
MWANZONI mwa msimu huu, hakuna shabiki yeyote wa Simba aliyekuwa na imani na timu hiyo kufanya maajabu katika michuano ya ndani na ile ya kimataifa, lakini ghafla nyota wapya 13 akiwamo Jean Charles Ahoua na Leonel Ateba wame-badilisha upepo na mtu aliyehusika kuwaleta amefichua siri ya nyota hao.
Simba iliyokosa ubingwa wa Ligi Kuu Bara na muichuano ya Kombe la Shirikisho kwa misimu mitatu mfululizo, hai-kuchukuliwa kama ni timu itakayoleta ushindani katika Ligi Kuu na hata michuano ya CAF na hata mabosi wa klabu hiyo walikuwa wakijitetea wanajenga timu mpya ya kuleta ushindani baadae.
Hata hivyo, mambo yamebadilika ghafla kwa Simba kuwa timu pekee ya Tanzania kutinga hatua ya robo fainali ya michuano ya CAF, lakini ikiongoza pia msimamo wa ligi mbele ya Yanga, Azam na Singida BS, huku ikielezwa mafanikio hayo yanabebwa zaidi na siri ya nyota 13 wapya akiwamo Ahoua na Ateba.
Upo hivi. Unamkumbuka yule skauti mkuu wa Simba, Mels Daalder? Basi kama hujui ni jamaa bado yupo kazini na amevunja ukimya akifichua siri za kina Ahoua waliosajiliwa dirisha kubwa kabla ya dirisha dogo kuongezwa Ellie Mpanzu na kueleza ndio waliobeba mafanikio ya Wekundu hao kwa sasa.
Daalder ameanika kila kitu juu ya usajili wa kina Ahoua anayeongoza orodha ya wachezaji waliotoa mchango mkubwa kwa timu hiyo hadi sasa katika Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho Afrika, huku akidokeza kuwa, kuna mashine nyingine mpya zipo njiani kutua Msimbazi kwa msimu ujao.
Akizungumza na Mwanaspoti, Daalder alisema kati ya nyota 15 wapya wanaoendelea kuipaisha Simba msimu huu, majina 13 yamepita mkononi mwake akishirikiana na mabosi wa klabu hiyo.
Raia huyo wa Uholanzi alisema usajili mpya wa Simba ikiwa imetoka kutoka kapa kwa msimu wa tatu na ulihusisha watu wazito wa Wekundu hao akiwamo Bilionea wa klabu hiyo, Mohammed Dewji na shabaha ilikuwa kutafuta wachezaji vijana wenye uwezo na vipaji vya kuitumikia timu kwa muda mrefu.
Daalder alisema usajili huo ulilenga kuijenga timu na kurejesha makali baada ya kuyumba misimu mitatu na hatua ya kwanza ilikuwa ni Bilionea MO Dewji kusimamia shoo ikiongezwa nguvu na vigogo wengine, kitu ambacho kinatrajiwa pia kuboreshwa zaidi dirisha lijalo la usajili.
Alisema kazi ilifanywa kwa ufasaha na mashine zikatua na ndani ya muda mchache matunda yamenza kuonekana ikiwa-mo kwa Ahoua kuongoza orodha ya wafungaji mabao wa klabu kwa sasa akiwa na saba yakiwamo mawili ya CAF na tano Ligi Kuu, akifuatiwa na Ateba aliyefunga mabao matano ya Ligi na mawili ya Kombe la Shirikisho na asisti mbili, kila moja katika michuano hiyo.
Daalder aliongeza tayari kwenye kompyuta yake kuna mahitaji ya Kocha wa Simba, Fadlu Davids ambayo anaendelea kuifanyia kazi akizunguka mataifa mbalimbali wakitaka watu wazito tayari kwa mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msi-mu ujao, michuano wanayoipigia hesabu zaidi baada ya msimu huu kukwama kutokana na kumaliza nafasi ya tatu Ligi Kuu iliyopita na kuangukia Kombe la Shirikisho Afrika.
“Bado naendelea kuitumikia, nipo ndani ya mkataba na Simba tunaendelea kutafuta wachezaji bora kwa ajili ya Simba, naona timu inaendelea kufanya vizuri kwa mashindano ya ndani na hata yale ya Afrika,” alisema Daadler na kuongeza;
“Nafurahia namna wachezaji wanavyoendelea kuipigania Simba, unajua kwenye wachezaji 15 ambao tuliwasajili msimu huu kuna majina 13 yalipita katika usaili wangu nikishirikiana na viongozi wa klabu hii ni hatua nzuri kwetu sote.
“Hivi karibuni nilikwenda hadi Tunisia nikaona maendeleo ya kikosi, safari ya maboresho inaendelea unaona dirisha hili dogo tuliingiza mchezaji mmoja pekee Mpanzu (Ellie), kifupi huyu ni mchezaji ambaye tulikuwa tunamhitaji tangu dirisha kubwa la nyuma,” alisema Daalder na kuongeza;
“Kujenga timu unatakiwa pia kuwa na utulivu, kuna wakati unatakiwa kusajili kwa mahitaji maalum na siyo kila dirisha unaingiza wachezaji wengi lakini dirisha kubwa ndio tunaweza kuingiza wengine wenye uwezo mkubwa zaidi.
“Tunaamini tunaweza kuchukua ubingwa au kupata tiketi ya kurudi kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikiwa hivyo tutahitaji baadhi ya wachezaji wenye uwezo mkubwa zaidi kwa ukubwa wa mechi hizo tunaendelea kufanyia kazi mahitaji ya makocha.
Daalder alimpongeza MO na Bodi ya Wakurugenzi nzima ya Simba kwa namna walivyosimamia uundwaji wa kikosi hicho kwa msimu huu.
“Unakumbuka nilikwambia awali kuna changamoto ya kupata wachezaji bora zaidi na eneo kubwa ni bajeti ya fedha, wa-kati huu mashabiki wa Simba wampongeze sana MO Dewji na bodi yake nzima kwa kufanya maamuzi makubwa kuboresha bajeti ya usajili ambayo imekwenda kutupa hawa wachezaji ambao wanaendelea kufanya makubwa.
“Hii ni hatua ya kwanza tu uongozi wa Simba bado unataka kufanya makubwa zaidi kwa kutafuta wachezaji bora zaidi ndiyo maana unaona tunaendelea kupambana kutafuta wachezaji bora Afrika nzima na hata nje ya Afrika.”