketo.

ACT- Wazalendo pamoja na vyama vya CUF, Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Chama cha Ukombozi wa Umma (Chauma) wapo kwenye hatua za mwisho kuwajua wagombea wao.
Wanatakiwa kukamilisha mchakato huo ili kuungana na vyama vya CCM, UPDP, NLD, AAFP na NCCR- Mageuzi ambavyo tayari vilishakamilisha hatua ya kuwajua wagombea wao katika uchaguzi mkuu.
Akizungumza Dar es Salaam jana Jumanne Mei 6, 2025 baada ya kukabidhiwa fomu hiyo, Kalikawe amesema amechukua uamuzi wa kuomba kuteuliwa kuwania nafasi hiyo kwa chama chake ili kuwatumikia Watanzania.
“Imani yangu nitapata fursa zaidi ya kufafanua mawazo na sera zangu baada ya kuteuliwa rasmi na chama changu kuwa mgombea wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema.
Kalikawe amesema anaomba kuteuliwa kuwania nafasi hiyo akitambua mazingira ya kisiasa nchini hayatoi uwanja sawa kwa vyama kushindana.
“Chama changu kimejizatiti kushiriki ili kulinda thamani ya kura nami iwapo nitateuliwa kupeperusha bendera, nipo tayari kuongoza mapambano hayo,”amesema Kalikawe.