Dar es Salaam. Wakati Ligi Kuu Bara ikiendelea kushika kasi nchini, kaa ni la moto kwa makocha msimu huu kwani licha ya kutomaliza msimu, ila tayari 13, kati ya timu 16, zinazoshiriki wametimuliwa, kutokana na kutokidhi mahitaji waliyopewa.
Mwananchi linakuletea makocha wote 13 walioondoka na kile walichokifanya, ikiwa ni watatu tu waliobakia wakiwemo, Ahmad Ally anayekiongoza kikosi cha maafande wa JKT Tanzania , Fadlu Davids (Simba) na Mecky Maxime wa timu ya Dodoma Jiji.

David Ouma
DAVID OUMA (COASTAL UNION)
Raia huyu wa Kenya ndiye alikuwa wa kwanza kutimuliwa Agosti 24, 2024, ikiwa ni muda mfupi tangu timu hiyo ipoteze mabao 3-0, dhidi ya kikosi cha Bravos do Maquis kutoka Angola, katika mchezo wa awali wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Ouma alijiunga na Coastal Union Novemba 9, 2023 akichukua nafasi ya aliyekuwa kocha mkuu wa kikosi hicho na Mkurugenzi wa Programu za vijana, Mwinyi Zahera aliyejiunga na Namungo huku akizifundisha timu za Sofapaka, Mathare United na Posta Rangers.
Uzoefu wake uliiwezesha Coastal kumaliza nafasi ya nne katika Ligi Kuu Bara msimu wa 2023-2024 na kufuzu michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza tangu mara ya mwisho iliposhiriki na kuishia raundi ya kwanza mwaka 1989.

Youssouph Dabo
YOUSSOUPH DABO (AZAM FC)
Septemba 3, 2024, uongozi wa Azam FC uliachana na aliyekuwa kocha mkuu wa kikosi hicho, Youssouph Dabo baada ya mwenendo mbaya wa matokeo ndani ya timu hiyo uliopelekea kutolewa katika hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2024-2025.
Dabo alitimuliwa baada ya kuiongoza timu hiyo katika mchezo mmoja tu wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2024-2025, dhidi ya Maafande wa JKT mechi iliyomalizika kwa suluhu.
Dabo alijiunga rasmi na Azam FC Mei 1, 2023, baada ya kuachana na Klabu ya ASC Jaraaf de Dakar ya kwao Senegal ambapo alitua ndani ya kikosi hicho kwa mkataba wa miaka mitatu akichukua nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Kocha Mkuu, Kally Ongala.
Septemba 7, 2024, uongozi wa Azam FC ulimtangaza aliyekuwa Kocha Mkuu wa RS Berkane, Rachid Taoussi raia wa Morocco kurithi mikoba ya Yousouph Dabo.

Fikiri Elias
FIKIRI ELIAS (KENGOLD)
Elias alianza msimu na kikosi hiki kilichopanda daraja msimu huu japo aliachana nacho Septemba 17, 2024, kwa makubaliano ya pande zote mbili baada ya mwenendo mbaya wa timu hiyo, tangu ilipopanda Ligi Kuu Bara kwa msimu huu wa 2024-2025.
Fikiri aliiongoza KenGold katika michezo mitatu ya Ligi Kuu Bara na kupoteza yote, akichapwa mabao 3-1, dhidi ya Singida Black Stars Agosti 18, 2024, akachapwa tena 2-1 na Fountain Gate Septemba 11, 2024, kisha kupoteza kwa bao 1-0, na KMC Septemba 16, 2024.
Baada ya hapo ikaongozwa na Jumanne Challe aliyeipandisha kama kocha wa muda kutokana na kutokidhi vigezo vya kusimamia benchi la ufundi ambapo katika michezo yake mitano ya Ligi Kuu Bara, alishinda mmoja tu, sare mmoja na kupoteza mitatu.
Oktoba 22, 2024, uongozi wa KenGold ulimtangaza, Omary Kapilima kuchukua nafasi ya Fikiri Elias kwa ajili ya kumalizia msimu mzima.
Hata hivyo, Januari 18, 2025, uongozi wa timu hiyo ulimtangaza Kocha Mkuu, Mserbia Vladislav Heric kuifundisha ingawa bado haonekani kwenye benchi.

Paul Nkata
PAUL NKATA (KAGERA SUGAR)
Oktoba 10, 2024, Klabu ya Kagera Sugar iliachana na aliyekuwa kocha mkuu wa kikosi hicho, Mganda Paul Nkata baada ya mwenendo mbaya ndani ya timu hiyo katika michezo mbalimbali ya Ligi Kuu Bara aliyoiongoza tangu msimu huu umeanza pia.
Nkata aliyewahi kuzifundisha timu mbalimbali zikiwemo, SC Villa na Express FC za kwao Uganda, alijiunga na Kagera Sugar Agosti 10, 2024, akichukua nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa kocha mkuu wa kikosi hicho, Fredy Felix ‘Minziro’.
Tangu Nkata achukue mikoba ya ‘Minziro’, aliiongoza Kagera Sugar katika jumla ya michezo saba ya Ligi Kuu Bara kwa msimu huu wa 2024-2025, ambapo kati yake alishinda mmoja, sare mmoja na kupoteza mitano akiiacha nafasi ya 14 na pointi nne.
Baada ya hapo Oktoba 17, 2024, uongozi wa Kagera ukamtangaza aliyekuwa kocha wa Coastal Union, Gwambina na Dodoma Jiji, Melis Medo, baada ya kuonyesha kiwango kizuri akiwa na kikosi cha Mtibwa Sugar kinachoshiriki Ligi Kuu ya Championship.
Februari 25, 2025, uongozi wa Kagera Sugar ulitangaza kuachana na Medo baada ya kutoridhishwa na mwenendo wa timu hiyo tangu ajiunge nayo, huku akiiongoza katika michezo 14, ya Ligi Kuu Bara, akishinda miwili, sare mitano na kupoteza saba sasa timu ipo chini ya Juma Kaseja.

GORAN KOPUNOVIC (PAMBA FC)
Raia huyo wa Serbia aliachana na Pamba Jiji Oktoba 16, 2024 baada ya kuiongoza timu hiyo katika michezo saba ya Ligi Kuu Bara, akitoka sare minne na kupoteza mitatu, jambo lililowapa mashaka mabosi wa kikosi hicho na kufanya uamuzi huo.
Goran alijiunga na timu hiyo msimu wa 2023-2024, baada ya kuachana na Tabora United ambapo alikiacha kikosi hicho nafasi ya 16, katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, kufuatia kukusanya jumla ya pointi zake nne katika michezo saba aliyokiongoza.
Hata hivyo, baada ya kuachana naye uongozi ulimtangaza Fredy Felix ‘Minziro’ anayeendelea kuifundisha hadi sasa.

FRANCIS KIMANZI (TABORA UNITED)
Oktoba 21, 2024, uongozi wa Tabora United ulitangaza kuachana na aliyekuwa kocha mkuu wa kikosi hicho Mkenya, Francis Kimanzi na msaidizi wake, Yusuf Chippo, baada ya mwenendo mbaya wa timu hiyo katika michezo ya Ligi Kuu Bara msimu huu.
Makocha hao wa Kenya, walijiunga na Tabora Julai 31, 2024, na kuiongoza katika jumla ya michezo minane ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2024-2025, ambapo kati yake walishinda miwili, sare miwili na kupoteza minne wakiiacha nafasi ya 11, na pointi nane.
Hata hivyo, Novemba 2, 2024, uongozi wa timu hiyo ulimtangaza, Mkongomani Anicet Kiazayidi kuchukua nafasi ya Kimanzi.

MWINYI ZAHERA (NAMUNGO FC)
Zahera ambaye kwa sasa ni mshauri wa benchi la ufundi la timu hiyo, kabla ya majukumu hayo alikuwa kocha mkuu, ingawa Oktoba 24, 2024 aliachana na Namungo na nafasi yake kuchukuliwa na Juma Mgunda.
Kabla ya uteuzi wa Mgunda, Zahera alikiongoza kikosi hicho katika jumla ya michezo saba ya Ligi Kuu Bara ambapo kati ya hiyo alishinda miwili tu huku akipoteza mitano, akikiacha nafasi ya 13, kwenye msimamo baada ya kukusanya pointi sita.

ABDIHAMID MOALLIN (KMC FC)
Novemba 11, 2024, uongozi wa KMC FC ulitangaza rasmi aliyekuwa kocha wa kikosi hicho, Abdihamid Moallin kujiuzulu katika nafasi hiyo, kwa makubaliano ya pande mbili baada ya kuiongoza msimu huu kwenye jumla ya michezo 11, ya Ligi Kuu Bara.
Kocha huyo, aliiongoza KMC katika michezo 11, ambapo kati ya hiyo alishinda minne, sare miwili na kupoteza mitano akiiacha nafasi ya saba na pointi 14.
Baada ya hatua hiyo, Novemba 14, 2024, KMC FC ikamtangaza aliyekuwa kocha wa muda wa Azam FC, Kally Ongala

MIGUEL GAMONDI (YANGA)
Novemba 15, 2024, uongozi wa Yanga uliachana na aliyekuwa kocha mkuu wa kikosi hicho, Miguel Gamondi baada ya kuiongoza timu hiyo msimu wa 2024-2025, katika michezo 10 ya Ligi Kuu Bara, ambapo kati yake alishinda minane na kupoteza miwili.
Hatua ya Gamondi kufukuzwa ilijiri baada ya timu hiyo kupoteza michezo miwili mfululizo ikianza na (1-0) v Azam FC na (3-1) v Tabora United na katika michezo 10, Yanga ilikuwa ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara na pointi zake 24.
Gamondi alijiunga na Yanga Juni 24, 2023 akichukua nafasi ya Mtunisia, Nasreddine Nabi.
Tangu ateuliwe kukiongoza kikosi hicho, Gamondi alikiongoza katika jumla ya michezo 40 ya Ligi Kuu Bara kuanzia msimu wa 2023-2024, hadi huu wa sasa wa 2024-2025, ambapo kiujumla kati ya hiyo alishinda 34, sare miwili tu na kupoteza minne.
Baada ya kuondoka Gamondi, Novemba 15, 2024, uongozi wa Yanga ulimtangaza aliyekuwa Kocha Mkuu wa TS Galaxy ya Afrika Kusini, Sead Ramovic raia wa Ujerumani aliyejiuzulu mwenyewe ndani ya timu hiyo kutokana na mwenendo mbaya wa matokeo.
Februari 4, 2025, uongozi wa Yanga ulitangaza kuachana na Ramovic kwa makubaliano ya pande zote mbili baada ya kuiongoza katika michezo 13, ambapo kati yake sita ni ya Ligi Kuu Bara, sita ya Ligi ya Mabingwa Afrika na mmoja wa Kombe la FA.
Katika michezo sita ya Ligi Kuu Bara, Ramovic alishinda yote na kufunga jumla ya mabao 22 na kuruhusu mawili tu, wakati kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika alishinda miwili, sare miwili na kupoteza miwili.
Katika Kombe la FA, Ramovic aliiongoza Yanga kwenye mchezo mmoja tu ambao ulikuwa ni wa hatua ya 64 bora na kushinda mabao 5-0 dhidi ya Copco FC kutoka jijini Mwanza.
Kiujumla, Ramovic aliiongoza Yanga katika jumla ya michezo 13, akishinda tisa, sare miwili na kupoteza miwili.
Baada ya hapo, Yanga ikamtangaza aliyekuwa Kocha wa Singida Black Stars, Miloud Hamdi mwenye uraia pacha wa Algeria na Ufaransa.

PATRICK AUSSEMS (SINGIDA BS)
Raia huyo wa Ubelgiji aliyetamba na timu mbalimbali zikiwemo Simba, aliachana na Singida Novemba 25, 2024 na msaidizi wake, Denis Kitambi kwa kile kilichoelezwa kufikia makubaliano ya pande zote mbili.
Hadi Aussems anaondoka alikuwa ameiongoza Singida katika jumla ya michezo 11, ya Ligi Kuu Bara na kati ya hiyo alishinda saba, sare mitatu na kupoteza mmoja tu, ambapo alikiacha kikosi hicho nafasi ya nne kwenye msimamo na pointi zake 24.
Baada ya hapo, uongozi wa timu hiyo ukamtangaza mkurugenzi wa ufundi wa kikosi hicho, Ramadhan Nswanzurimo kukiongoza kwa kushirikiana na Muhibu Kanu.
Nswanzurimo aliiongoza katika michezo mitano ya Ligi Kuu Bara ambapo alishinda mitatu.
Desemba 30, 2024, uongozi wa Singida Black Stars ulimtangaza rasmi Kocha, Miloud Hamdi. .
Hata hivyo, kocha huyo hajaiongoza timu hiyo katika mchezo wowote wa Ligi Kuu Bara baada ya kuondoka kisha kujiunga na Yanga Februari 4, 2025, sasa timu ipo chini ya David Ouma.

MBWANA MAKATA (TZ PRISONS)
Kikosi hiki cha Maafande kiliachana na aliyekuwa Kocha Mkuu, Mbwana Makata na msaidizi wake, Renatus Shija Desemba 28, 2024, baada ya kutoridhishwa na mwenendo wa matokeo.
Makata alikiongoza kikosi hicho katika jumla ya michezo 14 ya Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2024-2025, ambapo kati ya hiyo alishinda miwili tu, sare mitano na kupoteza saba, ambapo alikiacha kikiwa nafasi ya 15, kwenye msimamo na pointi 11.
Baada ya kuondoka Makata, timu hiyo ikakabidhiwa kwa Kocha Msaidizi, Shaban Mtupa aliyesimamia katika michezo miwili ya Ligi Kuu akianza na kichapo cha mabao 4-0, dhidi ya Yanga Desemba 22, kisha ushindi wa bao 1-0 na Pamba Jiji Desemba 26, 2024.

MOHAMED MUYA (FOUNTAIN GATE)
Muya ndiye kocha wa mwisho aliyeuaga mwaka 2024 vibaya baada ya kutimuliwa Desemba 29, 2024, ikiwa ni muda mfupi tangu kikosi hicho kikumbane na kichapo cha fedheha cha kucharazwa mabao 5-0, dhidi ya Yanga .
Hadi Muya anaondoka ndani ya kikosi hicho alikuwa amekiongoza katika jumla ya michezo 16, ya Ligi Kuu Bara ambapo kati yake alishinda sita, sare miwili na kupoteza minane, akikiacha kikiwa kwenye nafasi ya sita.
Januari 10, 2025, uongozi wa Fountain Gate ulimtangaza aliyekuwa Kocha Mkuu wa Sofapaka ya Kenya, Robert Matano.

ABDALLAH MOHAMED ‘BARESI’ (MASHUJAA FC)
‘Baresi’ ndiye kocha wa mwisho hadi sasa kutimuliwa ikiwa ni muda mfupi tu tangu kikosi hicho cha ‘Mapigo na Mwendo’ kuchapwa mabao 3-0, dhidi ya Singida Black Stars.
Kwa msimu wa 2024-2025, ‘Baresi’ aliiongoza Mashujaa katika jumla ya michezo 22, ambapo kati ya hiyo alishinda mitano tu, sare minane na kupoteza tisa, akifunga mabao 17 na kuruhusu 26, akiiacha ikishika nafasi ya 11 na pointi zake 23.
Kauli ya Bares
Akizungumza baada ya kutimuliwa kwake kikosini, ‘Baresi’ alisema ameridhia kuachana na timu hiyo kutokana na mwenendo mbaya.
“Matokeo mabaya tuliyopata ni sehemu ya mchezo, nafikiri ni upepo mbaya uliotupitia, sina shaka na wachezaji waliopo na naamini wataipambania Mashujaa isishuke daraja,” alisema Baresi aliyeifundisha timu hiyo kwa misimu miwili mfululizo na ndiye kocha pekee aliyekuwa amebaki ambaye alitoka na timu msimu uliopita.