Aina tano za saratani zinazosumbua zaidi Kanda ya Ziwa

Dodoma. Serikali imetaja aina tano za saratani zinazoongoza Kanda ya Ziwa, ambazo ni saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake, kibofu cha mkojo, damu, macho na figo.

Hayo yamesemwa leo, Jumatatu, Aprili 14, 2025, na Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel, akiwa bungeni wakati akijibu swali la msingi la mbunge wa Viti Maalumu, Kabula Shitobela.

Mbunge huyo aliuliza ni lini Serikali itatoa majibu ya tafiti zilizofanywa Kanda ya Ziwa, ili kubaini visababishi vya saratani iliyokithiri.

Dk Mollel amesema Serikali imefanya utafiti wa kina nchi nzima kwa lengo la kusaidia kutambua saratani zinazoongoza katika Kanda ya Ziwa.

Amesema katika utafiti huo wamebaini kuwepo kwa matatizo katika maeneo hayo matano, na juhudi zinaendelea ili kupambana na tatizo hilo.

“Wataalamu wamekusanya sampuli za damu 9,600 za watu ambao hawana saratani ili kulinganisha na sampuli za damu za wenye saratani. Utafiti huu utasaidia kubaini chanzo cha hizo saratani,” amesema Naibu Waziri.

Kwa mujibu wa Dk Mollel, kwa sasa bado utafiti unaendelea, na visababishi vinavyosemwa bado ni nadharia tu, kutokana na shughuli za kijamii katika maeneo husika.

Amesema hadi sasa, mpango wa kudhibiti ongezeko umejikita katika kutoa elimu ya afya kuhusu viashiria vinavyodhaniwa, pamoja na kuzingatia mkakati wa kitaifa wenye maeneo saba yaliyoainishwa ili kudhibiti viashiria vya saratani.

Akijibu maswali ya nyongeza kutoka kwa wabunge Stella Manyanya na Ritha Kabati, amesema Serikali imekuwa na utaratibu wa kusaidia wananchi wasiokuwa na uwezo, na kwa kipindi cha hivi karibuni, ilikuwa imetumia Sh667 bilioni kulipia matibabu.

Kuhusu malipo ya madaktari bingwa, amesema hakuna daktari ambaye halipwi fedha zake kwa kutoa huduma za kibingwa kwa kundi hili.

Hata hivyo, uchunguzi wa awali uliofanywa na Taasisi ya Aga Khan kwa kushirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando (BMC), pamoja na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), kuanzia Desemba 2020 hadi Septemba 2023, ulionesha kati ya watu 800,000 waliofanyiwa uchunguzi, watu 30,000 wana saratani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *