Ajinyonga baada ya kupata sifuri matokeo kidato cha nne

Geita. Rabia Paul (19), Mkazi wa Mtaa wa Msalala, Kata ya Kalangalala mjini Geita anadaiwa kujiua kwa kujinyonga baada ya kupata msongo wa mawazo kutokana na matokeo mabaya aliyoyapata katika mtihani wa taifa wa kidato cha nne.

Rabia aliyekuwa miongoni mwa wanafunzi 340 waliohitimu kidato cha nne mwaka 2024 katika Shule ya Sekondari Nyanza iliyopo Manispaa ya Geita alipata sifuri katika mtihani huo na tangu apokee matokeo hayo alikuwa mtu wa kujitenga na kukaa peke yake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita Safia Jongo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema limetokea jana Jumanne Februari 11, 2025 saa 10 alasiri ambapo alijinyonga kwa kutumia mtandio akiwa chumbani kwake.

Kamanda amesema chanzo cha kifo hicho ni binti kupata sifuri na alichukua uamuzi huo baada ya kusikia mama yake akimwelekeza mdogo wake aende akaangalie matokeo ya dada yake na aliposikia hivyo alijifungia chumbani wakijua amepumzika.

Salma Juma mama wa marehemu (mwenye kitenge chekundu) akifarijiwa na kina mama wenzake baada ya mwanae kujinyonga kwa kutumia mtandio.

“Lakini badaye waligundua amejinyonga na inaonekana marehemu alikua tayari amejua alipata sifuri kwenye matokeo ya kidato cha nne, nawaomba sana wazazi wakae karibu na watoto wajue furaha na huzuni zao,” amesema.

“Kunauwezekano mkubwa mama alimuona binti yake hayuko sawa lakini angemuweka karibu angejua changamoto aliyonayo maana kufeni masomo siyo kufeli maisha, maisha yapo angeweza kufanya kazi nyingine na akawa na maisha mazuri,” amesema Kamanda.

Ali Bakari, mjomba wa marehemu amesema alipata taarifa ya tukio na alipofika alikuta amejinyonga na walimuwahisha hospitali na walipomfikisha alikuwa tayari amepoteza maisha.

“Sisi tunahisi taarifa ya matokeo kuwa amefeli ndio imempa mawazo hadi kuamua kuchukua uamuzi huo maana ni binti aliyekuwa na bidii na anajituma kwenye masomo yake na ndio maana hakukubalina na matokeo akaamua kuchukua hatua aliyochukua,” amesema Bakari

“Baada ya kuambiwa matokeo alikuwa anakaa mwenyewe tulimpa moyo na kumwambia haya ni maisha lakini moyo haukukubali na ndio amefikia maamuzi haya aliyochukua,” amesema.

Doto Musa akimzungumzia binti huyo amesema ni binti mtulivu aliyekuwa akiishi na bibi yake kwa upendo na ni mtu mwenye huruma asiyekuwa kwenye makundi mabaya na kwamba uamuzi aliouchukua umewaacha mdomo wazi.

“Watoto wajifunze kutokana na hili wasichukue maamuzi bila kushirikisha mtu waangalie mwenendo wao maana wanawatia uchungu sana wazazi,” amesema Musa.

Mariam Shaban, mmoja wa wanafunzi waliokuwa wakisoma na marehemu amesema alikuwa mchangamfu anayependa kucheka na kuchekesha na kwamba taarifa za yeye kujinyonga zimewasikitisha.