Ilipopata ithibati ya kimataifa kama Mwajiri Bora wa Mwaka 2025 nchini kutoka kwa mamlaka ya rasilimali watu ya kimataifa, Top Employers Institute, mwanzoni mwa mwaka huu, Benki ya NMB si tu iliimarisha rekodi yake ya mafanikio ya kipekee, bali pia imeweka viwango vipya vya ajira na mazingira bora ya kazi kupitia mikakati endelevu ya ustawi wa wafanyakazi.
Hatua hii muhimu katika safari ya takriban miaka 30 ya mageuzi yenye tija ni uthibitisho wa dhamira endelevu ya NMB kuwa mahali bora pa kazi na mwajiri pendwa sokoni
Kwa mujibu wa Mkuu wa Idara ya Rasilimali Watu – Huduma Shirikishi, Bw. Joseph Ngalawa, wafanyakazi wenye furaha, afya bora, na ari ya kufanya kazi kwa bidii ni nguzo muhimu ya ufanisi wao binafsi, na mafanikio ya mwajiri wao kwa ujumla.

“Katika dunia ya sasa yenye ushindani mkubwa wa vipaji na rasilimali watu, uwekezaji katika maendeleo ya wafanyakazi, kuboresha mazingira ya ajira, na kuvutia vipaji bora ni msingi mkubwa wa mafanikio endelevu kwa taasisi yoyote inayozingatia mifumo ya kisasa ya ajira,” Bw Ngalawa alieleza katika mahojiano maalumu Jumamosi iliyopita uko Moshi, Kilimanjaro.
Mwajiri Kinara Kileleni Mlima Kilimanjaro
Mahojiano hayo yalifanyika baada ya hafla ya kuwapokea wafanyakazi wa Benki ya NMB waliopandisha Tuzo ya Mwajiri Bora Tanzania kwa mwaka 2025 kileleni mwa Mlima Kilimanjaro kuthibitisha na kuionesha Afrika nzima kuwa NMB ni kinara wa ajira na maendeleo ya wafanyakazi kwa ujumla.
Ngalawa alisisitiza kuwa kupitia programu zake za kisasa za ajira, Benki ya NMB imeonesha kwa vitendo kuwa mazingira bora ya kazi yanachochea hamasa, kuongeza tija, na kuwafanya wafanyakazi kujihisi kuwa sehemu ya taasisi kwa kushirikishwa katika maamuzi na mikakati yake ya maendeleo.
Aliongeza kuwa mafanikio makubwa ya NMB katika usimamizi wa rasilimali watu na uwekezaji wake katika maendeleo ya wafanyakazi ndiyo yameiwezesha kuorodheshwa miongoni mwa mashirika 2,400 bora duniani yanayotambuliwa kwa kukuza ajira na kulea vipaji.
“Leo tumekusanyika hapa si tu kusherehekea mafanikio haya makubwa ya wenzetu waliopanda Mlima Kilimanjaro, bali pia kuwapongeza kwa kujitoa na kujituma kwao katika kutekeleza dhamira yetu kama Benki ya NMB,” alisema Bw Ngalawa katika hafla iliyofanyika kwenye Lango la Mweka, moja ya njia kuu za kupanda na kushuka Mlima Kilimanjaro.
Ustawi wa Wafanyakazi ni zaidi ya Afya ya Kimwili
Kiongozi huyo alisisitiza kuwa kupanda Mlima Kilimanjaro kunahitaji ustahimilivu, mshikamano, na dhamira thabiti – sifa ambazo pia ni msingi wa utendaji wa kila siku wa NMB.

Hafla ya kuwapokea mashujaa waliopanda Mlima Kilimanjaro ilihudhuriwa na zaidi ya wafanyakazi 100, ambao mwaka huu walidhaminiwa kushiriki Kili Marathon, mbio ambazo zimekuwa ni sehemu ya juhudi za NMB kuimarisha ustawi wa wafanyakazi wake kimwili, kiafya, na kukuza mshikamano ndani ya taasisi.
Bw Ngalawa alieleza kuwa mpango wa ustawi wa wafanyakazi wa Benki ya NMB unakwenda mbali zaidi ya ustawi wa kawaida, ukilenga kuwapa wafanyakazi motisha, ari ya kufanya kazi, na mazingira bora ya maendeleo yao binafsi na mwajiri wao kwa ujumla
Mfano halisi wa juhudi hizi ni Siku ya Ustawi wa Wafanyakazi ya NMB, iliyoanzishwa wakati wa mashindano ya kwanza ya NMB Interzonal Competition mwezi Desemba mwaka jana jijini Mwanza.
Tamasha hilo si tu lilihimiza afya ya mwili na mshikamano wa kitimu, bali pia lilitoa fursa ya kuhamasisha mambo mbalimbali ya kafya ikiwemo pia ile ya akili, ushauri wa maendeleo binafsi, na elimu ya fedha, kuhakikisha ustawi wa wafanyakazi unazingatiwa kwa upana wake.
Sherehe za Mwajiri Bora Madrid, Hispania
Nne siku kabla ya kuanza safari ya kupandisha nishani ya ithibati ya Mwajiri Bora kwenye Mlima Kilimanjaro mnamo Februari 13, Mkuu wa Rasilimali Watu wa Benki ya NMB, Bw Emmanuel Akonaay, aliwakilisha benki hiyo kwenye sherehe za Top Employers Institute huko Madrid, Hispania, ambapo waajiri bora wa mwaka huu walitunukiwa.

Afisa Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo, Bw David Plink, alivutiwa na mchakato huo baada ya kuelezwa na Bw Akonaay kuhusu utekelezaji wake.
Bw Akonaay alifafanua kuwa safari hiyo ililenga kuonesha ubora wa NMB katika usimamizi wa rasilimali watu, huku ikiwahamasisha waajiri wengine kuwekeza katika mazingira bora ya kazi na maendeleo ya wafanyakazi wao kwa ujumla, kwani kufanya hivyo kunalipa.
Faida na manufaa ya kuwekeza katika ustawi wa wafanyakazi na kuboresha mazingira ya ajira ni nyingi, zikiwemo:
- Kukuza Ufanisi
- Wafanyakazi wenye afya bora na ari ya kufanya kazi huongeza tija na utendaji, hivyo kuimarisha matokeo chanya ya kibiashara.
- Kupunguza Gharama za Uendeshaji
- Mazingira mazuri ya kazi hupunguza kiwango cha mabadiliko ya wafanyakazi, na gharama za kiafya, hivyo kupunguza gharama zisizo za lazima.
- Kuimarisha Sifa na Ushawishi wa Chapa
- Waajiri wanaojali ustawi wa wafanyakazi huvutia vipaji bora, uongeza imani ya wateja, na uboresha uhusiano na wadau mbalimbali.
- Kuchochea Ubunifu na Uvumbuzi
- Mazingira rafiki yanayohamasisha wafanyakazi huchochea ubunifu na kuongeza ushindani wa taasisi husika sokoni.
Kadri Benki ya NMB inavyoendelea kukua na kuimarika kama kinara wa kila kitu katika tasnia ya fedha nchini, jitihada zake za kuboresha ajira na mazingira ya kazi zinaiweka katika nafasi nzuri ya kutekeleza mkakati wake wa biashara kwa mafanikio.
Kwa mujibu wa Afisa Mtendaji Mkuu, Bi Ruth Zaipuna, ustawi wa wafanyakazi ni sehemu muhimu ya mkakati huo, na benki itaendelea kuwekeza rasilimali za kutosha katika maendeleo yao kwa ajili ya ustawi endelevu na mafanikio ya pamoja.