
Mechi 23 tu zimetosha kwa Simba kuamini kiungo wake fundi Jean Charles Ahoua ni mali inayotakiwa kulindwa ipasavyo na kuendelea kuvaa jezi ya timu hiyo.
Kiungo huyo aliyecheza mechi 15 za Ligi Kuu Bara msimu huu na nane za Kombe la Shirikisho Afrika, amefunga mabao manane kwenye mashindano hayo ndani ya nusu msimu huu pekee.
Kiwango hicho na namba zake zimemvutia kocha wa timu hiyo, Fadlu Davids ambapo amewaambia mabosi wake wahakikishe anaendelea kuwepo kikosini ikiwezekana apewe mkataba mpya haraka, licha ya kuwa ndiyo kwanza ametumika kwa miezi sita kati ya miaka miwili aliyosaini.
Taarifa kutoka ndani ya Simba zinasema kiungo huyo raia wa Ivory Coast, ameshaanza mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya yakifanywa na viongozi wa Simba na wasimamizi wake.
Mabosi wa Simba wamepata baraka za kocha Fadlu, ambaye ametaka kiungo huyo kupewa mkataba mrefu zaidi ili kusalia ndani ya klabu hiyo.
Mwanaspoti linafahamu kwamba awali ilifika ofa kutoka katika klabu moja ya nje ikimtaka kiungo huyo, lakini Fadlu aligoma kumuachia akisema staa huyo ni mmoja wa wachezaji wake muhimu kikosini.
“Hatutaki kuona mpaka anafikia mwaka wa mwisho wa mkataba wake akiwa bado hajaongeza mkataba mpya, ndiyo maana mazungumzo yameanza haraka baada ya kocha kuonyesha kumhitaji zaidi.
“Kocha ametupa baraka zake kwamba aongezewe mkataba na unajua hapo nyuma ilikuja ofa moja ya klabu ya nje kumtaka Ahoua na tulipomshirikisha kocha akakataa akisema hataki aondoke,” alisema bosi mmoja wa Simba na kuongeza:
“Sababu zake zilikuwa za msingi alituchambulia kiufundi kwa kuangalia namba zake, ukiondoa Ahoua utaona namna alivyo na mchango mkubwa kwa asisti zake na hata mabao akiwazidi viungo wote.”
Kiungo huyo alijiunga na timu ya Simba msimu huu akitokea Stella Club d’Adjamé ya kwao nchini Ivory Coast ambapo alisaini mkataba wa miaka miwili akiwa tayari ametumikia miezi sita na kubaki mwaka mmoja na nusu.