
Shinyanga. Mkazi wa kata ya Ndembezi iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Athuman Idd (35) amekutwa amejinyonga katika kata ya Kolandoto, siku moja baada ya kuachiwa kutoka Polisi.
Hayo yameelezwa leo Aprili 02, 2025 na Mwenyekiti wa Mtaa wa Ndembezi, Mariam Mdoe akibainisha kuwa tukio hilo limetokea baada ya marehemu kutoka Polisi,
“Mke wa marehemu alifika ofisini kwangu akiomba barua ya dhamana kwa ajili ya mumewe aliyekuwa Polisi baada ya kuandika barua hiyo, mwanamke huyo alienda kumdhamini mumewe hata hivyo siku iliyofuata alinitafuta kwa simu na kunijulisha kuwa mumewe amekutwa amejinyonga” amesema Mariam.
Kaka wa marehemu, Masawe Jackson ameeleza kuwa marehemu Athuman Idd alikamatwa na polisi kwa kosa la kuendesha pikipiki akiwa amelewa na bila kuvaa kofia ngumu,
“Mimi ni kaka wa marehemu, mdogo wangu alikamatwa kwa kosa la kuendesha pikipiki akiwa amelewa na akiwa hajavaa kofia ngumu” amesema Jackson.
Mwananchi imemtafuta Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga, Kennedy Mgani ambaye amesema kuwa kutokana na kuwa katika majukumu mengine ya kikazi taarifa hiyo bado haijamfikia,
“Niko katika majukumu mengine ya kikazi na mkuu wa mkoa taarifa hiyo sina uhakika kama imefika ofisini kwangu” amesema Mgani.