
Nitatumia msingi wa tabia za binadamu kuelezea aina kuu nne za watu duniani, nitakuongoza walau ujifahamu na kuwafahamu wanaokuzunguka.
Naam, falsafa ya maendeleo ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere inasema ili nchi iendelee inahitaji ardhi, watu, siasa safi na uongozi bora. Leo napenda kuzungumzia watu.
Hivi karibuni nimesoma kitabu ‘Good to Great’ kilichoandikwa na Jim Collins, watu makini katika taasisi, kampuni au familia ndio watakao maendeleo ya kudumu, nami sina shaka nakubaliana naye.
Swali linabaki je, kuna watu wa aina ngapi duniani. Je, unatumia muda na watu wa aina gani, naamua kutumia muda wangu kuchimbua na kuchimba na kisha kubaini kuwa wako watu wa aina zifuatazo, ambao wameijaza dunia.
Tangu zamani na hata sasa dunia yetu yenye watu karibu bilioni 8 wako wa aina zifuatazo, nazitaja:
Wagiriki walitaja aina nne ambazo ni sanguine (damu), melancholy (nyongo nyeusi) choleric (nyongo ya njano) na Phlegmatic (uteute), hawa walitumia aina za majimaji ya mwili wa binadamu na kusema tabia zao, nitazifafanua hivi punde;
Historia inataja makundi mengine manne, moto (fire), dunia (earth), hewa (air) na maji (water). Waligawa tabia za watu kwenye makundi hayo.
Uko mgawanyo mwingine kwa jina unaitwa DISC, uliotajwa na mwanasaikolojia aitwaye William Martson, D inasimama Disicive/Dorminant (watu wenye maamuzi thabiti), I inasimama kama inspirational (watu wenye hamasa), S inasimama kama Stable/steady (watu wenye msimamo) na C inasimama kama Compliance (watu wa kufuata utaratibu).
Naam, na sasa kwa mujibu wa Thomas Ericson, anawagawa watu kwa rangi kuu nne; nyekundu, njano, kijani na bluu. Sasa ngoja niunganishe hizi nadharia nne ili tuwe na makundi manne ya watu, kwa kuzingatia tabia zao.
Choleric, red, fire, dominant hili ni kundi la watu makini, watu wanaozingatia matokeo, hawa wanaona mbali (visionary), hawana lelemama, ni hapa kazi tu. Hawa hawajali utanionaje, kazi kwanza mengine baadaye. Hawapotezi muda na ni wakali kupindukia wanapoona uzembe wa aina yeyote ile, ni wale wanaosema punda afe mzigo ufike, hawapendi blah blah.
2. Sanguine, yellow, air inspirational, hili kundi la pili duniani la watu wenye ushawishi, hawa wamejawa hamasa na ni wale wanaosema hakuna mkate mgumu mbele ya chai, hawaogopi ugumu wanaitenda kwa furaha, wanaongea sana. Hawa wakisimama kueleza jambo lazima wachombeze utani, wanafurahia kila hatua.
3. Phlegmatic, green, earth, stable, hili ni kundi la watu wenye msimamo, watu imara, hawayumbishwi hovyo, wanazingatia makubaliano na wanatekeleza yaliyokubalika, sio kigeugeu, mkiwa mnaongea wanasema zamani mambo yalikuwa hivi.
4. Melancholy, blue, water na compliance, hili ni kundi la watu wanaofuata utaratibu, huwezi kuwasikia wakichangia kwenye mjadala hadi pale tu taratibu zisipofuatwa, ni wachambuzi balaa na hawawezi kutenda jambo bila kuuliza taratibu zinasemaje, wako radhi kutumia muda wote kujadili taratibu za kazi kuliko kazi yenyewe. Duniani zaidi ya asilimia 80 watu wana mchanganyiko wa tabia za makundi mawili tu, asilimia 15 wana mchanganyiko wa makundi matatu na asilimia 5 ni kundi moja tu. Sasa ni muhimu kujitambua wewe ni nani, ziangalie tabia zako.
Tabia hizi zimefungwa katika makundi mawili, Introvert, yaani wakimya, hapa ni watu wa bluu na kijani, halafu na wale waongeaji hapa ni watu wa njano na nyekundu. Wengine wamesema ni bluu na nyekundu, hawana longolongo, pia njano na kijani hawa ni kazi na bata.
Nihitimishe kwa kusema, maisha tunayoishi ni matokeo ya watu waliotuzunguka na tabia zetu. Ukijua tabia za waliokuzunguka na kujua tabia yako basi utakuwa umetegua kitendawili.
Kwa kuwa hizi tabia ziko wazi na zinaunda aina nne za watu duniani, napenda kukujulisha namna itakavyozitumia ndivyo utakavyofanikiwa, wateja wako wa aina nne, wafanyakazi wako wa aina nne, kadhalika wachungaji, viongozi.
Ndiyo, wagonjwa wako wa aina nne na madaktari, hizi sifa za tabia zimefungamanishwa na utu wetu. Ndiyo, hakuna mkamilifu ila mapungufu nayo yako ya aina nne pekee. Ni muhimu kila mmoja kujijua na kuwajua wengine kisha kutumia mbinu kadhaa kujimudu na kuwamudu wengine.