Ajali ziara ya CCM Mbeya, miili kuagwa kesho

Mbeya. Wakati miili ya marehemu waliofariki kwa ajali jana kwenye ziara ya chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Mbeya, majeruhi wazungumzia maendeleo ya afya zao.

Jana Jumanne Februari 25, 2025 watu watatu walifariki papo hapo baada ya gari la serikali walilokuwa wakisafiria kugongana uso kwa uso na basi la Kampuni ya CRN katika eneo la Shamwengo wilayani Mbeya.

Waliofariki papo hapo ni pamoja na mwandishi wa kujitegemea, Furaha Simchimba, mjumbe wa kamati ya utekelezaji ya CCM Wilaya ya Rungwe, Daniel Mselewa na utingo wa basi, Isaya Geazi.

Hata hivyo, idadi ya vifo imeongezeka leo na kufikia wanne baada ya aliyekuwa majeruhi, Dereva wa Mkoa wa Mbeya, Thadei Focus, kufariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya.

Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Mbeya, Christopher Uhagile amesema ibada ya kuaga miili hiyo itafanyika kesho, Alhamisi, na kusimamiwa na chama hicho kwa kushirikiana na Serikali ya mkoa na watahakikisha taratibu zote zikiwamo za mazishi, zinasimamiwa ipasavyo.

Amesema viongozi mbalimbali wa chama ngazi ya Taifa, akiwamo Naibu Katibu Mkuu Bara na mlezi wa mkoa huo, John Mongela, Spika wa Bunge na Mbunge wa Mbeya Mjini, Dk Tulia Ackson, pamoja na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Fadhil Rajabu, watashiriki kwenye mazishi hayo.

Aidha, Uhagile amekanusha taarifa za kifo cha Katibu wa UWT Mkoa wa Mbeya, Lucia Suleakisema si za kweli.

Amesema majeruhi wanne, wakiwamo waandishi wa habari watatu na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa, James Mwampondele, wanaendelea kupata matibabu.

Kuhusu hoja ya gari la serikali kutumika katika ziara ya CCM, Uhagile amefafanua kuwa magari hayo yalihusika kutokana na ziara hiyo kujumuisha ukaguzi wa miradi ya serikali, hivyo baadhi ya magari yalitumika kusafirisha wataalamu waliokuwa sehemu ya ziara hiyo.

Majeruhi wazungumza

Mwandishi wa Chanel Ten, Epimacus Apolnali amesema anaendelea kupata nafuu, ingawa bado anahisi maumivu katika mguu wa kulia, shingo na kifua.

Ameeleza kuwa ajali hiyo ilitokea wakati wakielekea Mbeya, huku basi la CRN likiwa njiani kuelekea Mbarali, na kugongana uso kwa uso. Alijitambua akiwa hospitalini.

“Siyo kama jana, kwa sasa nashukuru Mungu afya inaimarika, ingawa bado naumwa sana mguu, shingo na kifua,” amesema Apolnali.

Naye mwandishi wa Dream FM, Seleman Ndelage amesema hali yake inaendelea kuimarika, huku akieleza kuwa anahisi maumivu mkononi na mgongoni.

“Hali yangu siyo mbaya sana, nimeanza kujitambua, ingawa bado naumwa mkono na mgongoni. Lakini nina matumaini hali itaendelea kuwa nzuri,” amesema Ndelage.

Kwa upande wake, mwandishi wa kujitegemea Denis George amesema; “Najitambua na hali yangu si mbaya sana. Maumivu bado yapo, hasa mkononi, mgongoni na sehemu za kichwani, lakini nina matumaini ya kupona,” amesema George.