Ahueni bei za Petroli, dizeli zikipungua

Dar es Salaam. Hatimaye watumiaji wa vyombo vya moto watapata ahueni na kupungua kwa kiasi cha fedha wanachotumia katika kununua mafuta baada ya bei zitakazotumika katika Mei kushuka.

Bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli hapa nchini zitaanza kutumika leo Jumatano, Mei 7, 2025 kwa mujibu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Mafuta (Ewura).

Kushuka kwa bei hii ni sawasawa na matarajio yaliyokuwa yamewekwa na Chama cha Waagizaji na Wasambazaji Mafuta Tanzania (Taomac), ikiwa ni baada ya Serikali kusaidia kutatua changamoto ya upatikanaji wa fedha za kigeni iliyokuwa ikiwakabili na kufanya bei za mafuta kuongezeka mfululizo kati ya Januari hadi Aprili mwaka huu.

Hili linashuhudiwa wakati ambapo pia gharama za uagizaji mafuta zimepungua kwa wastani wa asilimia 22.41 kwa mafuta ya petroli, asilimia 4.78 kwa mafuta dizeli na hakuna mabadiliko kwa mafuta ya taa katika Bandari ya Dar es Salaam.

Katika Bandari ya Tanga hakuna mabadiliko na katika bandari ya Mtwara zimepungua kwa wastani wa asilimia 34.81 kwa mafuta ya petroli na dizeli.

Kufuatia hilo sasa watu wa Dar es Salaam watanunua lita moja ya mafuta ya petroli kwa Sh2,947 kutoka Sh3,037 iliyokuwa ikiuzwa Aprili 2025, huku dizeli ikifikia Sh2,868 kutoka Sh2,936 mwezi uliopita.

Kwa upande wa mafuta ya taa ya rejareja yaliyopitia katika bandari ya Dar es Salaam yataendelea kununuliwa kwa Sh3,053 kama ilivyokuwa mwezi uliotangulia.

Petroli iliyopitia bandari ya Tanga sasa yatauzwa Sh2,994 kwa lita kutoka Sh3,083 iliyokuwapo Aprili mwaka huku dizeli ikiuzwa kwa Sh2,914 kutoka Sh2,982.

Tofauti na maeneo mengine, watumiaji wa mafuta ya petroli inayopitia bandari ya Mtwara wao watalazimika kuongeza fedha zaidi kwani sasa lita moja watanunua kwa Sh3,020 kutoka Sh3,109.

Hata hivyo kwa wale wa dizeli watapata ahueni kidogo kwani sasa watanunua lita moja kwa Sh2,940 kutoka Sh2,958 iliyokuwapo mwezi uliotangulia. Mafuta ya taa yakisalia Sh3,125 iliyokuwapo Aprili.

Kushuka kwa bei hizi Tanzania, kunaenda sambamba na ile ya soko la dunia ambapo taarifa inaonyesha kuwa bei kikomo kwa Mei 2025, zimepungua kwa asilimia 5.22 kwa mafuta ya petroli, asilimia, 5.21 kwa mafuta ya dizeli na asilimia 5.08 kwa mafuta ya taa mtawalia.

Wakati ambao dola ilitajwa kuwa sababu ya ongezeko la bei kati ya Januari hadi Aprili mwaka huu, taarifa hii ya Ewura imeonyesha kuwa wastani wa gharama za kubadilisha fedha za kigeni umepungua kwa asilimia 1.20.

Hiyo ni tofauti na ilivyokuwa Aprili mwaka huu ambapo kulikuwa na ongezeko la wastani wa gharama za kubadilisha fedha za kigeni kwa asilimia 1.91.

Ilitabiriwa bei kushuka

Alipozungumza na Mwananchi Aprili mwaka huu, Mkurugenzi Mtendaji wa Taomac, Raphael Mgaya alisema bei ya mafuta ingeanza kupungua mwezi huu baada ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kuhakikisha inapunguza makali ya dola.

“Kuanzia Desemba, Januari dola ilianza kuadimika na baadaye ikaanza kupanda jambo ambalo liliweka ugumu kwetu kama kampuni za uagizaji wa mafuta na ukiangalia tunayouza sasa tuliagiza Februari wakati ambapo dola imeanza kupanda, hivyo tunayoona leo ni matokeo ya hali ya nyuma,” alisema Mgaya.

Alisema jambo hilo lilifanya waagizaji kuathiriwa hasa Januari na Februari kwa baadhi ya kampuni kupata hasara jambo lililowasukuma kuitisha kikao cha pamoja kati yao, Ewura, BoT na Wizara ya Nishati na walikubaliana nini kinapaswa kufanywa.

“Ilionekana kuwa benki kuu itaingilia suala hili na kuhakikisha kunakuwa na dola za kutosha, angalau tunaona kuna ahueni kuanzia Februari yenyewe na Machi, sasa matokeo ya kilichofanyika ni kupungua  kwa bei za mafuta angalau Mei na Juni,” alisema Mgaya.

Pamoja na haya yote, Ewura imeendelea kuzisisitiza kampuni za mafuta kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani isipokuwa zisizidi kikomo, au kuwa chini ya bei iliyoruhusiwa kama zilivyokokotolewa kwa mujibu wa kanuni za Ewura za kupanga bei za mafuta za mwaka 2022.

Pia imevitaka vituo vyote vya mafuta kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana yakionesha bei za mafuta, punguzo, vivutio vya kibiashara vinavyotolewa na kituo husika.

“Pale ambapo inawezekana kuchagua, wateja wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta katika vituo vinavyouza kwa bei nafuu zaidi ili kushamirisha ushindani. Ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja,” imesema taarifa hiyo ya Ewura iliyosainiwa na Mkurugenzi Mkuu wake, Dk James Mwainyekule.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *