Ajali zaua 14 ndani ya siku nne Kilimanjaro, chanzo chatajwa

Mwanga. Wakati watu 14 wakifariki dunia huku wengine 117 wakijeruhiwa kwa ajali  ndani ya siku nne, mkoani Kilimanjaro, mashuhuda wa ajali hizo wamesema wembamba wa barabara katika maeneo ya milimani umekuwa ni changamoto na imekuwa ikichangia kutokea kwa matukio  ajali za mara kwa mara  hasa katika Wilaya za Same na Mwanga.

Ndani ya kipindi cha siku nne, Mkoa wa Kilimanjaro kwenye wilaya za Same na Mwanga zimetokea ajali tatu tofauti na kusababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali.

Tukio la kwanza lilitokea Machi 30, 2025, wilayani Same ikihusisha ajali mbili tofauti ambapo watu saba walifariki dunia wakiwemo wanakwaya sita wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Chome,  waliopata  ajali  katika barabara ya Bangalala wakitokea Chome kwenda Vudee na wengine 23 kujeruhiwa.

Ajali ya pili iliyotokea siku hiyohiyo, kwenye eneo la Njoro wilayani humo na kusababisha kifo cha mtu mmoja baada ya basi la kampuni ya Osaka kupata ajali na kusababisha watu wengine 52 kujeruhiwa.

Ajali ya tatu imetokea jana katika eneo la Kikweni wilayani Mwanga na kusababisha vifo vya watu saba na wengine 42 kujeruhiwa, baada ya basi kampuni ya Mvungi walilokuwa wakisafiria kupinduka wakati likipishana na magari mengine kwenye kona.

Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, amesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva kushindwa kulimudu gari wakati alipokuwa akipishana na gari jingine kwenye kona kali, na hivyo kuacha barabara na kutumbukia bondeni.

Kamanda Maigwa ameeleza kuwa wanamshikilia dereva wa basi hilo kwa mahojiano zaidi.

“Watu saba wamefariki dunia na wengine 42 wamejeruhiwa baada ya basi mali ya Kampuni ya Mvungi lililokuwa linatokea Ugweno kwenda jijini Dar es Salaam eneo la Kijiji cha Mamba Msangeni, kupinduka kwenye bonde na kusababisha vifo vya watu hao saba, wakiwemo wanawake watano, mtoto wa miaka miwili  na wanaume wawili,” amesema Kamanda Maigwa

Amewataja waliofariki dunia kuwa ni Ashura Omari Sakena (47) mkazi wa Vuchama, Zaituni Hashimu Mwanga (52) mkazi wa Masumbeni, Halima Omari ambaye ni mtoto wa miaka miwili na Judithi Safieli Mwanga (43) mkazi wa Mangio.

Wengine ni Haji Abubakari (50) mkazi wa Kifula, Hamadi Hussein Mshana (64) mkazi wa Ngalanga Ugweno na Benadetha (20) ambaye ni mfanyakazi wa ndani aliyetajwa kwa jina moja.

Amesema majeruhi wote wanaendelea na matibabu katika hospitali za Kifula, Hospitali ya Wilaya ya Mwanga, KCMC na Hospitali ya Mkoa ya Mawenzi huku miili ya marehemu ikihifadhiwa hospitali ya Wilaya ya Mwanga kusubiri uchunguzi na taratibu nyingine.

Akizungumzia ajali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema kulikuwa na magari mengine mlimani huku moja likiwa limeharibika na katika kupishana ikatokea ajali hiyo.

“Kule ni milimani, barabara yetu ni ya lami lakini kulikuwa na magari mengine ambayo yalikuwa yamesimama, moja limebeba mwili linapandisha juu mlimani, lakini wakati anajaribu kulipita hilo gari ambalo lilikuwa limeharibika, wakati anapita kuna gari lingine mbele lilikuwa linakuja, akaona wapishane na yule mwenye gari ndogo,  gari lile likaingia pembeni ya barabara kutokana na kuwapo kwa matope yanayotokana na mvua zinzzoendelea kunyesha likateleza na kupinduka,”amesema RC Babu

Andrea Msuya,  mkazi wa Msangeni, Wilaya ya Mwanga amesema chanzo cha ajali katika eneo hilo ni kutokana na kwamba  barabara  ni nyembamba na kona ni  kali katika eneo hilo, hivyo akasema barabara hiyo imekuwa ni changamoto kwa watumia wa vyombo vya usafiri.

“Tumesikitika na ajali kama hii kutokea Ugweno nadhani miundombinu ya barabara inaweza kuchangia, kwani katika eneo hili kuna kona kali halafu barabara ni nyembamba na kuna bonde na mwaka jana tumempoteza kijana wa bodaboda hapa na leo imetoke ajali hii mbaya sana,”amesema Msuya

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *