Ajira za walimu sasa mjadala kila kona

Dodoma. Mjadala unaoendelea sasa ni ajira kwa walimu. Ni mjadala wenye sura mbili.

Mosi ni wasiwasi uliopo kuhusu utaratibu mpya wa walimu hao kufanya usaili, tofauti na ilivyokuwa zamani, walipokuwa wakiitwa na kupangiwa vituo.

Pili, tangazo la ajira mpya za walimu lililotolewa Januari 2025, limekuja na kilio kingine cha kuwachanganya walimu waliomaliza kwa vipindi tofauti.

Hoja ya baadhi ya wadau ni kwamba huwezi kuwashindanisha walimu wanaosotea ajira tangu mwaka 2015 na wale waliomaliza mwaka 2023. Wanapendekeza waliomaliza zamani kupewa kipaumbele. 

Hizi ndizo hoja za  mjadala uloteka hisia za wadau wengi wa elimu mitandani na hata miongoni mwa wabunge, waliokutana jijjini Dodoma hivi karibuni.

Hata hivyo, Serikali kupitia taarifa yake iliyotolewa na Sekretarieti ya Ajira Februari 19,ilieleza kuwa lengo la utaratibu wa usaili, ni kupata nguvu kazi ya walimu wenye uwezo na weledi watakaochangia katika kuifikisha nchi yetu katika malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2050. 

“Tunawasihi wote wanaotafuta fursa za ajira katika utumishi wa umma wenye sifa stahiki wakiwemo walimu, kujiandaa vizuri kabla ya usaili, kujiamini na kushiriki katika usaili ili waweze kufaulu na kupangiwa vituo vya kazi kadiri nafasi za ajira zinapojitokeza,” ilisema Taarifa hiyo iliyotolewa na msemaji wake, Lynn Chawala.

Hali ilivyo kwa walimu wasio na ajira

Kwa muda sasa kumekuwa na vuguvugu kuhusu usaili wa ajira za ualimu kufanyika kwa kuzingatia miaka waliohitimu mafunzo,  ambapo wahitimu wa kada hiyo kutoka katika vyuo mbalimbali wa kati ya mwaka 2015-2023 waliamua kupaza sauti zao kupitia umoja wao  unaojulikana kwa jina Non Employed Teachers Organization ( NETO) 

Wahitimu hao  kupitia taarifa yao wanaelezea changamoto mbalimbali ambazo zimejitokeza kwenye mchakato wa usaili wa kada ya ualimu ulioanza Januari 14 hadi Februari 24 mwaka huu.

Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na upendeleo na vitendo vya rushwa kwenye vyumba vya usaili unaoendelea kwenye mikoa yote nchini pamoja na lugha zisizofaa kwa wanaosailiwa kutoka kwa wasimamizi wa usaili huo.

“Kukaa muda mrefu katika maeneo ya usaili mitihani imekuwa na dakika 40 lakini tunakaa kuanzia saa moja hadi saa nane. Haya ni matumizi mabaya ya rasilimali muda ukizingatia wanaowafanyia hivyo wana majukumu ya kifamilia huo muda wangeweza kuutumia kuzalisha,” anasema Taarifa na kuongeza:

“Kumekuwa na madhara makubwa kwa watoto, kinamama wajawazito na wenye udhaifu mbalimbali katika miili yao. Hii ni kutokana na kukaa muda mrefu bila kula wakisubiri kukamilisha zoezi la usaili.”

Pia wanalalamikia kutengwa kwa kituo kimoja ndani ya mkoa,  hali inayosababisha gharama za maisha kuwa kubwa kutokana na baadhi ya wasailiwa kutoka pembezoni mwa mji,  huku wakilazimika kujigharamia kwa muda wote wanaposubiri shughuli ya usaili hali inayoongeza gharama za maisha.

Wahitimu hao wanaitaka Serikali kurudisha uratatibu wa zamani wa kuwaajiri walimu pindi wanapomaliza vyuo vya ualimu,  ili kupunguza idadi kubwa ya walimu ambao wamezagaa mitaani bila ajira, huku elimu waliyoipata ikiwa  haiwawezeshi kujiajiri, wakitoa hoja kuwa  mafunzo waliyosomea ni ya kuitumikia Serikali na si kujiajiri.

Pia wanataka Serikali kusitisha mafunzo ya kada ya ualimu vyuoni,  hadi pale walimu wote waliohitimu watakapopata ajira.

Hata hivyo, akijibu changamoto za mchakato wa usaili, Chawala alisema 

ili kutekeleza dhana ya uwazi, usaili huo,  unasimamiwa kwa ushirikiano wa viongozi kutoka Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Wengine ni Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), taasisi nyingine za umma pamoja na ofisi za wakuu wa mikoa kote nchini. 

Watema nyongo mitandaoni

Baada ya majibu ya Serikali, kulikuwa na mjadala mpana katika mitandao ya jamii ambapo mtu aliyejitambulisha kwa jina la brigthon_the_totor,  alisema kuwaita walimu 28,000 kwenye usaili ili upate walimu 184, nalo linaweza kuwa ni moja ya maajabu makubwa kuwahi kutokea tangu nchi ipate uhuru.

“Unawaita watu hawa unawapa maswali ya kuchagua ili uwachuje wabaki 775 wa kwenda kwenye usaili wa mahojiano. Vuta picha ushindani huo utakuwaje mtu anapata alama 76 lakini kutokana na idadi iliyopo anaambiwa hajafaulu usaili,”aliandika.

Aliasema kingine kinachowauma zaidi ni kwamba hakuna vipaumbele yaani wahitimu wote wa kuanzia 2015 hadi mwaka 2023 wanashindanishwa bila kujali mwaka wa kumaliza wala umri wa mwombaji ajira.

“Kuna watu wamekaa mtaani karibu miaka 10 wakisubiri ajira lakini wanakuja kushindanishwa na mwalimu aliyehitimu mwaka mmoja nyuma, mimi nafikiri hii si sawa,”alisema.

Mwingine aliyejitambulisha kama Totty_Mwaisabala alisema amekata tamaa kabisa na hana pa kusemea, bali mbingu zinaona mateso anayoyapitia maana tangu mwaka 2015, yupo mtaani huku akiwa na vigezo vyote vya usaili.

“Bila Mungu yamkini ningechukua uamuzi mgumu sana halafu nimejitolea miaka na miaka, lakini bado sipati thamani kulitumikia Taifa langu inaniumiza sana,”anasema.

Kelvin2982  anaiomba Serikali kubadilisha uamuzi maana watu watazeeka na umri wa kuajiriwa utawatupa mkono, na kwamba utaratibu wa kuajiriwa kutokana na miaka ya kuhitimu ulikuwa ni mzuri sana.

“Ila sasa hivi ni maumivu mengi, hivi kweli maswali ya kuchagua ya dakika 40 yanampimaje mwalimu mahiri wakati vyeti vya kitaaluma wanavyo….”anasema.

Kilio bungeni 

Akichangia taarifa ya mwaka ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Februari 11, 2025, Mbunge wa Buyungu (CCM),  Aloyce Kamamba alisema usaili wa ajira kufanyika kwa kuwachanganya wahitimu wa miaka 10 iliyopita na waliomaliza mwaka jana hauko sawa.

Alisema Serikali iliwashawishi walimu wasomee ualimu na kuwapa mikopo ya elimu ya juu, lakini sasa wana miaka 10 wako nyumbani hawajaajiriwa, hivyo  Serikali ifanye kazi ya ziada kuwaajiri  walimu hasa waliohitimu siku nyingi.

“Wabunge walishauri kwa kuwa walimu wengi wako mtaani, ni vyema tuanze na walimu waliomaliza siku za nyuma,  wale wa awali ndio waanze kuajiriwa tunao walimu waliohitimu mwaka 2015, 2016, 2017,”alisema na kuongeza:

“Kwa nini wasianzwe hao? Na hii itatusaidia mheshimiwa mwenyekiti hata sisi itatusaidia kuwa na majibu sahihi kwa wananchi wetu. Muda mwingine  unaombwa tunaomba utusaidie kupata ajira.”

Akijibu  hoja ya Kamamba, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda alisema suala hilo lina maumivu yake makubwa na kuwa Serikali inaelewa umuhimu wa watu waliosomea ualimu kupata ajira.

“Tuna uchungu kwamba tungependa wapate ajira lakini tunaelewa umuhimu wa wanafunzi kupata walimu bora na tungependa wanafunzi wapate walimu  bora na sio bora tu walimu. 

“Mimi natoa wito kwa walimu, umekaa miaka 10 (mtaani) endelea kujiendeleza kwa sababu ukiitwa ukasailiwa utakuwa vizuri, ” alisema.

Aliongeza: “Natoa mfano, mwalimu wa Kiingereza tukikuta huwezi kuzungumza Kiingereza, hatuwezi kukuajiri kwa sababu umekaa miaka 10 mtaani. Itatuuma sana lakini itatuuma sana kumpelekea mwanafunzi mwalimu asiyeandaliwa vizuri.”

Alisema suala hilo ni la kisera kuwa walimu wataajiriwa kupitia mchujo huo na kuwa dhana hiyo haipo Tanzania tu bali ni utaratibu wa nchi mbalimbali zilizoendelea.

“Tunaweza kuwaajiri wote? Na hata walipokuwa darasani walikuwa wanafahamiana kuna aliyekuwa akishika nafasi ya kwanza kila siku na kuna aliyekuwa anashika nafasi ya mwisho na amefaulu na wanajua. Halafu wanakuja kuangalia aliyekuwa wa mwisho ameajiriwa,”alisema.

Profesa Mkenda alisema wanachoangalia ni maslahi ya wanafunzi wapate walimu bora na sio bora walimu na hivyo Serikali lazima ichukue uamuzi mgumu kwa maslahi ya Taifa.

Wadau wazungumza 

Mwalimu Bakari Mtembo anasema uelewa wa mtu aliyemaliza miaka mingi iliyopita, unakuwa ni tofauti na aliyemaliza miaka ya hivi karibuni kwa kuwa aliyehitimu zamani anakuwa amepitia mambo mengi, huku aliyemaliza mwaka jana akiwa na kumbukumbu kubwa ya aliyofundishwa.

“Kutunza kumbukumbu ya alichofundishwa miaka mitano ya nyuma ni kazi sana kuliko aliyemaliza mwaka jana. Kuwashindanisha hawa watu wawili kwa pamoja ni wazi huyu aliyemaliza hivi karibuni bado brain (akili) ya huyu aliyemaliza hivi karibuni itakuwa inafanya kazi zaidi ya yule wa miaka iliyopita,”anasema.

Hata hivyo, anasema waliomaliza miaka mingi iliyopita wana ujuzi mkubwa kwa sababu wengi wao wanajitolea kufundisha shuleni na hivyo kuwashindanisha makundi hayo mawili kwa pamoja. inawezekana Serikali isipate  kile inachokihitaji.

Anashauri Serikali kutengeneza utaratibu ambao hautalazimisha walimu kuwa na mitihani miwili ikiwemo kutumia vyeti vya kuhitimu mafunzo ya ualimu, kwa sababu mitihani wanayoifanya ya kuhitimu nayo imeandaliwa serikalini.

“Hawa wamefaulu,  sasa leo hii unapomweka katika usaili tena, unampima nini? Na kwanini hii kitu ipo kwa watu hawa wa chini. Mfano hawa waliomaliza urubani utamfanyia usaili tena? anahoji  Mtembo ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Walimu Tanzania (CWT).

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie anasema malalamiko hayo yanatoa ujumbe kuwa kuna changamoto kubwa ya ajira,  na inatoa picha walimu wamejaa mitaani pasipo ajira.

“Kulipokuwepo na uhaba wa walimu, Serikali ilikuja na mbinu mbalimbali ikiwemo kujenga vyuo mfano Mkwawa (Dar es Salaam). Na walidahiliwa wengi na walipokuwa wakimaliza walikuwa wakiajiriwa lakini tangu mwaka 2015 ndio hiyo changamoto,”anasema.

Dk Loisulie ambaye pia ni Mwenyekititi wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, (THTU), anasema msukumo wa Serikali wa kuzalisha walimu ubadilike ili kutozalisha changamoto nyingi kwa Taifa katika siku zijazo.

Anasisitiza kuwa usaili ubakie pale pale ili watu wapate ajira kwa kushindanishwa.

Kauli ya kusisitiza usaili inaungwa mkono na mzazi, Justina Andrew ambaye anasema kwa kufanya hivyo, itaiwezesha Serikali kupata walimu walio bora ambao wanaweza kufundisha wanafunzi watakaokuja kupambana sokoni na wenzao wa nchi nyingine.

“Lakini wapo wale ambao wanajitolea, tena katika mazingira magumu, Serikali iwaangalie hawa kwa kuwapa kipaumbele cha ajira kwa kuwa watakuwa wameshaona utendaji wao wa kazi wakati wanajitolea,”anasema.

Kama una maoni kuhusu habari hii tuandikie kupitia Whatsapp 0765864917.